Nav bar

Jumatatu, 19 Agosti 2024

RUKWA NAO WAREJESHA UVUVI WA ZIWA TANGANYIKA

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro Nyerere amewaongoza wananchi wa mkoa huo kwenye hafla ya ufunguzi wa shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika kwa upande wa mkoa huo iliyofanyika kwenye kata ya Kasanga Agosti 17, 2024.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa shughuli hizo Mhe. Nyerere ambaye alimwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mbali na kuwashukuru Wavuvi wa mkoa huo kwa uvumilivu wao wakati wote wa ufungaji wa ziwa hilo amewataka kuvua kwa kufuata sheria na taratibu ili kutunza rasilimali iliyopatikana.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede mbali na kuwaeleza wananchi wa mkoa huo umuhimu wa upumzishwaji wa Ziwa hilo, amewataka wavuvi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali wakati wote inapokuwa na kampeni inayolenga kulinda rasilimali za Uvuvi.

Akitoa Ushuhuda wa mavuno aliyopata baada ya ufunguzi huo, Mmoja wa wavuvi kutoka kijiji cha Kilewani Bw. Adam Pesambili amesema kuwa kwa usiku mmoja tu amefanikiwa kuvuna kiasi cha ndoo 60 za dagaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi Mil 4.5 tofauti na awali ambapo alikuwa hawezi kupata hata ndoo 2 kwa siku.

"Tunaomba Serikalo iendelee na mpango huu wa upumzishaji wa Ziwa kwa sababu tumeona manufaa yake" Ameongeza Bw. Pesambili.

Tukio hilo la Ufunguzi wa shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika mkoa wa Rukwa liliambatana na ugawaji wa makasha 70 ya kuhifadhia Samaki ambapo Wilaya ya Kalambo ilipata makasha 40 na Nkasi ilipata makasha 30.

Ufunguzi huo umefanyika ikiwa ni baada ya takribani miezi mitatu ya upumzishwaji wa Ziwa hilo ulioanza Mei 15, 2024.





PROF.SHEMDOE AFUNGA MAFUNZO YA WAVUVI KIZIMKAZI- ZANZIBAR

 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe jana tarehe 16 Agosti 2024 amefunga mafunzo ya wavuvi wadogo wadogo yaliyokuwa yanafanyika Zanzibar, Wilaya ya kusini Unguja katika Kijiji cha Kizimkazi.

Akifunga mafunzo hayo Prof.Shemdoe amesema kuwa Mafunzo hayo ni muhimu kwa Wavuvi hao kwasababu lengo lake kubwa ni kuwajengea uwezo Wavuvi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufugaji wa Samaki, Uchakataji wa Dagaa, Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi pamoja na Utunzaji wa mazingira ya bahari ili wazalishe kwa ufanisi na kujiongezea kipato.

Aidha, Prof. Shemdoe amesema kuwa anajua wavuvi wanachangamoto mbalimbali na ameahidi changamoto zote walizonazo wavuvi hao zitafanyiwa kazi kwa kuwa Serikali ya Awamu sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni sikivu na inawapenda Wavuvi.

Pia Prof.Shemdoe amesema kuwa anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanyia Sekta ya Uvuvi na Wavuvi kwa Ujumla, kwa sababu kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 tayari zaidi ya Boti 160 za kisasa za uvuvi zimeshakabidhiwa kwa vikundi mbalimbali vya Wavuvi hapa nchini.

Vilele, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Shemdoe amewambia wavuvi hao kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Wakati wa Tamasha la 9 la kizimkazi kwa Mwaka 2024 basi liambatane na mafunzo kwa wakazi wa Kizimkazi na Shehia zake Katika tasnia ya Uvuvi, Utalii, Ujasiriamali, Kilimo na kukuza sanaa.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) Dkt. Emmanuel Sweke ameishukuru Serikali kwa kuandaa mazingira bora na kuona uhitaji wa wavuvi mpaka kuandaa mafunzo hayo.

"Baada ya Mafunzo haya kukamilika, Serikali inategemea kuona wavuvi mnafanya uvuvi wenye tija na endelevu”. Alisema Sweke.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe alikutana na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar na kujadiliana nao mambo mbalimbali ya Sekta ya Uvuvi kwa Ujumla, Viongozi hao ni Mhe.Shaabani Othman, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Bw. Zahor Kassim El-Khaousy.





UHUSISHWAJI WA SEKTA BINAFSI KATIKA UKUZAJI VIUMBE MAJI NI JAMBO LA MSINGI - EMELDA

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya Uvuvi, Bi. Emelda Adam ame uhusishwaji wa sekta binafsi katika tasnia nzima ya ukuzaji viumbe maji ni jambo la msingi kwa sababu kwa sababu itaongeza mnyororo wa thamani.

Akizungumza, leo Agosti 15, 2024 mkoani Mwanza katika kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji lililoudhuliwa na nchi 18 za Afrika, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya Uvuvi, Bi. Emelda amesema ili nchi zinyanyuke kutoka hatua moja kwenda nyingine lazima ishirikishe sekta binafsi .

"na itambulike kwa sasa, ukuzaaji viumbe maji unachangia takribani pato la taifa kwa asilimia 50 kwenda 51 ya samaki wengi ambao wanazalishwa duniani." amesema Bi. Emelda

Aidha, Bi. Emelda alisema kwa Tanzania kwa sasa katika swala la ukuzaji viumbe maji tupo katika asilimia 10 na bado tuna nafasi ya kusogea mbele zaidi kama tutaendelea kuhusisha sekta binafsi katika swala zima la myororo wa thamani katika ufugaji viumbe maji, ikiwa pamoja na kupagikana kwa chakula cha kulishia samaki pamoja na mbegu bora za samaki.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Ambakisye Simtoe amesema duniani sahivi, samaki wanaofugwa wanachangia karibia asilimia 50 ya upatikanaji samaki duniani japo kwa upande wa Tanzania bado tupo chini.

Vilevile Bw. Simtoe amesema wataalamu wamekutana hapa katika kongamano hili la ukuzaji viumbe maji ili kujadili jinsi ya kuongeza shughuli za ukuzaji viumbe maji.

"kwa upande wa Tanzania tumeangalia fursa tulizonazo kama mito na maziwa katika kufanya shughuli za ufugaji samaki kwa njia ya vizimba japo moja ya changamoto zilizoonekana ni pamoja na upatikanaji wa vyakula vya kulishia samaki na mbegu bora za samaki" amesema Bw. Siimtoe

Mratibu wa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Etienne Hinrichsen amesema hili ni kongamano la tatu, la kwanza lilifanyika Kenya, mwaka huu tumefanya hapa Tanzania na kongamano hili aliishii hapa tu, kwani mwakani mwezi juni kongamano hili litafanyika nchini Uganda.

Bw. Hinrichsen aliendelea kusema kuwa watu wengi wameshwawishika na hili kongamano, na hii italeta chachu kubwa katika nchi mbalimbali katika swala la ukuzaji viumbe maji na kuzalisha zaidi.

 


Mratibu wa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Etienne Hinrichsen (kulia), akimpa tunzo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji na Afisa Kiungo wa Mradi wa TRUEFISH kwa Upande wa Tanzania, Dkt. Imani Kapinga (kushoto), ya kutambua mchango wake katika kuandaa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji, Agosti 15, 2024, Mwanza.








TANZANIA, CHINA KUIMARISHA BIASHARA YA MIFUGO NA UVUVI

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Forodha kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Yu Jianhua kujadiliana namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara baina ya nchi hizo mbili hususan kwenye sekta za mifugo na uvuvi.

Waziri Ulega amekutana na waziri Jianhua jijini Dar es Salaam mapema leo Agosti 14, 2024.

Akiongea katika mkutano huo, Waziri Ulega amesema kuwa mkutano wao huo ni muendelezo wa mkutano baina ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jiping ambapo walikubaliana masuala kadhaa ya kibiashara baina ya nchi hizo. 

“Mkutano wetu wa leo unahusu kufanya majadiliano ya namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara kwenye sekta za mifugo na uvuvi ikiwa ni muendelezo baada ya mkutano baina ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Ji Ping”, amesema

Amesema fursa ya biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi nchini China bado ni kubwa na hivyo wanaendelea kujipanga kutumia kila aina ya fursa hizo kushamirisha biashara ili kuinua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Aliongeza kwa kusema kuwa kupitia mikutano hiyo wanayoendelea kuifanya, Waziri Ulega anatumaini kuwa nchi hizo zitaendelea kutatua changamoto za kibiashara na kuendelea kuboresha ushirikiano kwa mbinu na nguvu zaidi ili wananchi wa pande zote mbili waweze kupata manufaa.

Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa, katika kuhakikisha biashara ya mifugo kutoka Tanzania inaaminika duniani, wamejipanga kufanya Kampeni kubwa ya kuchanja mifugo nchi nzima ili kuiepusha na magonjwa na kuifanya iwe bora kwa biashara ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Forodha wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe.Yu Jianhua amesema mahitaji ya kibiashara ya mazao ya samaki na nyama ni makubwa hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo ili kunufaika nazo.


Waziri wa Forodha wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe.Yu Jianhua akimkabidhi picha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wao wa kujadili namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara baina ya nchi hizo mbili hususan kwenye sekta za mifugo na uvuvi uliofanyika jijini Dar es Salaam mapema leo Agosti 14, 2024.




MNYETI AWATAKA WADAU WA UVUVI WAZALISHE SAMAKI KWA NJIA YA KISASA

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wadau wa uvuvi kuzalisha samaki kwa njia ya kisasa ili kuongeza wingi wa samaki kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu kwani kwa sasa kuna upungufu wa samaki.

Akizungumza, leo Agosti 13, 2024 mkoani Mwanza katika kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji lililoudhuliwa na nchi 18 za Afrika, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mnyeti amesema serikali itaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali ili wajitokeze kwa wingi na kufuga kwa teknolojia.

"tutaendela kuhamasisha wadau mbalimbali wajitokeze kwa wingi kwani vizimba vipo vingi vinavyohitaji wadau na tunawakaribisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali waje wawekeze kwa sababu maeneo ya kufugia samaki yapo na vizimba vipo." amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, Mhe. Mnyeti alisema awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuleta mabadiriko na maboresho makubwa, na ndio mana miezi nane iliyopita Mhe. Rais alikuja kukabidhi vizimba na boti za uvuvi hapa ziwa Viktoria.

Mhe. Mnyeti amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), inatoa mikopo isiyo na riba kwa hiyo wadau wa uvuvi waje kukopa kwa wingi ili kuzalisha samaki kwa wingi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla amesema ukuzaji viumbe maji ni moja ya fursa katika Uchumi wa Bluu, na juhudi hizi zimeleta ongezeko la uzalishaji, ambapo katika mwaka 2023 jumla ya tani laki tatu za mazao ya ukuzaji viumbe maji yalizalishwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kati ya hizo takribani tani laki moja na ishirini zilizalishwa hapa nchini Tanzania na hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika hizi nchi kwa kutoa ajira, lishe na kusaidia katika ukuaji wa uchumi katika nchi.

Vilevile Dkt. Madalla amesema juhudi hizi za uzalishaji kwa upande wa Tanzania zimetokana na serikali kuwezesha kuwepo kwa vituo vya ukuzaji viumbe maji kwa lengo la kutoa huduma za ugani na kuhamasisha mbinu bora za ukuzaji viumbe maji.

Mratibu wa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Etienne Hinrichsen amesema hatuna namna zaidi ya kukuza samaki kwa kutumia njia za vizimba kwa sababu kwa sasa maziwa yetu na mito hayana samaki wa kutosha kulisha idadi kubwa ya watu.

Bw. Hinrichsen aliendelea kusema inabidi kufanya kilimo cha ukuzaji viumbe maji na kuzalisha kwa wingi kwa lengo la kukidhi mahitaji.








TEKNOLOJIA YA JUNCAO SULUHISHO MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega  amesema teknolojia ya uzalishaji wa malisho aina ya Juncao ambayo imeanza kutumika hapa nchini ni suluhisho la  kumaliza changamoto za malisho ya mifugo na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

Waziri Ulega amesema  hayo wakati alipouongoza ugeni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) wakiwakilishwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo,  Earle Courtenay Rattray kutembelea Shamba la Serikali la Mbegu za malisho aina ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani leo Agosti 9, 2024.

“Katika shamba hili la serikali la Vikuge kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka huu wa 2024 tumeshapanda majani ya juncao ekari 21, mbegu zilizozalishwa ni Kilo 178,262, huku zaidi ya  wakulima 957 wakishiriki kulima majani hayo kwa hatua tofautitofauti”, amesema Ulega

Aidha, Waziri Ulega ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa mchango wao mkubwa katika kuwajengea uwezo wataalam mbalimbali wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuifahamu teknolojia hiyo ya ulimaji majani ya Juncao huku akisema kuwa teknolojia hiyo ni chachu katika kumaliza changamoto za malisho ya mifugo na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

“Teknolojia hii tumeichukua kama ni suluhu ya mahitaji ya malisho katika taifa letu”, ameongeza

Kwa upande wake, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa (UN),  Balozi Earle Courtenay Rattray amefurahishwa na maendeleo ya teknolojia hiyo hapa nchini huku akimpongeza  Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utayari wa kuipokea teknolojia hiyo ambayo inakwenda kuwa moja ya suluhisho ya changamoto ya malisho na migogoro ya wakulima na wafugaji hapa.

Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimueleza jambo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Earle Courtenay Rattray wakati walipotembelea Shamba la Serikali la Mbegu za malisho aina ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani leo Agosti 9, 2024.


Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimueleza jambo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Earle Courtenay Rattray (kushoto kwake) wakati walipotembelea Shamba la Serikali la Mbegu za malisho aina ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani leo Agosti 9, 2024.



NG'OMBE WA KITULO WAMSHANGAZA RIDHIWANI KIKWETE


◼️ Mnyeti agusia mpango wa Vizimba Ziwa Nyasa 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameshangazwa na ukubwa wa ng'ombe waliopo kwenye ranchi ya Kitulo mkoani Njombe.

Tukio hilo limetokea Agosti 8, 2024 jijini Mbeya kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya kimataifa ya wakulima kwa upande wa kanda ya Nyanda za Juu kusini ambapo Mhe. Kikwete alikuwa mgeni rasmi wa tukio hilo akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

"Pale kwetu sisi ni wafugaji tena wafugaji wa kisasa na nilikuwa ninasema nina ng'ombe mkubwa sana lakini leo nimekutana na ng'ombe mwenye uzito wa kilo 900 pale kwenye banda la Shamba la Mifugo la Kitulo, Hongera sana Mkuu wa Mkoa wa Njombe maana shamba hili lipo mkoani kwako" Amesema Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete ametumia jukwaa hilo kutoa rai kwa wafugaji wengine kufuga kisasa ili ufugaji wao uwe na tija na kubadili maisha yao kwa ujumla.

"Nimesikia pia huko Dodoma kuna ng'ombe anatoa lita 50 za maziwa kwa siku na kwa kuwa wameongeza siku za maonesho lazima nifike huko pia nikashuhudie ili nami niendelee kujifunza" Ameongeza Mhe. Kikwete.

Katika taarifa yake ya utangulizi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ameweka wazi kuwa Wizara yake imetenga fedha ya kufanya utafiti wa ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba kwa upande wa Ziwa Nyasa ili kuongeza wigo wa uzalishaji wa samaki katika ziwa hilo.

"Ufugaji huu ni ufugaji wa kisasa na dunia ndo imefikia huko na tayari umeanza kufanyika Mwanza na kwa upande wa Ziwa Tanganyika hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kuomba Vizimba vya kufugia samaki vilivyotolewa kwa wingi na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Aidha Mhe. Mnyeti amegusia mikakati mingine ya Serikali inayolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa samaki nchini ikiwa ni pamoja na kupumzisha maziwa huku akitoa mfano wa mafanikio yaliyopatikana baada ya kupumzishwa kwa Ziwa Tanganyika ambalo linatarajiwa kufunguliwa Agosti 15, 2024.




RAIS SAMIA ATOA BIL 1.1 KWA VIJANA WA BBT, KUFUGA KWA TIJA


Na. Edward Kondela

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhi Shilingi Bilioni 1.1 kwa vikundi 25 vya programu ya “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT) ili viweze kufuga kwa tija.

Kabla ya kukabidhi mfano wa hundi hiyo kwa baadhi ya wanufaika wa programu ya BBT, kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma (08.08.2024), Rais Samia ameonesha kufurahishwa namna vijana wanavyoendelea kunufaika kupitia sekta za mifugo na uvuvi, baada ya kutembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Rais Samia amewataka vijana kutumia vyema fursa zinazojitokeza ili waweze kujiinua kiuchumi na kutoa elimu kwa wenzao ambao bado hawajachangamkia fursa hizo hususan katika sekta za mifugo na uvuvi.

Wakati Rais Samia akikabidhi mfano wa hundi hiyo ya Shilingi Bilioni 1.1 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema fedha hiyo ni mkopo wenye masharti nafuu na kwamba serikali itaendelea kutoa mikopo kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.

Akihutubia wananchi walioshiriki kilele cha Maonesho ya Nane Nane ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma, Rais Samia amesema serikali imejipanga kujenga uchumi jumuishi unaowainua wananchi wote na kuwawezesha kunuifaika ipasavyo kupitia uwekezaji unaofanywa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Amefafanua kuwa serikali imeongeza bajeti kwa ajili ya kilimo, mifugo na uvuvi ili uwekezaji huo ulete mageuzi makubwa kwa kuongeza maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbolea, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, kuimarisha huduma za ugani kuboresha miundombinu ya kuhudumia mifugo pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani, chanjo, majosho na masoko.

Aidha, amesema serikali imeendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya mifugo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi, ukuzaji wa viumbe maji na utafutaji wa masoko na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wavuvi na wafugaji.

Kwa upande wake Waziri wa Miugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo, amesema kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 wizara imetengewa bajeti ya Shilingi Bilioni 465 ambayo ni maradufu ya bajeti iliyokuwa ikipata awali, ambazo zitawezesha kutatua changamoto za wafugaji na wavuvi.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha, serikali imeandaa kampeni kubwa ya kitaifa ya chanjo kwa ajili ya mifugo pamoja na kuitambua mifugo hiyo, ili kuhakikisha mifugo inakuwa na afya bora na kuleta tija kwa mfugaji.

Pia amesema imepanga kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya boti za uvuvi zisizopungua 450 na vizimba 900 kwa ajili ya kufugia samaki ili kukuza sekta hiyo kwa kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi Bilioni 1.1 kwa vikundi 25 vya programu ya “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT), ili kuviwezesha kufuga kwa tija, kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (08.08.2024)





MTAKA AKOSHWA NA KAZI ZA WIZARA NANENANE MBEYA

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau wake kupitia maonesho ya mwaka huu ya  kimataifa ya Kilimo (NaneNane) kwa upande wa kanda ya Nyanda za Juu kusini yanayoendelea mkoani Mbeya.

                   Mhe. Mtaka ametoa pongezi hizo mara baada ya kufika kwenye mabanda ya Wizara hiyo                       ambapo alioneshwa kuvutiwa zaidi na bidhaa ya viatu vinavyotengenezwa kutokana na                            ngozi inayozalishwa hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya nyanda za juu kusini ambaye pia ni Mratibu wa maonesho hayo kwenye kanda hiyo Bw.Edwin Chang'a amemueleza Mhe. Mtaka kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepeleka teknolojia mbalimbali katika maonesho hayo ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu ufugaji bora wa ng'ombe bora wa maziwa na nyama na aina mbalimbali za malisho ya Mifugo.

 

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI INAENDELEA KUTOA ELIMU YA UBORESHAJI MBARI ZA MBUZI WA KIENYEJI KWA WAFUGAJI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti a  Mifugo (TALIRI) inaendelea kutoa elimu ya uboreshaji wa mbari za mbuzi wa kienyeji kwa Wafugaji kupitia maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea kufanyika Kanda ya ziwa Magharibi katika Viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza.

Akitoa elimu hiyo kwa wadau waliotembelea kwenye banda la Wizara hiyo Agosti 06,2024. Afisa Mifugo wa Taasisi hiyo Bw. Amos Kisusi amesema madume ya mbuzi 15 ya Boer kutoka Afrika kusini yametumika kuboresha mbari za mbuzi 450 wa kienyeji waliotolewa na serikali. 

Bw. Kisusi amesema uboreshaji wa Mbari za Mbuzi aina ya boer ni moja ya miradi ya wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao unayooneshwa kupitia viwanja vya maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi Nane Nane jijini Mwanza, ambapo ulianza mwaka 2021 kwa ujenzi wa mabanda bora ya kuhifadhi Mbuzi aina ya Boer.

Aidha, Mbuzi 15 aina ya Boer walipokelewa 2022 kutoka nchini Afrika kusini kwa gharama ya shilingi milioni 42 na wakaanza kupanda majike wa kienyeji na hadi kufikia kuanza kuzaa mwezi Februari, 2024 kupata mbuzi chotara.

Pia, Mbuzi chotara mpaka sasa wanaendelea kukuzwa chini ya uangalizi wa TALIRI huku taratibu za upatikanaji wa vibali vya usambazaji wa mbuzi hao kwa wafugaji nchini kutoka wizarani zikiendelea.

Timu ya wataalamu  kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania Kanda ya ziwa wanaendelea kutoa elimu mbalimbali ya uzalishaji, Utafiti na ufugaji bora wa Mifugo.






Jumanne, 6 Agosti 2024

FETA YATOA ELIMU YA MFUMO WA KUZALISHA SAMAKI NA MAZAO "AQUAPONICS" NANENANE.

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) yatoa elimu ya mfumo wa kuzalisha samaki na Mazao kwa wadau waliotembelea kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea kufanyika Kanda ya Ziwa Magharibi, katika Viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza.

Akitoa elimu hiyo Agosti 04.2024, kwa wadau waliotembelea kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkufunzi wa Wakala hiyo kutoka Kampasi ya Nyegezi (Mwanza), Bw. Mukama Ndaro aliwaelezea mfumo huo unavyoleta faida kwa Wafugaji.

Bw. Ndaro ameelezea kuwa uchafu unaozalishwa na samaki unakuwa mbolea kwa mazao, na Mazao yanayasafisha maji kwa kuchuja mbolea (mkojo) inayotokana na samaki na kufanya maji hayo yawe masafi kwa matumizi ya ufugaji wa samaki tena. 

"Mchakato wa kuchuja mbolea au uchafu unatokana na samaki na chakula hufanywa kwa msaada wa Viorwa aina ya bakteria (Nitrobacter na Nitrosomonas)  Viorwa hao hugeuza Amonia kuwa Nitrite ambazo ni sumu kwa samaki Kisha Nitrite hugeuza kuwa Nitrate ambayo ni mbolea kwa mimea" amesema Bw. Ndaro.

Aidha, ameendelea kubainisha faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na matumizi bora ya eneo, matumizi bora ya maji, uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha usalama wa chakula (mazao na samaki)

Naye mhitimu wa Mafunzo ya Uvuvi  kutoka  Kampasi ya Nyegezi, Bw. Bryton  Okendo amesema kwa upande wake amenufaika na Mafunzo hayo ya mfumo wa "Aquaponics" kwa kupata elimu ya kuweza kujiajiri na kujitegemea kiuchumi, amesema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Maonesho hayo.

Pia, Wakala hiyo inaendelea kutoa elimu ya teknolojia mbalimbali ya ufugaji samaki kama teknolojia ya ufugaji samaki kwenye vizimba, teknolojia totoleshi (hatchery technology) teknolojia ya ufugaji kwenye matanki, Uzalishaji na Ukuzaji wa samaki wa mapambo, utengenezaji wa boti za "fiberglass" teknolojia ya usindikaji na kuongeza thamani mazao ya samaki.





WATAALAMU WAASWA KUPELEKA TEKNOLOJIA YA MIFUGO NA UVUVI VIJIJINI

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amewahasa wataalamu wa mifugo na uvuvi kupelekea na kufundisha teknolojia ya mifugo vijijini ili kuwapa wafugaji elimu ya kutosha kuhusu ufugaji wa kisasa kwa lengo la kuleta tija katika sekta hiyo.

Akizungumza, leo Agosti 4, 2024 mkoani Dodoma alipotembelea kwenye Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa yanayofanyika Kitaifa mkoani Dodoma katika mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Senyamule amesema wataalamu wahakikishe teknolojia hii inawafikia wadau wote wa mifugo na uvuvi, ususani maeneo ya vijijini.

"wataalamu wachukue hatua ya kwenda kwenye makundi ya wafugaji ili kwenda kuwaelimisha kuhusu teknolojia mpya ya ufugaji na kuhakikisha inawafikia" amesema Mhe. Senyamule

Aidha, Mhe. Senyamule alisema serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya Mifugo na Uvuvi kwani ameshuhudia teknolojia mbalimbali na nzuri katika mabanda ya Mifugo na Uvuvi.

Mhe. Senyamule alisema ata sekta binafsi pia wamepokea mabadiriko hayo ya kiteknolojia, ususani upande wa vijana wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambao wanatumia teknolojia hizi kama ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Vilevile Mhe. Senyamule ametoa wito kwa wadau wote wa Mifugo na Uvuvi  kutumia fursa hii ya maonesho haya ya nanenane ili kuweza kujifunza na kupata ufahamua juu ya teknolojia hii ya mifugo na uvuvi.







RC DENDEGO AWAKUMBUSHA WAFUGAJI KUFUGA KWA TIJA NA KIBIASHARA


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amewakumbusha wafugaji wote hapa nchini Tanzania kufuga kwa tija na kibiashara kwani ufugaji ni utajiri.

Akizungumza, leo Agosti 5, 2024 mkoani Dodoma alipotembelea eneo la arena ya mifugo katika maonesho ya nanenane ya Kimataifa yanayofanyika Kitaifa Mkoani Dodoma kushuhudia mifugo mbalimbali ikishindanishwa kwa ubora, Mhe. Dendego amesema wafugaji wanatakiwa kufuga kibiashara ili kuleta tija na kuongeza ajira ili kuondokana na umasikini na kuchangia uchumi wa nchi na wa mfugaji mmoja mmoja.

"serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya juhudi katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/25 yenye malengo ya kuendeleza Sekta ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo" amesema Mhe. Dendego

Aidha, Mhe. Dendego alisema shughuli hizi ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo ili kukuza kipato na ajira kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mhe. Dendego alisema kwa mwaka 2022 ukuaji wa sekta ya mifugo umefikia asilimia 5, ukichangia kwa asilimia 7.0 kwenye pato la taifa.

Vilevile Mhe. Dendego amesema ili kuhakikisha tija inapatikana katika sekta ya mifugo, Wizara imeweka vipaumbele vya kuimarisha upatikanaji wa maji, malisho na vyakula vya mifugo, kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, kuimarisha afya za mifugo, kuboresha huduma za ugani, kuimarisha huduma za utafiti na mafunzo ya taaluma za mifugo, kuimarisha masoko, kuwezesha thamani ya mazao ya mifugo na kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema lengo la maonesho na mashindano haya ya mifugo ni kuwahakikishia wafugaji kuwa matumizi ya teknolojia ya ufugaji yanawezekana katika mazingira ya kufuga kwenye maeneo wanayoishi na kushawishi matumizi ya teknolojia ya ufugaji bora.

Mh. Mnyeti alisema wizara inamkakati wa kufundisha teknolojia ya ufugaji kwa wafugaji, na pia wizara imejipanga kufanya zoezi la chanjo za mifugo, kujenga miundombinu muhimu ya mifugo ikiwemo majosho na miundombinu ya maji, uboreshaji wa mbali za mifugo, kuimarisha mashamba ya wizara, kuimarisha mbegu za malisho, uanzishaji wa mashamba darasa ya malisho katika halmashauri mbalimbali nchini, kuimarisha huduma za utafiti na ugani, kuhamasisha sekta binafsi na kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya mifugo, pamoja na kuendeleza programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).

Akiongea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema leo ameshukuru kwa kuona paredi ya gwaride ya mifugo ambalo ni jambo la kipekee na inathibitisha kabisa utajiri katika sekta ya mifugo.

Mhe. Senyamule amesema mifugo ni kati ya sekta kubwa zinazotegemewa na wananchi wengi katika swala la uchumi, chakula, kipato, nguvu kazi, mbolea na kama fahari.







Ijumaa, 2 Agosti 2024

PROF. SHEMDOE AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KWENYE MIFUGO NA UVUVI


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, amehimiza matumizi ya teknolojia ya Mifugo na Uvuvi kwa wafugaji ili kuweza kuleta tija katika uzalishaji.

Akizungumza, leo Agosti 2, 2024 mkoani Dodoma alipotembelea kwenye Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa yanayofanyika Kitaifa mkoani Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Shemdoe amesema kuwa katika haya maonyesho kuna teknolojia nzuri sana ya ufugaji na uvuvi kwa hiyo wafugaji na wavuvi wote waje kuchukua teknolojia hii ili kuboresha mifugo yao.

"mnakumbuka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa jana alisema  maana halisi ya haya maonesho ni kwamba wakulima waje kuchukua teknolojia" amesema Prof. Shemdoe

Aidha, Prof. Shemdoe alisema haya maonesho ya nanenane ni kwa mara ya kwanza yanaadhimishwa kimataifa hapa mkoani Dodoma na ameweza kutembelea mabanda mbalimbali ya mifugo na uvuvi pamoja na kilimo ikiwa na sehemu ya vipando.

Vilevile Prof. Shemdoe ametoa wito kwa watanzani kutumia siku nane kutembelea maonesho haya ya nanenane ili kujionea teknolojia mbalimbali zinazopatikana katika maonesho haya ambazo zitawasaidia katika shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, amemshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutembelea maonesho hayo ya nanenane.

Vilevile Mhe. Jabir amesema, maonesho haya yatawasaidia wananchi wa Tanzania kubadirisha maisha yao kwa kuongeza kipato na kukuza uchimi wa nchi, kwani elimu wanayoipata kwenye maonesho haya yatakuwa na maboresho na mapinduzi makubwa kwao. 









Alhamisi, 1 Agosti 2024

MAJALIWA ARIDHISHWA NA NANENANE DODOMA


Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na mikoa ya Dodoma na Singida imefanya maajabu ya kipekee katika maonesho ya nanenane ya mwaka 2024 ikiwa tofauti na miaka mingine ya maonesho hayo kwa kuboresha zaidi miundombinu na teknolojia mpya na za kisasa.

Akizungumza, leo Agosti 1, 2024 mkoani Dodoma katika Ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa Kanda ya Kati - Dodoma, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Kilimo ikishirikiana na menejimenti ya mkoa wa Dodoma na Singida, zimefanya vizuri katika maandalizi ya nanenane kwa mwaka 2024 na ameridhishwa na maandalizi ya maonesho hayo.

"mwaka huu Wizara zetu na mikoa ya Dodoma na Singida, zimefanya maajabu makubwa hapa viwanja vya nanenane Nzuguni, hii ni hatua kubwa sana inayohitaji pongezi toka kwenu kwa sababu hii imevunja rekodi ya maonesho yote ya miaka mingine." amesema Mhe. Majaliwa

Aidha, Mhe. Majaliwa alisema lengo la maonesho haya ya nanenane ni kutoa fursa kwa wafugaji, wavuvi, wanaushirika, wajasiriamali na wasindikaji, kwenda kujifunza teknolojia mbalimbali kutoka kwa wadau wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi ambapo pia ni Sekta binafsi na wao pia wapo pamoja na wataalamu waliopo serikalini wanaonyesha umuhimu wa sekta ya Mifugo na Uvuvi, Ushirika na ujasiriamali unavyoleta tija kwenye maisha ya kila mtu, lakini pia katika maonesho haya yanatoa nafasi kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa kuzidi kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kuuza bidhaa ambazo zinakuja kuuzwa katika eneo hili.

Mhe. Majaliwa alisema maonesho haya ni ya 31 toka kuanzishwa kwake, na yamekuwa yanaboreshwa kila mwaka na hii ni fursa kwa wadau wote wa Mifugo na Uvuvi na kusisitiza kuwa Nitoe rai kwa watanzania wajitokeza kwa wingi katika maonesho haya ili waende wakaone maonesho ya bidhaa mbalimbali na teknolojia mbalimbali zinazooneshwa katika viwanja hivyo.

Vilevile Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imekuwa inachukua hatua mbalimbali katika kutekeleza mipango na mikakati mahususi ya kihakikisha Sekta muhimu za Mifugo, Uvuvi na Kilimo zinaendelea kuwa muhimili muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuleta maendeleo kwa wananchi kwani zimekuwa zikishangia kwa ukubwa pato la taifa kwani kwa mwaka 2023/24 Sekta hizi zilichangia asilimia  26.5 ya pato la taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, amesema Wizara imeandaa mashindano ya Mifugo ambayo ina lengo la kuwahakikishia wafugaji kuwa matumizi ya teknoloji yanawezekana katika mazingira ya kufuga katika maeneo wanayoishi na kushawishi matumizi ya teknolojia ya ufugaji bora.

Vilevile Mhe. Mnyeti amesema, maonesho haya uwezesha wafugaji kujenga imani na wataalamu na ugani kwa kuhakikisha kuwa ushauri wao ni wa thamani na wenye tija, pia kusaidia kujenga imani kwa wafugaji kuhusiana na matumizi sahihi ya teknolojia ya ufugaji bora zinazotolewa na watafiti hapa nchini na kuwafundika kutumia mbinu hizo kuboresha ufugaji wao.

"Wizara yetu inaendelea kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta binafsi ili kuwezesha nchi kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya vyakula vya mifugo." amesema Mhe. Mnyeti

Mhe. Mnyeti aliongezea kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongeza Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka bilioni 295.9 kwa mwaka 2023/24 hadi bilioni bilion 460.33 kwa mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 55.5, ambazo fedha hizi zitaenda kuimarisha sekta za Mifugo na Uvuvi na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.