Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe jana tarehe 16 Agosti 2024 amefunga mafunzo ya wavuvi wadogo wadogo yaliyokuwa yanafanyika Zanzibar, Wilaya ya kusini Unguja katika Kijiji cha Kizimkazi.
Akifunga mafunzo hayo
Prof.Shemdoe amesema kuwa Mafunzo hayo ni muhimu kwa Wavuvi hao kwasababu lengo
lake kubwa ni kuwajengea uwezo Wavuvi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufugaji
wa Samaki, Uchakataji wa Dagaa, Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi pamoja na
Utunzaji wa mazingira ya bahari ili wazalishe kwa ufanisi na kujiongezea
kipato.
Aidha, Prof. Shemdoe amesema kuwa
anajua wavuvi wanachangamoto mbalimbali na ameahidi changamoto zote walizonazo
wavuvi hao zitafanyiwa kazi kwa kuwa Serikali ya Awamu sita inayoongozwa na
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni
sikivu na inawapenda Wavuvi.
Pia Prof.Shemdoe amesema kuwa
anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanyia Sekta ya Uvuvi na Wavuvi kwa
Ujumla, kwa sababu kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 tayari zaidi ya Boti 160 za
kisasa za uvuvi zimeshakabidhiwa kwa vikundi mbalimbali vya Wavuvi hapa nchini.
Vilele, Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Prof. Shemdoe amewambia wavuvi hao kuwa mafunzo hayo ni
utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Samia Suluhu Hassan kuwa Wakati wa Tamasha la 9 la kizimkazi kwa Mwaka 2024
basi liambatane na mafunzo kwa wakazi wa Kizimkazi na Shehia zake Katika tasnia
ya Uvuvi, Utalii, Ujasiriamali, Kilimo na kukuza sanaa.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi
Mkuu Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) Dkt. Emmanuel Sweke
ameishukuru Serikali kwa kuandaa mazingira bora na kuona uhitaji wa wavuvi
mpaka kuandaa mafunzo hayo.
"Baada ya Mafunzo haya
kukamilika, Serikali inategemea kuona wavuvi mnafanya uvuvi wenye tija na
endelevu”. Alisema Sweke.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe alikutana na Viongozi Waandamizi wa Wizara
ya Uchumi wa Buluu Zanzibar na kujadiliana nao mambo mbalimbali ya Sekta ya
Uvuvi kwa Ujumla, Viongozi hao ni Mhe.Shaabani Othman, Waziri wa Uchumi wa
Buluu na Uvuvi Zanzibar pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu
na Uvuvi Bw. Zahor Kassim El-Khaousy.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni