Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro Nyerere amewaongoza wananchi wa mkoa huo kwenye hafla ya ufunguzi wa shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika kwa upande wa mkoa huo iliyofanyika kwenye kata ya Kasanga Agosti 17, 2024.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa
shughuli hizo Mhe. Nyerere ambaye alimwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega mbali na kuwashukuru Wavuvi wa mkoa huo kwa uvumilivu wao wakati
wote wa ufungaji wa ziwa hilo amewataka kuvua kwa kufuata sheria na taratibu
ili kutunza rasilimali iliyopatikana.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede mbali na kuwaeleza
wananchi wa mkoa huo umuhimu wa upumzishwaji wa Ziwa hilo, amewataka wavuvi hao
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali wakati wote inapokuwa na kampeni
inayolenga kulinda rasilimali za Uvuvi.
Akitoa Ushuhuda wa mavuno
aliyopata baada ya ufunguzi huo, Mmoja wa wavuvi kutoka kijiji cha Kilewani Bw.
Adam Pesambili amesema kuwa kwa usiku mmoja tu amefanikiwa kuvuna kiasi cha
ndoo 60 za dagaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi Mil 4.5 tofauti na awali
ambapo alikuwa hawezi kupata hata ndoo 2 kwa siku.
"Tunaomba Serikalo iendelee
na mpango huu wa upumzishaji wa Ziwa kwa sababu tumeona manufaa yake"
Ameongeza Bw. Pesambili.
Tukio hilo la Ufunguzi wa
shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika mkoa wa Rukwa liliambatana na ugawaji wa
makasha 70 ya kuhifadhia Samaki ambapo Wilaya ya Kalambo ilipata makasha 40 na
Nkasi ilipata makasha 30.
Ufunguzi huo umefanyika ikiwa ni
baada ya takribani miezi mitatu ya upumzishwaji wa Ziwa hilo ulioanza Mei 15,
2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni