◼️ Mnyeti agusia mpango wa Vizimba Ziwa Nyasa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameshangazwa na ukubwa wa ng'ombe waliopo kwenye ranchi ya Kitulo mkoani Njombe.
Tukio hilo limetokea Agosti 8, 2024 jijini Mbeya kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya kimataifa ya wakulima kwa upande wa kanda ya Nyanda za Juu kusini ambapo Mhe. Kikwete alikuwa mgeni rasmi wa tukio hilo akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
"Pale kwetu sisi ni wafugaji tena wafugaji wa kisasa na nilikuwa ninasema nina ng'ombe mkubwa sana lakini leo nimekutana na ng'ombe mwenye uzito wa kilo 900 pale kwenye banda la Shamba la Mifugo la Kitulo, Hongera sana Mkuu wa Mkoa wa Njombe maana shamba hili lipo mkoani kwako" Amesema Mhe. Kikwete.
Mhe. Kikwete ametumia jukwaa hilo kutoa rai kwa wafugaji wengine kufuga kisasa ili ufugaji wao uwe na tija na kubadili maisha yao kwa ujumla.
"Nimesikia pia huko Dodoma kuna ng'ombe anatoa lita 50 za maziwa kwa siku na kwa kuwa wameongeza siku za maonesho lazima nifike huko pia nikashuhudie ili nami niendelee kujifunza" Ameongeza Mhe. Kikwete.
Katika taarifa yake ya utangulizi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ameweka wazi kuwa Wizara yake imetenga fedha ya kufanya utafiti wa ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba kwa upande wa Ziwa Nyasa ili kuongeza wigo wa uzalishaji wa samaki katika ziwa hilo.
"Ufugaji huu ni ufugaji wa kisasa na dunia ndo imefikia huko na tayari umeanza kufanyika Mwanza na kwa upande wa Ziwa Tanganyika hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kuomba Vizimba vya kufugia samaki vilivyotolewa kwa wingi na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" Amesisitiza Mhe. Mnyeti.
Aidha Mhe. Mnyeti amegusia mikakati mingine ya Serikali inayolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa samaki nchini ikiwa ni pamoja na kupumzisha maziwa huku akitoa mfano wa mafanikio yaliyopatikana baada ya kupumzishwa kwa Ziwa Tanganyika ambalo linatarajiwa kufunguliwa Agosti 15, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni