Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wadau wa uvuvi kuzalisha samaki kwa njia ya kisasa ili kuongeza wingi wa samaki kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu kwani kwa sasa kuna upungufu wa samaki.
Akizungumza, leo Agosti 13, 2024 mkoani Mwanza katika kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji lililoudhuliwa na nchi 18 za Afrika, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mnyeti amesema serikali itaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali ili wajitokeze kwa wingi na kufuga kwa teknolojia.
"tutaendela kuhamasisha wadau mbalimbali wajitokeze kwa wingi kwani vizimba vipo vingi vinavyohitaji wadau na tunawakaribisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali waje wawekeze kwa sababu maeneo ya kufugia samaki yapo na vizimba vipo." amesema Mhe. Mnyeti
Aidha, Mhe. Mnyeti alisema awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuleta mabadiriko na maboresho makubwa, na ndio mana miezi nane iliyopita Mhe. Rais alikuja kukabidhi vizimba na boti za uvuvi hapa ziwa Viktoria.
Mhe. Mnyeti amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), inatoa mikopo isiyo na riba kwa hiyo wadau wa uvuvi waje kukopa kwa wingi ili kuzalisha samaki kwa wingi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla amesema ukuzaji viumbe maji ni moja ya fursa katika Uchumi wa Bluu, na juhudi hizi zimeleta ongezeko la uzalishaji, ambapo katika mwaka 2023 jumla ya tani laki tatu za mazao ya ukuzaji viumbe maji yalizalishwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kati ya hizo takribani tani laki moja na ishirini zilizalishwa hapa nchini Tanzania na hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika hizi nchi kwa kutoa ajira, lishe na kusaidia katika ukuaji wa uchumi katika nchi.
Vilevile Dkt. Madalla amesema juhudi hizi za uzalishaji kwa upande wa Tanzania zimetokana na serikali kuwezesha kuwepo kwa vituo vya ukuzaji viumbe maji kwa lengo la kutoa huduma za ugani na kuhamasisha mbinu bora za ukuzaji viumbe maji.
Mratibu wa Kongamano la Tatu la Afrika Mashariki la Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Etienne Hinrichsen amesema hatuna namna zaidi ya kukuza samaki kwa kutumia njia za vizimba kwa sababu kwa sasa maziwa yetu na mito hayana samaki wa kutosha kulisha idadi kubwa ya watu.
Bw. Hinrichsen aliendelea kusema inabidi kufanya kilimo cha ukuzaji viumbe maji na kuzalisha kwa wingi kwa lengo la kukidhi mahitaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni