Nav bar

Jumanne, 6 Agosti 2024

FETA YATOA ELIMU YA MFUMO WA KUZALISHA SAMAKI NA MAZAO "AQUAPONICS" NANENANE.

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) yatoa elimu ya mfumo wa kuzalisha samaki na Mazao kwa wadau waliotembelea kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea kufanyika Kanda ya Ziwa Magharibi, katika Viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza.

Akitoa elimu hiyo Agosti 04.2024, kwa wadau waliotembelea kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkufunzi wa Wakala hiyo kutoka Kampasi ya Nyegezi (Mwanza), Bw. Mukama Ndaro aliwaelezea mfumo huo unavyoleta faida kwa Wafugaji.

Bw. Ndaro ameelezea kuwa uchafu unaozalishwa na samaki unakuwa mbolea kwa mazao, na Mazao yanayasafisha maji kwa kuchuja mbolea (mkojo) inayotokana na samaki na kufanya maji hayo yawe masafi kwa matumizi ya ufugaji wa samaki tena. 

"Mchakato wa kuchuja mbolea au uchafu unatokana na samaki na chakula hufanywa kwa msaada wa Viorwa aina ya bakteria (Nitrobacter na Nitrosomonas)  Viorwa hao hugeuza Amonia kuwa Nitrite ambazo ni sumu kwa samaki Kisha Nitrite hugeuza kuwa Nitrate ambayo ni mbolea kwa mimea" amesema Bw. Ndaro.

Aidha, ameendelea kubainisha faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na matumizi bora ya eneo, matumizi bora ya maji, uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha usalama wa chakula (mazao na samaki)

Naye mhitimu wa Mafunzo ya Uvuvi  kutoka  Kampasi ya Nyegezi, Bw. Bryton  Okendo amesema kwa upande wake amenufaika na Mafunzo hayo ya mfumo wa "Aquaponics" kwa kupata elimu ya kuweza kujiajiri na kujitegemea kiuchumi, amesema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Maonesho hayo.

Pia, Wakala hiyo inaendelea kutoa elimu ya teknolojia mbalimbali ya ufugaji samaki kama teknolojia ya ufugaji samaki kwenye vizimba, teknolojia totoleshi (hatchery technology) teknolojia ya ufugaji kwenye matanki, Uzalishaji na Ukuzaji wa samaki wa mapambo, utengenezaji wa boti za "fiberglass" teknolojia ya usindikaji na kuongeza thamani mazao ya samaki.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni