Na. Edward Kondela
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhi Shilingi Bilioni 1.1 kwa vikundi 25 vya programu ya “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT) ili viweze kufuga kwa tija.
Kabla ya kukabidhi mfano wa hundi hiyo kwa baadhi ya wanufaika wa programu ya BBT, kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma (08.08.2024), Rais Samia ameonesha kufurahishwa namna vijana wanavyoendelea kunufaika kupitia sekta za mifugo na uvuvi, baada ya kutembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Rais Samia amewataka vijana kutumia vyema fursa zinazojitokeza ili waweze kujiinua kiuchumi na kutoa elimu kwa wenzao ambao bado hawajachangamkia fursa hizo hususan katika sekta za mifugo na uvuvi.
Wakati Rais Samia akikabidhi mfano wa hundi hiyo ya Shilingi Bilioni 1.1 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema fedha hiyo ni mkopo wenye masharti nafuu na kwamba serikali itaendelea kutoa mikopo kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.
Akihutubia wananchi walioshiriki kilele cha Maonesho ya Nane Nane ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma, Rais Samia amesema serikali imejipanga kujenga uchumi jumuishi unaowainua wananchi wote na kuwawezesha kunuifaika ipasavyo kupitia uwekezaji unaofanywa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Amefafanua kuwa serikali imeongeza bajeti kwa ajili ya kilimo, mifugo na uvuvi ili uwekezaji huo ulete mageuzi makubwa kwa kuongeza maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbolea, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, kuimarisha huduma za ugani kuboresha miundombinu ya kuhudumia mifugo pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani, chanjo, majosho na masoko.
Aidha, amesema serikali imeendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya mifugo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi, ukuzaji wa viumbe maji na utafutaji wa masoko na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wavuvi na wafugaji.
Kwa upande wake Waziri wa Miugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo, amesema kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 wizara imetengewa bajeti ya Shilingi Bilioni 465 ambayo ni maradufu ya bajeti iliyokuwa ikipata awali, ambazo zitawezesha kutatua changamoto za wafugaji na wavuvi.
Amesema kwa mwaka huu wa fedha, serikali imeandaa kampeni kubwa ya kitaifa ya chanjo kwa ajili ya mifugo pamoja na kuitambua mifugo hiyo, ili kuhakikisha mifugo inakuwa na afya bora na kuleta tija kwa mfugaji.
Pia amesema imepanga kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya boti za uvuvi zisizopungua 450 na vizimba 900 kwa ajili ya kufugia samaki ili kukuza sekta hiyo kwa kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni