Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema teknolojia ya uzalishaji wa malisho aina ya Juncao ambayo imeanza kutumika hapa nchini ni suluhisho la kumaliza changamoto za malisho ya mifugo na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.
Waziri Ulega amesema hayo wakati alipouongoza ugeni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) wakiwakilishwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Earle Courtenay Rattray kutembelea Shamba la Serikali la Mbegu za malisho aina ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani leo Agosti 9, 2024.
“Katika shamba hili la serikali la Vikuge kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka huu wa 2024 tumeshapanda majani ya juncao ekari 21, mbegu zilizozalishwa ni Kilo 178,262, huku zaidi ya wakulima 957 wakishiriki kulima majani hayo kwa hatua tofautitofauti”, amesema Ulega
Aidha, Waziri Ulega ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa mchango wao mkubwa katika kuwajengea uwezo wataalam mbalimbali wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuifahamu teknolojia hiyo ya ulimaji majani ya Juncao huku akisema kuwa teknolojia hiyo ni chachu katika kumaliza changamoto za malisho ya mifugo na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.
“Teknolojia hii tumeichukua kama ni suluhu ya mahitaji ya malisho katika taifa letu”, ameongeza
Kwa upande wake, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa (UN), Balozi Earle Courtenay Rattray amefurahishwa na maendeleo ya teknolojia hiyo hapa nchini huku akimpongeza Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utayari wa kuipokea teknolojia hiyo ambayo inakwenda kuwa moja ya suluhisho ya changamoto ya malisho na migogoro ya wakulima na wafugaji hapa.
Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimueleza jambo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Earle Courtenay Rattray wakati walipotembelea Shamba la Serikali la Mbegu za malisho aina ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani leo Agosti 9, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni