Nav bar

Jumanne, 6 Agosti 2024

RC DENDEGO AWAKUMBUSHA WAFUGAJI KUFUGA KWA TIJA NA KIBIASHARA


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amewakumbusha wafugaji wote hapa nchini Tanzania kufuga kwa tija na kibiashara kwani ufugaji ni utajiri.

Akizungumza, leo Agosti 5, 2024 mkoani Dodoma alipotembelea eneo la arena ya mifugo katika maonesho ya nanenane ya Kimataifa yanayofanyika Kitaifa Mkoani Dodoma kushuhudia mifugo mbalimbali ikishindanishwa kwa ubora, Mhe. Dendego amesema wafugaji wanatakiwa kufuga kibiashara ili kuleta tija na kuongeza ajira ili kuondokana na umasikini na kuchangia uchumi wa nchi na wa mfugaji mmoja mmoja.

"serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya juhudi katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/25 yenye malengo ya kuendeleza Sekta ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo" amesema Mhe. Dendego

Aidha, Mhe. Dendego alisema shughuli hizi ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo ili kukuza kipato na ajira kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mhe. Dendego alisema kwa mwaka 2022 ukuaji wa sekta ya mifugo umefikia asilimia 5, ukichangia kwa asilimia 7.0 kwenye pato la taifa.

Vilevile Mhe. Dendego amesema ili kuhakikisha tija inapatikana katika sekta ya mifugo, Wizara imeweka vipaumbele vya kuimarisha upatikanaji wa maji, malisho na vyakula vya mifugo, kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, kuimarisha afya za mifugo, kuboresha huduma za ugani, kuimarisha huduma za utafiti na mafunzo ya taaluma za mifugo, kuimarisha masoko, kuwezesha thamani ya mazao ya mifugo na kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema lengo la maonesho na mashindano haya ya mifugo ni kuwahakikishia wafugaji kuwa matumizi ya teknolojia ya ufugaji yanawezekana katika mazingira ya kufuga kwenye maeneo wanayoishi na kushawishi matumizi ya teknolojia ya ufugaji bora.

Mh. Mnyeti alisema wizara inamkakati wa kufundisha teknolojia ya ufugaji kwa wafugaji, na pia wizara imejipanga kufanya zoezi la chanjo za mifugo, kujenga miundombinu muhimu ya mifugo ikiwemo majosho na miundombinu ya maji, uboreshaji wa mbali za mifugo, kuimarisha mashamba ya wizara, kuimarisha mbegu za malisho, uanzishaji wa mashamba darasa ya malisho katika halmashauri mbalimbali nchini, kuimarisha huduma za utafiti na ugani, kuhamasisha sekta binafsi na kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya mifugo, pamoja na kuendeleza programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).

Akiongea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema leo ameshukuru kwa kuona paredi ya gwaride ya mifugo ambalo ni jambo la kipekee na inathibitisha kabisa utajiri katika sekta ya mifugo.

Mhe. Senyamule amesema mifugo ni kati ya sekta kubwa zinazotegemewa na wananchi wengi katika swala la uchumi, chakula, kipato, nguvu kazi, mbolea na kama fahari.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni