Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na mikoa ya Dodoma na Singida imefanya maajabu ya kipekee katika maonesho ya nanenane ya mwaka 2024 ikiwa tofauti na miaka mingine ya maonesho hayo kwa kuboresha zaidi miundombinu na teknolojia mpya na za kisasa.
Akizungumza, leo Agosti 1, 2024 mkoani Dodoma katika Ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa Kanda ya Kati - Dodoma, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Kilimo ikishirikiana na menejimenti ya mkoa wa Dodoma na Singida, zimefanya vizuri katika maandalizi ya nanenane kwa mwaka 2024 na ameridhishwa na maandalizi ya maonesho hayo.
"mwaka huu Wizara zetu na mikoa ya Dodoma na Singida, zimefanya maajabu makubwa hapa viwanja vya nanenane Nzuguni, hii ni hatua kubwa sana inayohitaji pongezi toka kwenu kwa sababu hii imevunja rekodi ya maonesho yote ya miaka mingine." amesema Mhe. Majaliwa
Aidha, Mhe. Majaliwa alisema lengo la maonesho haya ya nanenane ni kutoa fursa kwa wafugaji, wavuvi, wanaushirika, wajasiriamali na wasindikaji, kwenda kujifunza teknolojia mbalimbali kutoka kwa wadau wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi ambapo pia ni Sekta binafsi na wao pia wapo pamoja na wataalamu waliopo serikalini wanaonyesha umuhimu wa sekta ya Mifugo na Uvuvi, Ushirika na ujasiriamali unavyoleta tija kwenye maisha ya kila mtu, lakini pia katika maonesho haya yanatoa nafasi kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa kuzidi kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kuuza bidhaa ambazo zinakuja kuuzwa katika eneo hili.
Mhe. Majaliwa alisema maonesho haya ni ya 31 toka kuanzishwa kwake, na yamekuwa yanaboreshwa kila mwaka na hii ni fursa kwa wadau wote wa Mifugo na Uvuvi na kusisitiza kuwa Nitoe rai kwa watanzania wajitokeza kwa wingi katika maonesho haya ili waende wakaone maonesho ya bidhaa mbalimbali na teknolojia mbalimbali zinazooneshwa katika viwanja hivyo.
Vilevile Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imekuwa inachukua hatua mbalimbali katika kutekeleza mipango na mikakati mahususi ya kihakikisha Sekta muhimu za Mifugo, Uvuvi na Kilimo zinaendelea kuwa muhimili muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuleta maendeleo kwa wananchi kwani zimekuwa zikishangia kwa ukubwa pato la taifa kwani kwa mwaka 2023/24 Sekta hizi zilichangia asilimia 26.5 ya pato la taifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, amesema Wizara imeandaa mashindano ya Mifugo ambayo ina lengo la kuwahakikishia wafugaji kuwa matumizi ya teknoloji yanawezekana katika mazingira ya kufuga katika maeneo wanayoishi na kushawishi matumizi ya teknolojia ya ufugaji bora.
Vilevile Mhe. Mnyeti amesema, maonesho haya uwezesha wafugaji kujenga imani na wataalamu na ugani kwa kuhakikisha kuwa ushauri wao ni wa thamani na wenye tija, pia kusaidia kujenga imani kwa wafugaji kuhusiana na matumizi sahihi ya teknolojia ya ufugaji bora zinazotolewa na watafiti hapa nchini na kuwafundika kutumia mbinu hizo kuboresha ufugaji wao.
"Wizara yetu inaendelea kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta binafsi ili kuwezesha nchi kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya vyakula vya mifugo." amesema Mhe. Mnyeti
Mhe. Mnyeti aliongezea kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongeza Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka bilioni 295.9 kwa mwaka 2023/24 hadi bilioni bilion 460.33 kwa mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 55.5, ambazo fedha hizi zitaenda kuimarisha sekta za Mifugo na Uvuvi na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni