Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega ametangaza mpango wa Serikali wa
kupumzisha shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu
ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli
zao ziwani humo.
Waziri Ulega ametoa
kauli ya serikali kwa nyakati tofauti ambapo awali alitoa kauli hiyo
akizungumza na wadau wa uvuvi kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na baadaye
kuzungumza na wananchi na wadau wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Mwalo wa
Katonga Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2024.
Akiwa kwenye kikao cha
ndani na wadau wa uvuvi Waziri Ulega alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo
utaanza rasmi Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu na hiyo ikiwa ni Utekelezaji wa
Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua
na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
Akieleza sababu ya maamuzi
hayo alisema ni kutokana na utafiti kubainisha kuwa kumekuwepo na upungufu
mkubwa wa samaki na dagaa katika ziwa Tanganyika kunakotokana na ongezeko kubwa
la uvuvi usio endelevu uliopelekea uharibifu wa mazalia ya samaki.
"Pamoja na kufunga
shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika, Serikali ya Mhe. Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan imeanza kutekeleza njia mbadala za kuwawezesha wananchi
kujiendeleza kiuchumi katika ziwa Tanganyika ikiwemo kukopesha vikundi maboti
na vizimba kwa ajili ya miradi ya ufugaji wa samaki na tayari imetenga shilingi
milioni 200 kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kubainisha maeneo
yanayofaa kwa ufugaji huo,' alisema Waziri Ulega
Aliongeza kuwa Mhe. Rais,
Dkt. Samia ametoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha
uzalishaji wa vifaranga vya samaki bora mkoani humo kwa ajili ya kuwawezesha
wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kuwa na uhakika wa kupata vifaranga bora
wakati wote.
Halikadhalika alifafanua
kuwa hatua hiyo ya kupumzisha ziwa sio jambo geni kwa sababu linafanyika katika
Mikoa ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ambapo wanafunga miamba kwa ajili
ya uvuvi wa pweza na matokeo yameonesha kuwa wakati wa kufungua tani takriban
100 zimekuwa zikipatikana.
Aidha, alitumia nafasi hiyo
pia kuwahimiza wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo ya
vizimba na maboti ili waweze kujikwamua kiuchumi katika nyakati hizo za
upumzishaji wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti alisema kuwa mpango huo una
manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla na ni muhimu kuharakisha
utekelezaji wake ili kunusuru ziwa hilo ambalo uzalishaji wake umeshuka sana.
Mnyeti alisema kuwa zipo
nchi duniani zimetekeleza mpango huo na faida kubwa imeonekana kwa kuongeza
mazao ya uvuvi, kuongeza mapato kwa wavuvi na serikali kwa kiwango kikubwa.
Awali Mwakilishi wa
Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ambakisye Simtoe akiwasilisha
hali ya uvuvi na wingi wa samaki ziwa Tanganyika alisema kuwa umepungua na kwa
sasa hali sio nzuri.
Ambakisye alisema kuwa
mwaka 1995 takwimu zilikuwa zikionyesha kuwepo kwa wingi wa samaki tani 197,493
zinazoweza kuvuliwa kwa mwaka ambapo kiwango hicho kimeshuka na kufikia tani
144,690. Pia, uvuvi umeshuka kutoka tani 104,178 mwaka 2020 na kufikia tani
85,180.
Naye Mkurugenzi wa
Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Paul Deogratius alisema kuwa
mkataba mdogo wa nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika ibara ya saba wa mwaka 2021
unaitaka Tanzania kutekeleza ulinzi na utunzaji wa rasilimali za ziwa
Tanganyika ikiwemo shughuli za uvuvi.
Deogratius alisema kuwa
nchi za Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia zilitekeleza mkataba
huo mwaka jana isipokuwa Tanzania jambo ambalo halileti picha nzuri kwenye
uhusiano na ushirikiano wa kimataifa.
Wabunge wa Mkoa wa Kigoma,
Mhe. Kilumbe Ng'enda wa Kigoma Mjini na Mhe. Josephine Genzabuke wakizungumza
kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Ulega uliofanyika katika mwalo wa Katonga
wameunga mkono mpango huo wa serikali na kusema utaleta faida kubwa kwa sekta
ya uvuvi.
Miongoni mwa Nchi Wanachama
wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika sambamba na Tanzania ni pamoja na Zambia, Burundi
na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo ambao wao walishaanza kutekeleza zoezi hilo
la upumzishaji wa ziwa Mwaka jana (2023).
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na wananchi (hawapo pichani)
wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Ziwa Tanganyika alipokutana nao katika
Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega akisalimiana na baadhi ya kina mama wanaojishughulisha na
uvuvi wakati wa mkutano uliofanyika kwenye Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma
Januari 9, 2024.
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na
Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi muda mfupi baada ya kumaliza kikao na
wadau wa uvuvi (hawapo pichani) kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Januari
9, 2024. Kushoto kwake ni Naibu Waziri was Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander
Mnyeti. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Sekta ya Uvuvi, Bi. Agnes Meena.