Na. Edward Kondela
Maafisa mifugo nchini
wametakiwa kufanya kazi za udaktari wa mifugo walizosomea na kuwatembelea
wafugaji badala ya kuwa wakusanya mapato wa halmashauri.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amebainisha hayo (15.01.2024) mjini Dodoma wakati
akizindua Baraza la Veterinari Tanzania awamu ya sita baada ya baraza hilo
kupata wajumbe.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa baraza hilo Mhe. Mnyeti amesema baadhi ya maafisa mifugo wamekuwa
wakijikita zaidi kwenye kukusanya mapato ya halmashauri minadani badala ya
kuwatembelea wafugaji ili kujua matatizo yao.
“Maafisa mifugo kwenye
halmashauri wanajifanya watumishi wa halmashauri kwa ajili ya kukusanya mapato
kwenye minada kukusanya ushuru wa ng’ombe badala ya kufanya kazi za udaktari na
kuwatembelea wafugaji.” Amesema Mhe. Mnyeti
Aidha, amelitaka Baraza la
Veterinari Tanzania kuhakikisha linachukua hatua zaidi kwa maafisa mifugo ambao
wamekuwa wakifanya kazi kinyume na maadili pamoja na kuwapatia semina mara kwa
mara ili kuwakumbusha wajibu wao kwa wananchi.
Amesema pia ifike wakati
maafisa mifugo ambao wanakiuka maadili wafukuzwe kazi pamoja na kufutiwa leseni
zao ili kazi hiyo ifanywe na watu ambao watafuata taratibu na maadili ya kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Mifuo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema ana imani maafisa mifugo
ambao walikuwa wakituma maombi kwa ajili ya kusajiliwa kwenye Baraza la
Veterinari Tanzania sasa wataanza kusajiliwa rasmi kwa kuwa baraza hilo tayari
limezinduliwa.
Amefafanua kuwa amekuwa
akipata ujumbe kwa njia ya simu kutoka kwa baadhi ya maafisa mifugo ambao
wamekuwa wakihitaji kusajiliwa lakini hawakuweza kusajiliwa kwa kuwa baraza
halikuwa na wajumbe.
Naye Mwenyekiti wa Baraza
la Veterinari Tanzania Prof. Lughano Kusiluka amesema baraza limekuwa
likisimamia sheria za veterinari kwa kuhakikisha wataalamu wanaohusika na kutoa
huduma za afya za wanyama wafugwao na wasiofugwa wanafanya kazi kwa kufuata
sheria na maadili.
Ameongeza kuwa kazi kubwa
ya baraza ni kuwaandikisha na kuwaingiza kwenye daftari la baraza hilo na
kufuatilia kiwango na huduma wanazotoa, kusimamia elimu ya wanyama inayotolewa
na taasisi mbalimbali na kufuatilia kwa ukaribu wadau wapate huduma
inayotakiwa.
Baraza la Veterinari
Tanzania awamu ya sita lililozinduliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Alexander Mnyeti litadumu kwa miaka mitatu.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza baada ya kuzindua Baraza la Veterinari
Tanzania awamu ya sita jijini Dodoma ambapo amewataka maafisa mifugo nchini
kufanya kazi za udaktari wa mifugo walizosomea na kuwatembelea wafugaji badala
ya kuwa wakusanya mapato wa halmashauri. (15.01.2024)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifuo
na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amebainisha kuwa ana imani maafisa mifugo ambao
walikuwa wakituma maombi kwa ajili ya kusajiliwa kwenye Baraza la Veterinari
Tanzania sasa wataanza kusajiliwa rasmi kwa kuwa baraza hilo tayari
limezinduliwa. Prof. Shemdoe amesema hayo wakati wa uzinduzi wa baraza hilo
awamu ya sita. (15.01.2024)
Picha ya pamoja ya Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akiwa na Katibu Mkuu wa wizara
hiyo Prof. Riziki Shemdoe, Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania Prof.
Lughano Kusiluka, Msajili wa baraza hilo Dkt. Amani Kilemile pamoja na wajumbe
wa baraza hilo baada ya kuzinduliwa rasmi jijini Dodoma. (15.01.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni