◾
Aipa Kongole Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia zoezi la Uhakiki wa Vikundi vya
Wavuvi, Wakuzaji viumbe maji.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa
Mhe. Christopher Ngubiagai ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuziongezea nguvu
timu za Doria baharini zilizopo wilayani humo ili ziweze kuendelea kupambana na
Uvuvi haramu.
Mhe. Ngubiagai amesema hayo
baada ya kupokea timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyofika
Wilayani hapo kwa ajili ya zoezi la uhakiki wa taarifa za vikundi vya Wavuvi na
wakuzaji viumbe maji Januari 17, 2023.
" Jitihada hizi kubwa
za kuwawezesha Wavuvi zitakuwa na maana kubwa zaidi kama tutahakikisha
rasilimali za bahari zinapatikana kwa wingi na hili litawezekana kama tuweka
mkazo na nguvu kwenye kupambana na uvuvi haramu ukanda huu wa bahari"
Amesema Mhe. Ngubiagai.
Mhe. Ngubiagai amedokeza
kuwa licha ya Wilaya yake kuendelea na doria ya kupambana na changamoto hiyo
ikiwa ni pamoja na kukagua nyenzo zinazotumiwa na wavuvi hao bado nguvu
waliyonayo haitoshi kupambana na eneo kubwa la bahari linaloizunguka Wilaya
hiyo.
"Tunazo jumuiya za
Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) ambazo kwa kweli zinatusaidia sana
kwenye hili ila bahati mbaya hata wenyewe hawana vifaa vya kisasa vya kuweza
kudhibiti hali hiyo kwa hiyo bado nguvu kubwa inahitajika" Amesisitiza
Mhe. Ngubiagai.
Aidha Mhe. Ngubiagai
ameipongeza Wizara kwa utekelezaji wa programu ya "Jenga Kesho iliyo bora
kwa wajasiriamali wanawake na vijana" (BBT-LIFE) ambapo amesema kuwa
tayari wilaya yake imeshatenga maeneo ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya
shughuli za ufugaji wa samaki na kilimo cha zao la Mwani.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe maji baharini Dkt. Hamis Nikuli amesema kuwa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kutekeleza miradi mbalimbali Wilayani Kilwa ikiwa
ni pamoja na Kujenga chanja za kisasa za kukaushia Mwani na Ghala kubwa la
kuhifadhi zao hilo.
"Lakini pia tayari
kuna hatua za kudhibiti uvuvi haramu zimeshaanza kuchukuliwa upande wa
Dar-es-salaam ambapo zinatarajiwa kufika kwenye maeneo yote yanayopitiwa na
bahari" Ameongeza Dkt. Nikuli.
Timu ya Wataalam kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na zoezi la uhakiki wa vikundi vya Wavuvi
na Wakuzaji Viumbe Maji kupitia ujazwaji wa dodoso maalum lenye taarifa zote za
Msingi lengo likiwa ni kuiwezesha Serikali kuelekeza rasilimali kwa mujibu wa
mahitaji ya vikundi hivyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Ukuzaji Viumbe Maji baharini Dkt. Hamis Nikuli (kulia) akimueleza Mkuu wa
Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai (katikati) namna yeye na timu yake
watakavyoendesha zoezi la Uhakiki wa vikundi vya Wavuvi na Wakuzaji viumbe maji
waliopo Wilayani humo Januari 17, 2024. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo
Bw. Yusuph Mwinyi.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Ukuzaji Viumbe Maji baharini Dkt. Hamis Nikuli (kulia mbele) akimueleza Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa Bw. Shija Lyela (katikati) namna
yeye na timu yake watakavyoendesha zoezi la Uhakiki wa vikundi vya Wavuvi na
Wakuzaji viumbe maji waliopo Wilayani humo Januari 17, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni