Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza wananchi wanaoishi Mtwara na maeneo mengine ya
ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kuchangamkia fursa ya ufugaji wa Majongoo Bahari, Kaa, Kambakochi pamoja na
kufanya kilimo cha Mwani kwa sababu mazao hayo yanahitajika sana katika nchi za
Asia hususan China.
Waziri Ulega ametoa rai
hiyo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha
Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruvula kinachojengwa Msimbati, mkoani Mtwara Januari 14,
2024.
“Mahitahi ya Majongoo
Bahari, Kaa, Mwani, Kambakochi na Mwatiko ni makubwa katika nchi za Asia hasa
china, hivyo ni lazima tucheze na fursa tulizonazo ili tuweze kufanikiwa na
ndio maana serikali inatoa elimu kuwawezesha wananchi hususan vijana na
kinamama kufanya shughuli hizo ili wauze nje ya nchi wajipatie kipato”, alisema
Ulega
Halikadhalika, aliwahimiza
wananchi kujipanga vyema ikiwemo kuunda vikundi ili serikali iweze kuwatambua
na kuwapatia mikopo ya vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuwawezesha kufanya
shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, Waziri Ulega
alionesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha ukuzaji viumbe
maji cha Ruvula huku akiamini kuwa kitakamilika kwa wakati ili kianze kufanya
kazi.
Awali, Mhandisi kutoka Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Bw. George Kwandu alimweleza Waziri Ulega kuwa ujenzi wa
kituo hicho umefikia asilimia 90 na kwamba mpaka itakapofika Januari 30, 2024
mradi huo utakuwa tayari umekamilika.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega (katikati)akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Ukuzaji
Viumbe Maji kinachojengwa Msimbati, Ruvula, mkoani Mtwara alipofanya ziara ya
kukagua kituo hicho Januari 14, 2024. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe.
Ahmed Abbas. Kulia ni Mhandisi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. George
Kwandu.
Pichani ni muonekano wa
jengo la kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji linalojengwa Msimbati, Ruvula, mkoani
Mtwara alipofanya ziara ya kukagua kituo hicho Januari 14, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni