Nav bar

Jumanne, 23 Januari 2024

PWANI IPO TAYARI KUTEKELEZA BBT-LIFE-MCHATTA

Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Bw. Rashid Mchatta amekutana na ujumbe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi upande wa sekta ya Mifugo Januari 15, 2024 na kufanya nao mazungumzo  kuhusu  namna ya kutekeleza mradi wa "Jenga kesho iliyo bora kwa wajasiriamali wanawake na Vijana (BBT-LIFE) kwa Mkoani humo.

Akiongoza kikao hicho Bw. Mchatta ameipongeza na kuishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka programu hiyo mkoani kwake ambapo ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wake.

"Tunatambua tija kubwa watakayoipata vijana hawa na wanawake watakaofanikiwa kuchaguliwa kuingia kwenye programu hii hivyo niwashukuru sana kwa kuuleta mpango huu hapa Pwani" Amesema Bw. Mchatta.

Akizungumza wakati wa kikao hicho  Mkurugenzi msaidizi  wa utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt Hassan Mrutu  amesema kuwa  utekelezaji huo umewalenga vijana na wanawake katika  suala zima la Ufugaji wa kibiashara ambapo jumla ya vijana 30 watakaochaguliwa wanatarajiwa kunufaika na mpango huo utakaotekelezwa kwa siku 90.

Mazungumzo hayo baina ya pande hizo yamefanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambapo mbali na watalaam hao kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pia yalihudhuriwa na wataalam kutoka Sekretariet ya Mkoa. 


Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo (Mifugo) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Hassan Mrutu (mbele kushoto) akimuelezea Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bw. Rashid Mchatta (kulia) namna wizara inavyotarajia kutekeleza mradi wa "Jenga kesho iliyo bora" (BBT-LIFE) kwa upande wa sekta ya Mifugo mkoani humo muda mfupi baada ya kufika ofisini kwake Januari 15, 2024.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bw. Rashid Mchatta (katikati mbele) akiongoza kikao baina ya timu ya wataalam wa mkoa huo na wale wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinachohusu utekelezaji wa programu ya "Jenga kesho iliyo bora" BBT-LIFE kwa upande wa sekta ya Mifugo mkoani humo Januari 15, 2024.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni