Mkurugenzi Msaidizi wa
Ukuzaji Viumbe Maji upande wa mazao ya bahari Dkt. Hamis Nikuli amewataka
wafugaji jongoo bahari mkoani Mtwara kufuata sheria na taratibu za ufugaji wa
zao hilo.
Dkt. Nikuli ameyasema hayo
wakati wa zoezi la ujazaji wa dodoso linalohusu taarifa za wavuvi na wakuzaji
viumbe maji lililofanyika Januari 12,
2024 kwenye kampasi ya Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi (FETA) iliyopo eneo la
Mikindani mkoani humo.
"Tunahamasisha sana
ufugaji wa jongoo bahari kwa sababu wale waliopo kwenye maji ya asili kwa huku
Tanzania bara hawaruhusiwi kuvuliwa kwa sasa lakini ni lazima kila mtu au
kikundi kifuate taratibu zilizopo kwenye kibali chake na isitokee mmoja wenu
akatumia kibali cha mwenzie kuvuna jongoo hao" Amesema Dkt. Nikuli.
Dkt. Nikuli ameongeza kuwa
ni lazima wafugaji jongoo bahari wote waliopo mkoani humo kuhakikisha wanatoa
taarifa sahihi za idadi ya jongoo bahari wanaowafuga na kuwa waaminifu pindi
wanapopewa kibali cha kuvuna ili wavune idadi waliyoidhinishiwa kwenye vibali
hivyo.
Akizungumzia kuhusu
madodoso ya taarifa za wavuvi na wakuzaji viumbe maji waliopo mkoani humo, Dkt.
Nikuli amesema kuwa hatua hiyo imetokana na kutopatikana kwa haraka na usahihi
wa taarifa za mvuvi mmoja mmoja, kikundi au kampuni inayojihusisha na uvuvi au
ukuzaji viumbe maji pindi zinapohitajika kwa ajili ya madhumuni mbalimbali
ikiwemo mikopo inayotolewa na Taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo.
" Hadi sasa Mkoa wa
Mtwara una vikundi 97 vinavyofuga na vinavyotarajia kufuga jongoo bahari na kwa
ujumla dodoso hili limegusia taarifa za watu binafsi, kikundi na kampuni
zinazojishughulisha na Uvuvi au Ukuzaji viumbe maji na kwa kuwa nyie
mnajishughulisha na ufugaji jongoo bahari, taarifa mnazojaza zitaturahisishia
kuelekeza rasilimali tunazopata kutoka kwa wadau wetu wa sekta kwa mujibu wa
mahitaji mliyonayo" Amesisitiza Dkt. Nikuli.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Vikundi vya wafugaji wa jongoo bahari eneo la Mtwara Mikindani Bw. Ramadhan
Banda amefurahishwa na hatua hiyo ya Wizara kukusanya taarifa zao huku akiweka
wazi kuwa wamepata somo kubwa la namna bora ya kudhibiti soko la jongoo bahari
ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wauzaji wa zao hilo kiholela.
"Nimefurahi pia
kusikia hakuna mtu anayeruhusiwa kuvuna jongoo bahari bila kibali kutoka kwenu
(wizarani) kwa sababu hatua hiyo itamaliza changamoto ya wizi wa zao hilo
ambapo wengi wamekuwa wakiibuka sokoni na jongoo waliyowaiba kwenye vizimba vya
wenzao" Ameongeza Bw. Banda.
Timu ya Wataalam kutoka
Wizara ya mifugo na Uvuvi inaendesha zoezi la ujazaji madodoso ya Taarifa za
Wavuvi na wakuzaji viumbe maji Mkoani kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi kwa lengo
la kuwa na taarifa sahihi za makundi hayo pindi wanapohitaji kuwawezesha nyenzo mbalimbali za uendeshaji
wa shughuli zao.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Ukuzaji Viumbe Maji (Bahari) Dkt. Hamis Nikuli akizungumza na vikundi vya
Ufugaji jongoo bahari wa eneo la Mtwara Mikindani (hawapo pichani) wakati wa zoezi la Ujazaji wa dodoso
linalohusu taarifa za Wavuvi na wakuzaji viumbe maji waliopo mkoani Mtwara
lililofanyika Januari 12, 2024, Kulia kwake ni Mwenyekiti wa vikundi hivyo Bw.
Ramadhan Banda na kushoto kwake ni Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi Bi. Janeth Rukanda.
Afisa Uvuvi Mwandamizi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi
Kresensia Mtweve (kulia) akiweka taarifa za mmoja wa wafugaji jongoo
bahari kwenye dodoso wakati wa zoezi la
ujazaji wa taarifa hilo lililofanyika Januari 12, 2024, Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi
ya Mikindani mkoani Mtwara.
Afisa Uvuvi Mkuu kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi Janeth Rukanda (kushoto) akifafanua jambo wakati
wa zoezi la ujazaji wa dodoso la wavuvi na wakuzaji viumbe maji lililofanyika
Januari 12, 2024, Chuo cha Mafunzo ya
Uvuvi (FETA) kampasi ya Mikindani mkoani
Mtwara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni