Na. Edward Kondela
Serikali yaazimia
kupumzisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa kipindi cha miezi
mitatu kwa miaka mitatu mfululizo ili kuongeza mazalia ya samaki na kuhamasisha
ufugaji samaki kwa njia ya vizimba katika ziwa hilo.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amebainisha hayo (10.01.2024) kwa nyakati tofauti
wakati alipokuwa akiongea na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi na
wadau wa uvuvi katika mkoa huo wakiwemo wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi
katika Mwalo wa Ikola uliopo katika Wilaya ya Tanganyika.
Naibu Waziri Mnyeti amesema
serikali imeazimia kupumzisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kuanzia
tarehe 15 Mei hadi tarehe 15 Agosti Mwaka 2024 ikiwa ni utekelezaji wa Mkataba
wa Kikanda wa Usimamizi wa Uvuvi endelevu katika ziwa hilo na bonde lake ambapo
nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kwa maana ya Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Tanzania na
Zambia zilitia saini mkataba huo Tarehe 9 Mwezi Desemba Mwaka 2021 kwenye
mkutano wa 9 wa mawaziri wa nchi hizo.
Mhe. Mnyeti amebainisha
kuwa lengo la mkataba huo kwa nchi hizo ni kutoa muda kwa samaki kuzaliana
ambapo kutokana na tafiti zilizofanywa na Tasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania
(TAFIRI) katika kipindi cha Mwezi Mei na Agosti samaki huwa wanazaliana kwa
wingi.
“Tunapumzisha ziwa hili kwa
sababu samaki wanaenda kuisha ziwani ili tupishe wazaliane baada ya muda wa
miezi mitatu tutaendelea na shughuli za uvuvi na jambo hili litakuwa la kila
mwaka ili kuruhusu mazalia ya samaki ni mkataba wa nchi zinazozunguka Ziwa
Tanganyika.” Amesema Mhe. Mnyeti
Aidha, ametaka wananchi
wanaofanya shughuli za uvuvi katika ziwa hilo kupatiwa elimu ya kutosha na pia
serikali itaweka nguvu kwa wananchi hao kujikita katika ufugaji wa samaki kwa
njia ya vizimba kwenye ziwa hilo huku wakiacha samaki wa asili waliopo ziwani
kuzaliana.
Ameongeza kuwa serikali
itafanya tathmini ya kupumzisha shughuli za uvuvi katika maziwa mengine kila
baada ya muda kwa kipindi ambacho itaona inafaa ili samaki waweze kuzaliana kwa
wingi ambapo kwa sasa inaanza na Ziwa Tanganyika.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amesema uongozi wa mkoa huo uko tayari
kusimamia utekelezaji huo ambao tayari umeanza kutekelezwa kwa mara ya kwanza
Mwaka 2023 na nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika ambapo Tanzania
itatekeleza kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Mhe. Mrindoko amewataka
wakazi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa kuwa ni kwa manufaa yao na kwamba
matarajio ni baada ya kufungwa Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu kutakuwa na
ongezeko la samaki na katika kipindi cha miaka mitatu serikali itaweza kupata
tathmini ya ongezeko la samaki.
Nao baadhi ya wananchi
katika Mwalo wa Ikola Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi wamepokea taarifa hiyo
na kuahidi kushirikiana na serikali wakati wote wa miezi mitatu ambapo shughuli
za uvuvi zitakapokuwa hazifanywi katika Ziwa Tanganyika ili kupisha samaki
kuzaliana kwa wingi.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kiwango cha samaki katika Ziwa Tanganyika kimekuwa
kikipungua kila mwaka huku baadhi ya wavuvi wakitoa ushuhuda wa kupotea kabisa
baadhi ya samaki katika ziwa hilo.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza na wananchi wanaojishughulisha na uvuvi
katika Mwalo wa Ikola uliopo Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi juu ya maamuzi
ya serikali kulipumzisha Ziwa Tanganyika kwa shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu
kuanzia tarehe 15 Mwezi Mei hadi tarehe 15 Mwezi Agosti Mwaka 2024.
(10.01.2024)
Afisa Uvuvi Mkuu kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Ambakisye Simtoe akifafanua hoja mbalimbali kwa
wananchi wa Mwalo wa Ikola uliopo Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, baada ya
wananchi hao kupatiwa taarifa juu ya upumzishwaji wa Ziwa Tanganyika kwa
shughuli za uvuvi ili kuacha samaki wazaliane. (10.01.2024)
Mkurugenzi Msaidizi wa
Undelezaji Rasilimali za Uvuvi Bi. Merisia Mparazo akizungumza na wananchi
wakati akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwenye
mkutano wa hadhara katika Mwalo wa Ikola juu ya upumzishaji wa shughuli za
uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu. (10.01.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni