Nav bar

Jumanne, 23 Januari 2024

ZIWA TANGANYIKA KUPUMZISHWA ILI KUWEZESHA SAMAKI KUZALIANA


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ametangaza mpango wa Serikali wa kupumzisha  shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.

Waziri Ulega  ametoa kauli ya serikali kwa nyakati tofauti ambapo awali alitoa kauli hiyo akizungumza na wadau wa uvuvi kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na baadaye kuzungumza na wananchi na wadau wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2024.

Akiwa kwenye kikao cha ndani na wadau wa uvuvi Waziri Ulega alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza rasmi Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu na hiyo ikiwa ni Utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Akieleza sababu ya maamuzi hayo alisema ni kutokana na utafiti kubainisha kuwa kumekuwepo na upungufu mkubwa wa samaki na dagaa katika ziwa Tanganyika kunakotokana na ongezeko kubwa la uvuvi usio endelevu uliopelekea uharibifu wa mazalia ya samaki.

"Pamoja na kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika, Serikali ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza kutekeleza njia mbadala za kuwawezesha wananchi kujiendeleza kiuchumi katika ziwa Tanganyika ikiwemo kukopesha vikundi maboti na vizimba kwa ajili ya miradi ya ufugaji wa samaki na tayari imetenga shilingi milioni 200 kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kubainisha maeneo yanayofaa kwa ufugaji huo,' alisema Waziri Ulega

Aliongeza kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia ametoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki bora mkoani humo kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kuwa na uhakika wa kupata vifaranga bora wakati wote.

Halikadhalika alifafanua kuwa hatua hiyo ya kupumzisha ziwa sio jambo geni kwa sababu linafanyika katika Mikoa ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ambapo wanafunga miamba kwa ajili ya uvuvi wa pweza na matokeo yameonesha kuwa wakati wa kufungua tani takriban 100 zimekuwa zikipatikana.

Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo ya vizimba na maboti ili waweze kujikwamua kiuchumi katika nyakati hizo za upumzishaji wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti alisema kuwa mpango huo una manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla na ni muhimu kuharakisha utekelezaji wake ili kunusuru ziwa hilo ambalo uzalishaji wake umeshuka sana.

Mnyeti alisema kuwa zipo nchi duniani zimetekeleza mpango huo na faida kubwa imeonekana kwa kuongeza mazao ya uvuvi, kuongeza mapato kwa wavuvi na serikali kwa kiwango kikubwa.

Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ambakisye Simtoe akiwasilisha hali ya uvuvi na wingi wa samaki ziwa Tanganyika alisema kuwa umepungua na kwa sasa hali sio nzuri.

Ambakisye alisema kuwa mwaka 1995 takwimu zilikuwa zikionyesha kuwepo kwa wingi wa samaki tani 197,493 zinazoweza kuvuliwa kwa mwaka ambapo kiwango hicho kimeshuka na kufikia tani 144,690. Pia, uvuvi umeshuka kutoka tani 104,178 mwaka 2020 na kufikia tani 85,180.

Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Paul Deogratius alisema kuwa mkataba mdogo wa nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika ibara ya saba wa mwaka 2021 unaitaka Tanzania kutekeleza ulinzi na utunzaji wa rasilimali za ziwa Tanganyika ikiwemo shughuli za uvuvi.

Deogratius alisema kuwa nchi za Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia zilitekeleza mkataba huo mwaka jana isipokuwa Tanzania jambo ambalo halileti picha nzuri kwenye uhusiano na ushirikiano wa kimataifa.

Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Kilumbe Ng'enda wa Kigoma Mjini na Mhe. Josephine Genzabuke wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Ulega uliofanyika katika mwalo wa Katonga wameunga mkono mpango huo wa serikali na kusema utaleta faida kubwa kwa sekta ya uvuvi.

Miongoni mwa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika sambamba na Tanzania ni pamoja na Zambia, Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo ambao wao walishaanza kutekeleza zoezi hilo la upumzishaji wa ziwa Mwaka jana (2023).


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Ziwa Tanganyika alipokutana nao katika Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akisalimiana na baadhi ya kina mama wanaojishughulisha na uvuvi wakati wa mkutano uliofanyika kwenye Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi muda mfupi baada ya kumaliza kikao na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Januari 9, 2024. Kushoto kwake ni Naibu Waziri was Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Sekta ya Uvuvi, Bi. Agnes Meena.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni