Leo Januari 18, 2024,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Wawekezaji kutoka
Kampuni ya Uwekezaji ya Contractus ya nchini Poland ambao wameonesha nia ya
kufanya uwekezaji kwenye tasnia ya Maziwa hapa nchini.
Wawekezaji hao ambao ni
Makamu Mwenyekiti wa Kampuni Contractus, Bw. Witold Karczewski na Makamu
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya Poland ambaye pia ni Meneja Mauzo wa
Kampuni, Bw. Adam Borawski wameonesha nia ya kuingia ubia na Serikali ya
Tanzania Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuleta telnolojia ya kisasa ya
kupoza maziwa katika vituo mbalimbali vya kukusanyia maziwa nchini.
Nia yao kuanzia mwaka 2024/
2025 kuanza uwekezaji huo ambapo wataanza na vituo 500 nchi nzima vyenye uwezo
wa kukusanya kati ya lita 2000 hadi 6000 kwa siku. Uwekezaji huo
unatarajiwa kuongeza ukusanyaji wa lita
takribani milioni moja za maziwa kwa siku hapa nchini.
Aidha, mpango huo
unaotarajiwa kuwa wa miaka 2 unakadiriwa kugharimu TZS. Bilioni 175, na
inakusudiwa kupata ufadhili kutoka kwa Wadau na Serikali ya Poland.
Kwa upande wake, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia wawekezaji hao ushirikiano
wa kutosha ili mradi huo uweze kuanza haraka ili tasnia ya maziwa iweze kuwa na
tija zaidi kwa taifa.
Kampuni hiyo ya Contractus
inatengeneza na kuuza Machine/Vifaa vya Kukusanyia maziwa ambazo zinatumia
umeme wa jua na wana uzoefu wa kufanya kazi katika Tasnia ya Maziwa hususan
usambazaji wa mashine na vifaa vya kukusanyia na kusindika maziwa kwa miaka 35
katika nchi mbalimbali ikiwemo nchi za Ulaya, Asia, na Afrika. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe na Msajili wa Bodi ya Maziwa,
Prof. George Msalya.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya
Contractus, Bw. Witold Karczewski wakati wa mazungumzo yao kuhusu uwekezaji
katika sekta ya maziwa yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya waziri huyo jijini
Dar es Salaam mapema leo Januari 18, 2024. Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Prof.
Riziki Shemdoe na kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya
Wafanyabiashara ya Poland ambaye pia ni Meneja Mauzo wa Kampuni, Bw. Adam
Borawski.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu
Mwenyekiti wa Kampuni Contractus, Bw. Witold Karczewski (wapili kulia) muda
mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao kuhusu uwekezaji katika tasnia ya maziwa
yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya waziri huyo jijini Dar es Salaam mapema leo
Januari 18, 2024. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe. Wa
kwanza kushoto ni Msajili wa Bodi ya Maziwa, Prof. George Msalya na wa kwanza
kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya Poland ambaye pia ni
Meneja Mauzo wa Kampuni ya Contractus, Bw. Adam Borawski.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni