UJENZI WA BANDARI YA UVUVI MBIONI KUANZA
Na Saja Kigumbe Serikali imeweka wazi kuwa mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi unatarajia kuanza muda wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu. Bandari hiyo ambayo inatarajiwa kujengwa Wilayani Kilwa Masoko, Mkoani Lindi inatarajiwa kuwa chachu ya kuimarika kwa uchumi wa buluu nchini. Hayo yalibainishwa Machi 16, 2022 Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya uvuvi, Dkt. Erastus Mosha wakati wa mkutano wa wadau uliolenga kupitia rasimu ya taarifa ya upembuzi yakinifu wa mradi huo wa kimkakati. Alisema bandari hiyo itaiwezesha nchi kupata mapato kupitia meli za uvuvi na bidhaa zinazotokana na uvuvi zitauzwa hapa ndani na nje ya nchi. Dkt. Mosha alisema Serikali tayari imetenga fedha za kufanikisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa. “Tanzania hatujawahi kuwa na bandari ya uvuvi na hili limesababisha tumeshindwa kunufaika vya kutosha kupitia ras...