◾ Ni
kufuatia matokeo mazuri ya utekelezaji wa mradi wa ECF
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi amesema kuwa Wizara yake inakusudia
kukifanya kituo cha Utafiti wa Mifugo kanda ya Kaskazini cha West Kilimanjaro
kuwa kitivo cha Ubora kwenye uzalishaji wa mbuzi na kondoo walioboreshwa kwa
ajili ya kuwapa wafugaji nchini ili waweze kufuga kwa tija.
Prof. Mushi amesema hayo
leo Machi 05, 2024 baada ya kufika kwenye kituo hicho kilichopo chini ya Taasisi
ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) ambapo ameweka wazi nia ya Serikali
kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza kiwango cha nyama bora inayouzwa nje
kupitia kituo hicho.
"Kama mnavyotambua
nchi yetu kwa sasa imeongeza kasi katika kusafirisha nyama nje ya nchi na zaidi
ya asilimia 90 ya nyama tunayopeleka huko ni ya mbuzi na kondoo hivyo tuna kila
sababu ya kuongeza uzalishaji wa wanyama hao" Ameongeza Prof. Mushi.
Aidha Prof. Mushi
amemuelekeza Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Leonard Marwa na timu yake ya
wataalam kuongeza jitihada kwenye utafiti wa mbari, magonjwa, lishe na utunzaji
wa mifugo kwa ujumla ili kukifanya kituo hicho kuwa kitovu cha uzalishaji wa
mbuzi na kondoo bora watakaokidhi soko la ndani na nje ya nchi.
"Sisi kama Wizara
tunaona huu ndo wakati muafaka wa kuifanya nchi yetu kuwa kinara kwenye
uzalishaji wa mbuzi na kondoo wengi na sio kwa idadi tu bali kwa ubora pia kwa
sababu wataalam tunao, ardhi nzuri tunayo na hali nzuri ya hewa tunayo"
Amesisitiza Prof. Mushi.
Hatua hiyo ya Serikali
kukifanya kituo hicho kuwa kitivo cha ubora kwenye uzalishaji wa mbuzi na
kondoo nchini inatokana na mafanikio yaliyopatikana kwenye utekelezaji wa mradi
wa ECF ambapo Serikali ilipeleka jumla ya mbuzi na kondoo 465 ili kuzalisha
mbegu itakayosambazwa kwa wafugaji nchini.
Mkurugenzi wa Kituo cha
Utafiti wa Mifugo kanda ya kaskazini cha West Kilimanjaro Dkt. Leonard Marwa
(kushoto) akimueleza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)
Prof. Daniel Mushi kuhusu utekelezaji wa mradi wa ECF muda mfupi baada ya Prof.
Mushi kufika kituoni hapo leo Machi 05, 2024 mkoani Kilimanjaro.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi akimuangalia mmoja wa ndama wa mbuzi
waliozalishwa kupitia mradi wa ECF kwenye kituo cha Utafiti wa Mifugo kanda ya
Kaskazini cha West Kilimanjaro muda mfupi baada ya kufika kituoni hapo leo
Machi 05, 2024 mkoani Kilimanjaro.