Wafugaji kutoka kijiji cha Msomera kilichopo Handeni mkoani Tanga leo februari 28, 2024 wametembea taasisi za Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Buhuri mkoani humo na ile ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya Mashariki ambapo wamefurahishwa na elimu ya ufugaji waliyoipata kwenye Taasisi hizo.
Akizungumza mara baada ya
kukamilisha ziara hiyo ya siku moja, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera Bw.
Martin Paraketi ambaye mbali na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na
Uvuvi na Taasisi zake kwa kuwawezesha fursa hiyo ya mafunzo amewataka wafugaji
wa kijiji chake kuwa mabalozi kwa wafugaji wengine kupitia yale waliyojifunza
kutoka kwa wataalam wa taasisi zake.
"Tunatambua Serikali
imetambua umuhimu wetu kuja kujifunza hapa ili tushirikiane na wataalam wake
kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wenzetu tuliowaacha huko hivyo nitoe rai kwa
wenzangu kila mmoja kutimiza wajibu wa kuelimisha kaya inayomzunguka kule
Msomera" Amesema Bw. Paraketi
Aidha Bw. Paraketi ameiomba
Serikali kuwashirikisha wananchi wa kijiji chake wakati wote wa utafiti wa
masuala mbalimbali yanayolenga ufugaji bora jambo ambalo anaamini litazidi
kuongeza ujuzi kwa wafugaji waliopo kijijini hapo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa TALIRI kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku amewahamasisha wafugaji hao
kuchangamkia fursa ya biashara ya malisho ya Mifugo inayoonekana kuongezeka
thamani kadri siku zinavyoenda.
"Kwa sasa mbegu za
malisho aina ya "cenchrus" zinauzwa shilingi 25,000 kwa kilo na hiyo
ni kwa bei ya Serikali lakini kwa upande wa Taasisi binafsi zinauzwa 35,000
hadi 40,000 kwa kilo hivyo niwaombe mgeukie na kwenye fursa hii itakayowasaidia
sana" Amesema Bw. Nziku.
Akizungumza wakati wa
kuhitimisha ziara hiyo, Mkugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa amesema kuwa ziara hiyo ni miongoni mwa
jitihada za Serikali kupitia Wizara yake katika kuhakikisha wafugaji wa kijiji cha
Msomera wanajifunza kwa vitendo namna ya kufanya ufugaji bora na wenye tija.
"Taasisi hizi ni zenu
na mnakaribishwa kuzitembela na kujifunza wakati wowote hata kama mtawezeshwa
na wadau wengine kufanya hivyo na sisi tunaangalia namna ya kuja kutoa mafunzo
kwenye vitongoji vya Olmolot, Urkung'u, Mkababu, katikati na eneo lote la
"area F" Ameongeza Dkt. Mwilawa.
Mbali na kupewa elimu ya
uzalishaji na utunzaji wa malisho bora ya mifugo, wafugaji hao wa kijiji cha
Msomera walipewa mbegu za malisho hayo ili wakapande kwenye eneo watakalotumia
kama shamba darasa kijijini kwao.
Mkurugenzi wa Utafiti,
Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa (kushoto)
akiwaelimisha wafugaji wa kijiji cha Msomera kuhusu kilimo cha Malisho bora ya
Mifugo walipofika kwenye Shamba la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI)
kanda ya Mashariki mkoani Tanga Februari 28, 2024.
Mkurugenzi wa Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku
(kushoto) akiwaeleza wafugaji wa kijiji cha Msomera kuhusu shughuli
zinazofanywa na TALIRI kwenye kanda hiyo muda mfupi walipowasili hapo februari
28, 2024 mkoani Tanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba (kushoto) akimkabidhi
Mwenyekiti wa kijiji cha Msomera Bw.Martin Paraketi sehemu ya mbegu za malisho
ya Mifugo zitakazopandwa kwenye shamba darasa la kijiji hicho wakati wa ziara
ya wafugaji hao kwenye Taasisi hiyo kanda ya Mashariki mkoani Tanga februari
28, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni