Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu imezindua awamu ya pili ya program ya Jenga kesho iliyo bora kwa wanawake na vijana kwa upande wa sekta ya Uvuvi maarufu kama “BBT-LIFE” tukio lililofanyika leo februari 23, 2024 kwenye Wakala ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Mbegani Bagamoyo mkoani Pwani.
Uzinduzi huo ambao
umetanguliwa na mafunzo ya siku 5 ya kubadili fikra kwa vijana na wanawake 300
waliochaguliwa kunufaika na awamu ya pili
program hiyo umefanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Uvuvi) Bi. Agness Meena ambaye amewasisitiza vijana hao kuhakikisha wanatumia
vema mafunzo kwa vitendo watakayopewa kwa muda wa miezi 3 kwenye vituo
walivypangiwa baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo ya Nadharia.
“Baada ya kukamilika kwa
mafunzo ya siku 5 ya “mind-set transformation” mnaenda kwenye mafunzo kwa
vitendo kwa muda wa miezi 3, nitoe rai kwenu wote mkazingatie yale yote
mtakayojifunza huko ili mkitoka huko muweze kujiajiri na kuajiri wenzenu ambao
hawakupata fursa ya kushiriki kwenye programu kwa awamu hii” Amesema Bi. Meena.
Bi. Meena ameongeza kuwa
lengo la Wizara yake ni kutengeneza vijana na wanawake watakaokuwa
wajasiriamali wakubwa kwenye upande wa sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji wa samaki
kwenye vyanzo vya asili vya maji chumvi
na baridi, mabwawa na kilimo cha zao la mwani.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Bw.Robert
Masingiri amebainisha kuwa utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya BBT-LIFE
ni sehemu ya utekelezaji wa program ya Taifa ya kukuza ujuzi nchini kupitia
kipengele cha mafunzo ya wanagenzi.
“Programu hii yote
inagharamiwa na Serikali na kila mwaka huwa inatenga kiasi cha Bil.9 kwa ajili
ya kuhakikisha vijana na wanawake wanapata ujuzi stahiki ili waweze kujiajiri
na mpaka sasa imeshatoa kiasi cha shilingi Bil. 5.5 kwa ajili ya utekelezaji wa
program hiyo” Amesizitiza Bw. Masingiri.
Akizungumzia namna Taasisi
yake ilivyojipanga kuwawezesha mikopo wahitimu wa program hiyo, Mwakilishi wa
benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Bw. Kezilahabi Jumanne amesema kuwa
walipata nafasi ya kutoa elimu ya uandaaji maandiko ya kibiashara kwa wanufaika
hao hivyo anaamini baada ya kuhitimu mafunzo hayo baadhi yao watakuwa wateja
wao wa moja kwa moja kupitia mikopo watakayowawezesha.
Wakizungumza kwa niaba ya
wanufaika wenzao wao, Mshiriki kutoka Zanzibar Bi. Samia Othman na mwingine
kutoka Kagera Bw. Marius Juvinali wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuingia
kwenye awamu ya pili ya programu ya BBT-LIFE ambapo wameahidi kuzingatia yale
yote watakayoelekezwa wakati wa mafunzo kwa vitendo kwenye vituo
walivyopangiwa.
Utekelezaji wa programu ya
“Jenga Kesho iliyo bora kwa wanawake na vijana kupitia sekta ya Uvuvi kwa mwaka
huu unafanyika kwa mara ya pili ambapo kwa mwaka jana Programu hii ilihusisha
vijana na wanawake 200 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya
pamoja na wanufaika wa BBT-LIFE waliokuwa na changamoto ya usikivu hafifu Bw.
Sayid Ngasa (kulia nyuma) na Bi. Maria Mahona (katikati nyuma) muda mfupi baada
ya uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika Leo Februari 23, 2024 Bagamoyo mkoani
Pwani. Kushoto nyuma ni Mtafsiri wao wa lugha ya alama Bw. Mmanga Haji. Wengine pichani ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Bw. Robert Masingiri
(kulia mbele) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Uvuvi (FETA)
Dkt. Semvua Mzighani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya
pamoja na wanufaika wa awamu ya pili ya programu ya BBT-LIFE (Uvuvi) muda mfupi
baada ya uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika Leo Februari 23, 2024 Bagamoyo
mkoani Pwani. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,
Vijana, Ajira na wenye ulemavu Bw. Robert Masingiri na kushoto ni Mtendaji Mkuu
wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni