◾
Wanufaika waanza kupigwa msasa
Serikali kupitia wizara ya
Mifugo na uvuvi imeanza kutekeleza programu ya "Jenga kesho iliyo bora kwa
wajasiriamali wanawake na vijana upande wa sekta ya Uvuvi kupitia mafunzo
yanayotolewa kwa vijana na wanawake 300 kutoka pande mbalimbali za nchi yaliyoanza kutolewa
februari 19, 2024 kwenye chuo cha mafunzo ya uvuvi (FETA) kampasi ya Mbegani
Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bi. Imelda
Adam amewataka washiriki wa programu hiyo kuzingatia yale yote watayoelekezwa
wakati wote wa mafunzo hayo ya nadharia yatakayofanyika kwa siku 5 ili waweze
kufanya vizuri watakapoenda vituoni kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
"Programu hii inalenga
kuwageuza wahitimu wa ngazi mbalimbali kwenye kada ya Uvuvi kuweza kujiajiri
badala ya kusubiri kuajiriwa na lengo la Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa
na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha vijana na wanawake wengi zaidi
wanawezeshwa kupitia programu hii" Amesema Bi Imelda.
Aidha Bi. Imelda amewataka
washiriki hao kutobweteka na kiasi cha fedha wanachopewa na Serikali kwa ajili
ya kujikimu wakati wote wa mafunzo na badala yake wajikite kwenye mtazamo wa
kuandaa kesho yao iliyo bora baada ya kuhitimu mafunzo hayo.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi
Mwandamizi kutoka Wizarani hapo Bw. Clemence Katunzi amewataka wanufaika hao
kuhakikisha elimu watakayoipata mara baada ya kuhitimu mafunzo huo wanaipeleka
kwenye jamii zinazowazunguka katika maeneo yao.
"Tutawapanga kwenye
vituo mbalimbali ambavyo vitakuwa jumuishi na awamu hii tutakuwa na vituo 17
ambapo kimoja upande wa Zanzibar na 16 vipo Tanzania bara" Ameongeza Bw.
Katunzi.
Utekelezaji wa programu ya
Jenga kesho iliyo bora kwa wajasiriamali wanawake na vijana awamu ya pili
unatarajiwa kuchukua miezi 3 mara baada ya kukamilika kwa mafunzo kwa nadharia
yanayofanyika kuanzia Februari 19-23, 2024.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Imelda Adam (kulia) akizungumza na wanufaika
wa programu ya BBT-LIFE (Uvuvi) awamu ya pili wakati wa ufunguzi wa programu
hiyo uliofanyika leo Februari 19, 2024 kwenye Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi (FETA)
kampasi ya Mbegani wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Afisa Uvuvi Mwandamizi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Clemence Katunzi (kulia) akifafanua namna programu
ya BBT-LIFE (Uvuvi) awamu ya pili itakavyotekelezwa wakati wa ufunguzi wa programu hiyo
uliofanyika leo Februari 19, 2024 kwenye Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi (FETA)
kampasi ya Mbegani wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni