- Pia Yawarasimishia ekari 200 walizokuwa wakimiliki awali kinyume na utaratibu.
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewapa wananchi wa
kijiji cha Kalimaji eneo lenye ukubwa wa ekari 1000 zilizokuwa zinamilikiwa na
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha West Kilimanjaro
kilichopo kanda ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro.
Akikabidhi eneo hilo kwa
kamati ya Usalama ya Mkoa huo leo Machi, 05, 2024 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi amesema kuwa Wizara yake
imeridhia kutoa eneo hilo na kurasimisha ekari 200 za awali zilizokuwa
zikitwaliwa na wananchi hao kinyume na utaratibu na kufanya kijiji hicho kuwa
na eneo lenye ukubwa wa ekari 1200.
"Mhe. Mwenyekiti wa
Kamati ya Usalama sisi kama Wizara tumeridhia kutoa eneo hilo la sehemu ya
kituo chetu cha Utafiti cha West Kilimanjaro na tunabariki taratibu zote za
kuwamilikisha wananchi wa kijiji hicho ziendelee" Amesisitiza Prof. Mushi.
Akizungumza kufuatia uamuzi
huo Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.
Nurdin Babu ameipongeza Wizara kwa uamuzi huo ambapo ameongeza kuwa hatua hiyo
inaakisi nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania kupitia shughuli za
uzalishaji kiuchumi zitakazofanywa na wananchi hao kwenye eneo walilopewa.
Uamuzi huo wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) ni
utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri
kilichoketi Agosti 07, 2021 ambapo kiliamua baadhi ya maeneo ya Serikali
kumegwa kwa manufaa ya wananchi ili waweze kuyatumia kwa shughuli zao za
kijamii na kiuchumi.
Katibu Tawala wa mkoa wa
Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (wa pili kushoto) na
timu ya wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) muda mfupi
kabla ya makabidhiano ya ekari 1000 za eneo la Kituo cha Utafiti wa Mifugo cha
west Kilimanjaro kwa wananchi wa mkoa huo leo Machi 05, 2024.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (wa pili kushoto) akifafanua
jambo ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda
(katikati) muda mfupi kabla ya kuikabidhi kamati ya Usalama ya Mkoa huo ekari
1000 za eneo la Kituo cha Utafiti wa
Mifugo cha West Kilimanjaro leo Machi
05, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni