Na. Edward Kondela
Serikali imesema katika
kipindi kifupi kijacho itahakikisha vibali vinavyohusu masuala ya uvuvi
vinatolewa kwa njia ya kieletroniki ndani ya siku saba.
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema hayo leo
(27.02.2024) katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, wakati
alipofanya kikao kifupi na baadhi ya wadau wa uvuvi wanaojishughulisha na
uuzaji wa nyavu za uvuvi.
Prof. Sheikh amesema kuwa
mfumo wa kutoa vibali kwa njia ya kieletroniki utawezesha kutolewa vibali ndani
ya siku saba ili kurahisisha huduma kwa wadau wa Sekta ya Uvuvi kupata vibali
popote walipo.
Ameongeza kuwa mikakati ya
wizara ni kwamba kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2023/24 inatarajia kuanza
rasmi utoaji wa vibali hivyo kwa nji ya kieletroniki.
Ameongeza kuwa nia ya
serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni
kupunguza ucheleweshaji wa vibali na kuifanya Sekta ya Uvuvi kuchangia kwa
kiasi kikubwa katika pato la taifa.
Katika kikao hicho pia
Prof. Sheikh amepata muda wa kuwaarifu wadau hao mikakati mbalimbali ya
serikali katika kukuza Sekta ya Uvuvi pamoja na kujibu hoja na maswali
mbalimbali kutoka kwa wadau juu ya kuimarisha sekta hiyo.
Baadhi ya wadau wa Sekta ya
Uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za uvuvi waliohudhuria kikao hicho,
wamepongeza namna serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyofanya
jitiohada mbalimbali za kukuza sekta hiyo ikiwemo ya kuhakikisha uwepo wa zana
bora za uvuvi.
Wamesema wako pamoja na serikali katika kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa ili kulinda rasilimali za uvuvi na kuomba uwepo wa mikakati zaidi ya kudhibitiwa kwa nyavu haramu ambao hazitakiwi nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh akizungumza na
baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi (hawapo pichani) wanaojishughulisha na uuzaji
wa nyavu za uvuvi ambapo amewahakikishia kuwa katika kipindi kifupi kijacho
serikali itaanza kutoa vibali vinavyohusu masuala ya uvuvi kwa njia ya
kieletroniki ndani ya siku saba. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za
wizara jijini Dar es Salaam. (27.02.2024)
Mratibu wa mradi wa
Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (TASFAM) kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nichrous Mlalila akisikiliza hoja mbalimbali
kutoka kwa wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za
uvuvi, wakati wa kikao alichohitisha Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara
ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (hayupo pichani) na wadau hao
kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam. (27.02.2024)
Picha ya pamoja ya
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed
Sheikh (wa tatu kutoka kulia, mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na
baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za
uvuvi na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, baada ya kikao
kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, kujadili
namna ya kuboresha sekta hiyo. (27.02.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni