Na. Edward Kondela
Serikali ya Tanzania
kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhiwa boti mbili kutoka Taasisi ya
Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya
kufanya doria na kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria.
Akikabidhiwa boti hizo
pamoja na injini tatu na redio maalum kwa ajili ya mawasiliano leo (04.03.2024)
jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Prof. Mohammed Sheikh amesema vifaa hivyo vitasaidia katika juhudi za serikali
kulinda, kuendeleza na kukuza rasilimali za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria na
Tanzania kwa ujumla.
Amesema anamshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea
kutoa fedha kwa ajili ya kukuza Sekta ya Uvuvi na kukuza mahusiano katika nchi
tatu za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zinatumia Ziwa Victoria.
Ameongeza kuwa lengo la
serikali ni kuhakikisha inalinda rasilimali za uvuvi huku akitaja hatua ambazo
zimechukuliwa ikiwemo ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Januari 30 mwaka
huu, ambapo aligawa boti za uvuvi za kisasa 55 kati ya 160, lengo likiwa ni
kuwawezesha wavuvi kuwa na vifaa bora kwa ajili ya uvuvi ndani ya Ziwa
Victoria.
Amebainisha kuwa LVFO
wameamua kuja na mradi wa pamoja ili kulinda rasilimali za uvuvi wakiwezeshwa
na Umoja wa Ulaya ili kuhakikisha samaki wanapatikana kwa wingi na kufikishwa
viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.
Pia, amesema baada ya
kukabidhiwa vifaa kutakuwa na mafunzo kwa maofisa ili kuhakikisha wanapambana
na uhalifu wa uvuvi haramu kwa kutumia njia za kisasa na kuwakamata wahalifu.
Kwa upande wake Bw. Lukunya
Edward akimwakilisha Katibu Mtendaji wa LVFO wakati wa kukabidhi boti hizo kwa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema vifaa hivyo vitatumika zaidi katika
kudhibiti uvuvi haramu na kutunza rasilimali za uvuvi.
Amefafanua kuwa katika kudhibiti
uvuvi haramu kutasaidia kukuza samaki kwa wingi na kuongeza upatikanaji wa
samaki na kuwezesha jamii zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria kunufaika na
mazao ya uvuvi.
Tanzania kukabidhiwa boti
mbili zenye thamani ya takriban Shilingi Milioni 100 pamoja na vifaa vingine
kwa ajili ya doria ndani ya Ziwa Victoria ni mradi uliopita kwenye Taasisi ya
Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo jumla ya
boti sita na injini tisa zimegaiwa kwa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (wa kwanza kulia)
akikagua boti mbili za doria kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa
Victoria, kabla ya kukabidhiwa boti hizo kwa serikali kutoka Taasisi ya Uvuvi
ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. (04.03.2024)
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (mwenye koti
jeusi, katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa boti mbili za
doria kwa serikali ili kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria.
(04.03.2024)
Moja ya boti za kudhibiti
uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria, iliyokabidhiwa kwa serikali kupitia Wizara
ya Mifugo na Uvuvi ikiwa kwenye majaribio, ambapo Tanzania imekabidhiwa boti
mbili zenye thamani ya takriban Shilingi Milioni 100 pamoja na vifaa vingine
kwa ajili ya doria ndani ya Ziwa Victoria kupitia mradi wa Taasisi ya Uvuvi ya
Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo jumla ya boti sita
na injini tisa zimegaiwa kwa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.
(04.03.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni