Na. Edward Kondela
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
inaendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwataka watendaji wa wizara hiyo kuendelea
kuwatembelea wadau wa Sekta ya Uvuvi ili kutatua changamoto zao.
Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi)
Bi. Agness Meena amebainisha hayo leo (28.02.2024) katika ofisi ndogo za wizara
jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha wadau wa viwanda na biashara ya mazao
ya uvuvi ili kusikiliza hoja zao na changamoto zinazowakabili.
Bi. Meena amesema wizara
inataka kupunguza changamoto zilizopo katika Sekta ya Uvuvi kwa kufanya
mikutano na wadau na kufanya maboresho yakiwemo ya kisera na kisheria ili sekta
hiyo izidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa.
Amebainisha kuwa kupitia hotuba
aliyotoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kugawa boti na vizimba
jijini Mwanza, amesema lengo la serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni
kutatua changamoto za sekta hiyo kupitia vikao endelevu.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema wizara imepokea maoni yote
yaliyotolewa na wadau hao na kwamba watahakikisha yanafanyiwa kazi na kwamba
katika kikao kijacho hoja zao zitakuwa zimefanyiwa kazi.
Amesema katika kikao hicho
wadau hao hawapaswi kukata tamaa kwa kuwa baadhi ya hoja huenda zikawa
zinafanyiwa kazi hatua kwa hatua hadi kufikia muafaka.
Nao baadhi ya wadau wa
viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi waliohudhuria kikao hicho wamepongeza
namna serikali inavyoendelea kuwajali na kuwapa fursa ya kuwasikiliza huku
wakishauri hatua zaidi ziendelee kuchukuliwa ikiwemo elimu dhidi ya uvuvi
haramu.
Wameongeza kuwa kwa sasa
serikali imechukua hatua kubwa katika kulinda rasilimali za uvuvi huku wakiomba
kuboreshwa zaidi kwa mazingira ya uwekezaji ili wapate masoko zaidi ya mazao
hayo hususan nje ya nchi.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na vikao vya kukutana na wadau wa Sekta ya Uvuvi maeneo mbalimbali nchini ili kupata maoni na hoja za wadau hao ili zifanyiwe kazi lengo likiwa ni kukuza zaidi na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi)
Bi. Agness Meena akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa viwanda na biashara
ya mazao ya uvuvi kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es
Salaam, ambapo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kutekeleza agizo la
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la
kuwataka watendaji wa wizara hiyo kuendelea kuwatembelea wadau wa Sekta ya
Uvuvi ili kutatua changamoto zao. (28.02.2024)
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh akizungumza wakati
wa kikao cha wadau wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi kilichofanyika
katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, ambapo amewahakikishia wadau
hao kuwa maoni yao yatafanyiwa kazi na kupatiwa mrejesho katika vikao vijavyo
ili kukuza Sekta ya Uvuvi nchini. (28.02.2024)
Picha ya pamoja ya Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bi. Agness Meena (wa tano kutoka
kulia, mstari wa kwanza) akiwa na baadhi ya watendaji kutoka wizarani na wadau
wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi, baada ya kikao kilichofanyika katika
ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam ili kusikiliza maswali na hoja zao
katika kukuza Sekta ya Uvuvi nchini. (28.02.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni