Na. Edward Kondela
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kutoa jicho la pekee katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kwa kuongeza
mabwawa ya kunyweshea mifugo na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii
kulinda malisho.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt.
Mpango amebainisha hayo leo (10.02.2024) Wilayani Longido akiwa kwenye ziara ya
kikazi wakati akizindua Kituo cha Afya Ketumbeine na mradi wa kusambaza umeme
vijijini awamu ya tatu mzunguko wa kwanza unaotekelezwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA).
Ameongeza kuwa mabwawa
yanayoonesha udhaifu yakarabatiwe na hiyo ndiyo itakuwa zawadi kwa wakazi wa
Wilaya ya Longido kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan.
“Ndugu zangu hawa ni
wafugaji, mmeanza kazi vizuri lakini, ninawataka tena kutoa jicho la pekee kwa
Wilaya ya Longido, kuongeza mabwawa ya kunyweshea mifugo yao na kushirikiana na
Wizara ya Maliasili na Utalii kulinda malisho na mabwawa yanayoonesha udhaifu
yakarabatiwe.” Amesema Mhe. Dkt. Mpango
Mhe. Dkt. Mpango
amebainisha hayo baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Arusha Bw. Thomas Ole Sabaya kumueleza Makamu wa Rais kuwa wafugaji hawana kazi
nyingine zaidi ya kufuga hivyo wanategemea sana maeneo yao kwa ajili ya kufuga
na malisho.
Pia, ameiomba serikali
iwasaidie kuweka utaratibu ukiwemo wa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye
maeneo yao ili kulinda maeneo ya malisho wakati wote hali itakayoondoa ufugaji
wa kuhamahama na kusababisha migogoro maeneo mengine.
Naye Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema wizara imeendelea kusogeza huduma
mbalimbali kwa wafugaji wa Wilaya ya Longido ikiwa ni pamoja na kuchimba
mabwawa makubwa kwa ajili ya kusambaza maji kwa mifugo pamoja na majosho.
Mhe. Mnyeti amefafanua kuwa
katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 serikali imetenga Shilingi Milioni 46
kwa ajili ya kujenga majosho mawili katika vijiji vya jirani pamoja na josho
kubwa ambalo tayari limezinduliwa mwaka jana.
Aidha, amesema kutokana na
ukame katika baadhi ya maeneo serikali itahakikisha inaendelea kusogeza maji
karibu kwa kushirikiana na Wizara ya Maji ili wafugaji waweze kupata maji kwa
ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo.
Pia, amesema wizara kwa
sasa inaendelea kuhamasisha ujengaji wa mabwawa ya kufugia samaki na kuiasa
jamii ya kimasai kula samaki kama ambavyo baadhi yao wameanza kula.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt.
Philip Mpango akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Wilaya ya Longido Mkoani
Arusha, ambapo aliambatana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango amezindua pia mradi
wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Longido Samia, utakaogharimu
Shilingi Bilioni Tatu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa uzinduzi
wa Kituo cha Afya Ketumbeine na mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu
mzunguko wa kwanza unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika
Wilaya ya Longido Mkoani Arusha, ambapo ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi
kutoa jicho la pekee katika wilaya hiyo kwa kuongeza mabwawa ya kunyweshea
mifugo na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kulinda malisho.
(10.02.2024)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza katika ziara ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Wilaya ya
Longido Mkoani Arusha, ambapo amesema wizara imeendelea kusogeza huduma
mbalimbali kwa wafugaji wa Wilaya ya Longido ikiwa ni pamoja na kuchimba
mabwawa makubwa kwa ajili ya kusambaza maji kwa mifugo pamoja na majosho.
(10.02.2024)
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi
mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti
(kulia) wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Longido Mkoani
Arusha. (10.02.2024)
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa kwenye moja ya picha za
pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Alexander Mnyeti, wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Longido
Mkoani Arusha. (10.02.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni