Nav bar

Alhamisi, 4 Aprili 2019

MWEKEZAJI MKOANI MARA KUJENGA KIWANDA CHA NYAMA.




Mwekezaji katika sekta ya mifugo mkoani Mara, Mh. Vedastus Matayo, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Musoma mjini, baada ya kutembelewa na Dawati la sekta binafsi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ameamua kuanzisha kiwanda cha nyama mkoani hapo ili kuboresha soko la mifugo katika mkoa huo  na ajira watanzania.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Mbunge huyo wakati alipotembelewa na Dawati la sekta binafsi  katika maeneo ya shughuli zake za ufugaji Wilayani Sengereti na Bunda, kwa lengo la kuibua na kushawishi kuwekeza kibiashara kwa Mbunge  huyo.

Mbunge huyo aliwambia wataalam hao wa Dawati kuwa ana mifugo aina, Ng’ombe zaidi ya 2000 aina ya Borani ambao ndiyo wengi na aina nyingine ya semental ambao ni wachache, mbuzi zaidi ya 2500 na kondoo zaidi ya 1000, mifugo yote hii iko wilaya za Bunda na Sengereti.

Aidha aliwaeleza aina ya ufugaji anaofuga wa kugoresha mifugo hiyo ya asili kwa njia ya uhimilishaji kwa kuchukua mbegu bora za mifugo toka NAIC Arusha na kuja kuchanganya na ng’ombe wetu majie wa asili ili kupata ng’ombe chotara mwenye uwezo wa kutoa nyama nyingi na maziwa mengi kuliko wale wa kienyeji.

Aliwaeleza wanadawati hilo la sekta  binafsi kuwa kwa kufanya hivyo ameweza zalisha mifugo mingi ambayo soko lake likawa ni changamoto, hivyo kuhitaji kuwa na kiwanda cha kuchakata nyama mkoa wa Mara.

Akizungumzia soko la mifugo hiyo baada ya kuizalisha kwa wingi na kuinenepeshamifugo hiyo alisema kuwa anauza kwa wenyeji wenye mabucha mkoani Mara na wakati mwengine huwauza nchi, nchini Kenya ng’ombe wa nyama.

Aidha kwa upande wa ng’ombe wa maziwa ambapo chotara hutoa maziwa mengi kiasi kuliko wale wa asili hufanya matumizi ya familia yake na wafanyakazi katika shughli zake za ufugaji na kilimo.

Kutokana na rasilimali hiyo kubwa aliyokuwanayo bwana Matayo ya mifugo na soko la mifugo hiyo ni changamoto kutegemea mkoa wa Mara tu na nchi jirani, dawati la sekta binafsi walimshauri kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama ili rasilimali ya mifugo mingi aliyo nayo ipate soko  katika kiwanda hicho.

Vilevile wataalam wa dawati walisema akianzisha kiwanda atazalisha bidhaa zitokanazo na nyama na kuziuza kwa bei yenye manufaa kwa vile atakuwa ameongeza thamani badala ya kuuza malighafi ya ng’ombe hai au mifugo hai, Mh. Matayo alikubaliana nao na kuahidiwa atapatiwa mkopo toka Banki ya maendeleo ya kilimo (TADB) na watashirikiana naye kuandaa andiko la mkopo huo wenye riba nafuu.



Mh. Mbunge wa Musoma mjini Mh. Vedastus Mathayo akiwa ofisini kwake akiongea na wataalamu wa dawati la sekta binafsi ambao hawaonekani pichani.

SERIKALI IMEANDAA SHERIA MPYA YA UKUZAJI VIUMBE MAJI




Serikali imeandaa sheria mpya ya ukuzaji viumbe maji ili kuboresha sheria ya zamani ya uvuvi ya namba 22 ya mwaka 2003 ikiwa ni hatua itakayosaida kuweka mazingira bora kwa ajili ya wadau wa uvuvi na kuweza kutambua idara ya ukuzaji viumbe maji

Haya yalibainishwa jana na Katibu Mkuu wa sekta ya uvuvi Dkt. Rashidi Tamatama  Wakati akifungua mkutano wa kutoa maoni kwa wadau wa uvuvi toka kanda ya  kati Dodoma kwenye ukumbi ya Holly Cross Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa sheria hiyo mpya ya ukuzaji viumbe maji itajenga mazingira mazuri kwa wadau wa uvuvi kufanya kazi zao bila vikwazo.

Aliendelea kusema kuwa sheria mpya itasaidia kujenga serikali ya awamu 5 ya uchumi wa viwanda vya kati katika sekta ya uvuvi.

Katibu Mkuu huyo aliwaambia wadau hao kuwa serikali itawezesha sheria hiyo ya ukuzaji viumbe maji ili kufikia mahitaji sera ya Taifa ya uvuvi ya mwaka 2015 ilivyosema mikakati imeelekezwa kuendeleza rasilimali ya mazao ya baharini ikiwemo samaki.

Dkt. Tamatama alisema kuwa sera ya Taifa ya Uvuvi pia inalenga kuendeleza ukuaji viumbe maji ambavyo ni pamoja na kuunda rasilimali ya samaki pamoja na viumbe wengine wa baharini.
Aidha alisema sheria mpya itasaidia nchi kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika sekta ya uvuvi.

Vilevile Katibu Mkuu Dkt. Tamatama amesema sheria mpya itasaidia kuipatia serikali uhalali wa kufanya kazi ili kuboresha ulinzi wa rasilimali ya uvuvi na mazao yake.

Hivyo Katibu Mkuu huyo alisema sheria hii inakuja kwa wakati muafaka, wakati idadi kubwa ya wanajihusisha na ufugaji wa samaki kama chanzo cha kuongeza kipato cha maisha yao.
Mkutano huo uliwakutanisha wavuvi, wafanyabiashara ya samaki ambao walitoa maoni yao mbalimbali ili kuboresha rasimu ya sheria hiyo mpya kabla ya kwenda bungeni kujadiliwa na kupitishwa.



Katibu Mkuu sekta ya uvuvi Dkt. Rashid  Tamatama  akifungua mkutano wa wadau wa uvuvi wa kutoa maoni ya sheria mpya

ZOEZI LA UOGESHAJI WA MIFUGO KANDA YA KATI

WIZARA ya mifugo na uvuvi, imeandaa mikakati ya kuboresha sekta ya mifugo hapa nchini, moja ya mkakati huo ni ule wa kudhibiti magonjwa ya mifugo ambapo imewahimiza wafugaji kuzingataia matumizi ya majosho yenye dawa za kuogesha ng’ombe ili kutokomeza magonjwa yatokanayo na kupe.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na Naibu Waziri wa mifugo na uvuvi Mheshimiwa Abdalah Ulega wakati wa zoezi la uhamasishaji wa uogeshaji wa ng’ombe kanda ya kati mkoani Singida, katika kijiji cha Mgori kilichopo halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini.

Katika uhamasishaji huo waziri Ulega aliwataka wafugaji kufanya zoezi la uogeshaji wa mifugo uliyoanzishwa uwe wenye tija na endelevu, kwa vile hivi sasa hakuna sababu za kushindwa kuogesha mifugo  yao katika majosho yenye dawa ya kudhibiti  kupe yaliyotolewa na serikali bure.

Alisema hivi sasa serikali katika zoezi hili, imetoa dawa bure kwa halmashauri zote nchini, na kukarabati majosho yote yaliyokuwa hayafanyi kazi, ili wafugaji waweze kuogesha mifugo yao, kukinga ugonjwa hatari unaoenezewa na kupe, ambao unaoongozwa katika vifo vya ng’ombe hapa nchini.

Hapo, mwanzo shughuli hizo zilikuwa zikifanywa kwa kutofuata taratibu nzuri za makusanyo yalikuwa yakitoka kwa wafugaji walipokuwa wakipata huduma za kuogesha mifugo yao, hazikuwa na taarifa ya mapato na matumizi na hivyo kushindwa kuwa na utaratibu endelevu wa shughuli hiyo, majosho mengi yalisimama kufanya kazi na mifugo haikugoeshwa.

Katika kampeni hii ya uhamasishaji wa uogeshaji wa mifugo, tozo imepunguzwa ambapo hivi sasa kila ng’ombe anaogeshwa katika majoshi ni shilingi 50 tu, huku nyuma uogeshaji ulikuwa unatozwa wastani wa shilling mia 200 kwa kila ng’ombe na kwa mbuzi ilikuwa shililngi 10.

“nyie wafugaji msikalie rasilimali hii ya mifugo mliokuwa mnayo, kwani ni uchumi mkubwa sana mliyokuwa nayo kwenu na pia kwa Taifa ili kuongeza mapato, yanayotokana na mifugo yenu” alisema mheshimiwa Ulega.

Aidha alifafanua kuwa ufugaji kwa kufuata taratibu za ufugaji wa kisasa na kibiahsra kwa kuvuna mifugo inapozidi katika eneo uliyokuwa nayo, itakusaidia kupata kipato katika kuboresha maisha yako na ya familia.  Uhamasishaji huu unafuatia uzinduzi wa kampeni ya uogeshaji wa mifugo, iliyofanywa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina  katika kijiji cha Buzirayombo Halmashauri ya Chato Mkoa wa Geita.

Naibu Waziri Wa Mifugo Na Uvuvi Mh. Abdallah Ulega, katikati mwenye shati la rangi ya bluu  akiandaa dawa ya josho ili kuogesha mifugo


MIGOGORO MIKUBWA 14 KATI YA 29 YATATULIWA NA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara kupitia timu yake maalum ya kushughulikia migogoro, hadi sasa imetatua migogoro mikubwa 14 kati ya 29 inayohusisha wakulima na wafugaji pamoja na hifadhi na wawekezaji.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Bw. Lengai Ole Sabaya pamoja na viongozi wengine wa wilaya hiyo, mara baada ya kuarifiwa kuwepo kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Hai na kubainisha kuwa ni hatari kwa jamii inayoishi pamoja kuwa na mgogoro wa aina hiyo.

“Nitamsisitiza katibu mkuu mifugo aliangalie kwa karibu sana hili kwa sababu ni hatari sana kwa jamii inayoishi pamoja kutokuwa na maelewano ya kuachiana maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.” Alisema Mhe. Ulega

Mhe. Ulega ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya kumuarifu kuwa baadhi ya maeneo yenye migogoro ni Kata ya KIA ambapo wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao katika maeneo ya uwanja wa ndege wa KIA, pamoja na wakulima wilayani humo kutotaka kuwaachia wafugaji maeneo wasiyoyatumia kwa kilimo hususan yenye magadi kwa ajili ya malisho kwa wafugaji hivyo kutengeneza chuki dhidi yao.

Naibu Waziri Ulega amemshauri pia mkuu huyo wa wilaya kutumia Chuo cha Mifugo Tengeru na Kituo cha Uhimilishaji cha Taifa (NAIC) vilivyopo Mkoani Arusha ili kuleta mabadiliko kwa wafugaji katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro kwa kuwa na ng’ombe wachache na wenye tija ukizingatia ukanda huo kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinahitaji maziwa kwa wingi katika uzalishaji wao.

“Ukanda huu kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinahitaji lita laki moja ya maziwa kwa siku na bado hayatoshelezi hadi inawalazimu kuchukua maziwa kutoka mikoa ya Iringa na Njombe ni vyema mkashirikiana na wizara kutoa elimu ili wafugaji wa wilaya hii wabadilike kwa kufuga kisasa hususan ng’ombe wa maziwa badala ya kuwa na ng’ombe wengi wasio na tija kiuchumi.” Alisema Mhe. Ulega

Naibu Waziri Ulega amemshauri pia mkuu wa wilaya Bw. Sabaya kuwa na kampeni maalum ya kutoa elimu kwa wafugaji pamoja na kushirikiana na wataalam ili wilaya hiyo iwe ya mfano katika kubadilisha fikra za wafugaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya amesema changamoto kubwa zilizopo wilayani hapo ni mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ambao tayari upo katika hatua mbalimbali za kutatuliwa pamoja na wafugaji kutokuwa tayari kubadilika kutoka kwenye ufugaji wa zamani wa kuwa na makundi makubwa ya mifugo isiyo na tija.

Kufuatia mazungumzo baina yake na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ulega, mkuu huyo wa wilaya amesema atazidi kushirikiana na wizara hiyo ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatulika na kuifanya wilaya hiyo kuzidi kunufaika na mifugo iliyopo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akifafanua jambo kwa viongozi wa Wilaya ya Hai (hawapo pichani) namna ya kuiboresha sekta ya mifugo wilayani humo




Baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Hai, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya wakiwasilisha hoja mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega


WANANCHI WAONYWA KUTOTUMIA VIBAYA MATAMKO YA RAIS WA NCHI, KUKWEPA KODI



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wananchi hususan wafugaji kutotumia matamko ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli vibaya kwa kutafuta mianya ya kutolipa kodi.

Prof. Gabriel amebainisha hayo akiwa katika mnada wa upili wa Meserani uliopo wilaya ya Monduli Mkoani Arusha mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa watumishi waliopo katika mnada huo na kusikiliza kero za wafugaji.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kufanya ziara hiyo Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha mwezi mmoja itashirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kutoa tafsiri sahihi ya mfanyabiashara mdogo anayestahili kukatiwa kitambulisho cha biashara ndogo ndogo (machinga) cha Shilingi Elfu Ishirini kwa mwaka, kilichotolewa na Rais Magufuli kutokana baadhi ya wafugaji kutaka kufahamu endapo wanastahili kupatiwa vitambulisho.

“Mheshimiwa rais alikuwa amelenga hasa wale wafanyabiashara wadogo wadogo na tunachoamini tutaendelea kulifanyia kazi lakini suala la machinga kwamba naye mfanyabiashara wa ng’ombe kuhusishwa katika sifa za mfanyabiashara ndogondogo bado ni gumu kulitolea majibu, lakini ushauri tusitumie matamko ya rais vibaya tusitafute kichaka cha kujificha kwamba nawe ni machinga, wewe mwenyewe fikiria na jitafakari tulipe kodi na tujenge nchi yetu.” Alisema Prof. Gabriel

Akizungumza na wafugaji hao Prof. Gabriel amepokea kilio cha wafugaji kuwa wamekuwa wakiuza ng’ombe kwa makadirio au matakwa ya mnunuzi kutokana na kutokuwepo kwa mizani ili waweze kuuza ng’ombe kwa kilo badala ya bei ya kukadiria kati ya mfugaji na mnunuzi wa ng’ombe, kitendo ambacho wafugaji hao wamesema kimekuwa kikiwafanya wasiuze mifugo yao kwa bei yenye tija kwao.

“Lengo letu ni kuhakikisha minada yote hasa ya upili na ile ya mipakani inatumia mizani, mnada wa Kimesera mzani wake uko tayari unatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuondokana na bei ya kukisia katika kipindi cha mwezi mmoja.” Alisema Prof. Gabriel

Aidha katibu mkuu huyo, amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuhakikisha wanawapatia ng’ombe malisho bora ili wapate mazao bora ya mifugo yao huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikihakikisha inaendelea kuimarisha matibabu ili mifugo iwe na afya bora.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema pia licha ya uwepo wa masoko ya mifugo hususan ng’ombe hapa nchini, wizara inajikita katika kutafuta masoko ya mifugo nje ya nchi.

“Tunachoangalia hivi sasa ni kuangalia na masoko ya nje ya nchi lakini hauwezi kuuza ng’ombe nje ya nchi ambaye hana afya bora na tunaamini tukiendelea hivi hata mchango wetu wa wizara kwenye uchumi wa viwanda utakuwa ni mzuri.” Alisema Prof. Gabriel

Naye Bw. Kandidi Mlinyi ambaye ni msimamizi wa mnada wa Meserani amesema kuwa wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika ukanda wa Wilaya ya Monduli hivyo kuwa na mazingira magumu ya upatikanaji wa huduma hiyo mnadani.

Kauli hiyo imeungwa mkono na baadhi ya wafugaji ambao wamesema ng’ombe wanaposafirishwa kutoka maeneo mbalimbali kuja katika mnada huo, kwa wastani wanakunywa maji lita 20 hadi 60 lakini kutokana na ukosefu wa maji ng’ombe wanakuwa katika mazingira magumu hali inayosababisha ng’ombe hao kuchoka kwa kuwa wanapoteza maji mengi mwilini.

Katika ziara hiyo ya Katibu Mkuu Prof. Gabriel wafugaji wamepongeza utendaji kazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwa viongozi na watendaji wa wizara wamekuwa wakifika mara kwa mara kwa wananchi wakiwemo wafugaji ili kutatua kero zao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika uongozi wa mnada wa Meserani kwa siku zaidi ya ng’ombe 500 huuzwa na kusafirishwa kwenda katika mikoa mbalimbali wakati wa msimu ambao unakuwa na ng’ombe wengi kuanzia mwezi Machi hadi Julai kila mwaka.



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gariel akikagua ubora wa baadhi ya ng'ombe waliofikishwa katika mnada wa Meserani


 

YALIYOJIRI KATIKA MKUTANO WA KUJADILI AFYA YA WANYAMA DUNIANI ULIOFANYIKA MJINI HAMMAMET, TUNISIA.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) amehudhuria Mkutano Mkuu wa 23 wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) Kamisheni ya Afrika, uliofanyika Mjini Hammament nchini Tunisia.

Mkutano huo uliojumuisha nchi zaidi ya 25 za bara la Afrika zikiwemo Zambia, Zimbabwe, Misri, Kenya, Uganda, Tunisia na Chad ulikuwa na malengo ya kuangalia afya ya wanyama, haki za wanyama, uzalishaji wa mifugo na usalama wa chakula kitokanacho na mifugo na kutoa mapendekezo kulingana na kanuni za shirika hilo duniani.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) akiambatana na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa wizara hiyo Dkt. Hezron Nonga amepata fursa ya kufanya kikao cha ana kwa ana na uongozi mkuu wa Shirika hilo la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kwa kuzungumza na rais wa shirika hilo Dkt. Mark Schipp, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Monique Eloit na mwakilishi wa shirika hilo kwa Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Afrika Dkt. Samuel Wakusama.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Ulega ameshukuru uongozi huo kwa ushirikiano wake na Tanzania kwa kuendelea kuisaidia nchi katika miradi mbalimbali ya kulinda afya za wanyama hapa nchini.

Aidha ameelezea nafasi ya Tanzania katika rasilimali za asili ikiwemo mifugo na uvuvi ambapo kwa upande wa mifugo ametoa takwimu za mifugo iliyopo nchini pamoja na vikwazo ambavyo sekta ya mifugo inakabiliana navyo yakiwemo magonjwa, kasi ndogo ya mifugo kuzaliana (Poor Breeding) na uzalishaji duni (Low Productivity) hali ambayo inasababisha nchi kushindwa kusafirisha mifugo na mazao yatokanayo na mifugo kama vile nyama kwenda katika masoko ya nje ya nchi.

Mhe. Naibu Waziri Ulega ameliomba Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kuisaidia nchi ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto hizo ili kukuza uchumi na kipato cha wadau wa sekta ya mifugo ambapo kwa pamoja uongozi huo umeahidi kuzifanyia kazi.

Licha ya mazungumzo hayo, Mhe. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Hamis Ulega (MB) kupitia kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Dkt. Hezron Nonga, amewakabidhi andiko linalofafanua kwa kina sekta ya uvuvi nchini, changamoto zake na maeneo yenye uhitaji ili kuuwezesha uongozi huo kuendelea katika hatua ya utekelezaji.

Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Naibu Waziri Ulega ameueleza uongozi wa OIE kuhusu nia ya Tanzania kuandaa mkutano ujao kwa kuwa ni nchi yenye mifugo na wanyamapori wengi, mazingira mazuri ya uwezekaji na taasisi maalum zinazoshughulikia masuala ya viwango, ubora wa bidhaa na usalama wa chakula.

Katika kutathmini afya za wanyama, wataalamu wamejadili magonjwa mbalimbali ya wanyama yaliyopo katika bara la Afrika hususan kwa nchi wanachama, athari na namna yakuyakabili yakiwemo magonjwa ya miguu na midomo (FMD), Kichaa cha mbwa na homa ya Bonde la Ufa (RVF).

Aidha kikao kimetathmini kwa pamoja miradi mbalimbali yenye lengo la kuimarisha afya za wanyama pamoja na michango ya wahisani ikiwemo Benki ya Dunia, Mchango wa Wataalam wa Kati wa Mifugo (Veterinary Paraprofessionals) na nafasi yao katika kuimarisha huduma za afya ya wanyama katika Bara la Afrika.


Kikao cha ana kwa ana kati ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) (wa pili kutoka kulia) na Uongozi wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE). Kutoka kushoto: Mwakilishi wa OIE Kanda ya Kusini mwa Afrika Dkt. Samuel Wakusama, Rais wa OIE na Kamisheni ya Australia Dkt. Mark Schipp na Mkurugenzi Mkuu wa OIE Dkt. Monique Eloit na Mkurugezi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (wa kwanza kulia) Dkt. Hezron Nonga.



MAKUBALIANO KATI YA SERIKALI NA BILL AND MELINDA GATES YATAKIWA KUTEKELEZWA




Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha mikakati ambayo serikali imekubaliana na Taasisi ya Bill and Melinda Gates katika sekta ya mifugo inatekelezwa kama walivyokubaliana.

Naibu Waziri Ulega amesema hayo ofisni kwake jijini Dodoma alipotembelewa na ujumbe kutoka Taasisi ya Bill and Melinda Gates katika ofisi za wizara hiyo na kubainisha kuwa serikali inahakikikisha Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Mifugo Tanzania unatekelezwa na kuishukuru taasisi hiyo kwa kutoa mchango mkubwa katika mpango huo.

“Sisi tuko pamoja na nyinyi na tunathamini makubaliano yetu na hatuwezi kuvunja makubaliano yetu ninawahakikishia kuwa nitamuagiza katibu mkuu afanye ufuatiliaji wa karibu sana kuhakikisha kwamba sisi tuna mikakati yetu tunayoifanya  lakini hii mikakati yote inaenda sambamba na kile tulichokubaliana.” Alisema Mhe. Ulega

Naibu Waziri Ulega pia amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa karibu katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kulinda rasilimali za nchi kwa kutumia Operesheni Nzagamba na Operesheni Sangara ili kuondoa mambo yaliyokuwa yakifanywa bila utaratibu na kuisababishia serikali hasara.

“Tunafanya ulinzi wa rasilimali na kuondoa ule uholela na kuhakikisha kuwa zile sheria, taratibu na kanuni zinafuatwa sana kwa sababu hata masoko ya kimataifa yalitaka uholela usiwepo, mambo yawe katika utaratibu wa kisheria na kanuni zinazoongoza sekta.” Alisema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inahakikisha katika operesheni hizo sheria, kanuni na taratibu za sekta za mifugo na uvuvi zinafuatwa ili sekta hizo ziweze kusonga mbele kwa kumuwekea mazingira mazuri mwananchi ili aweze kufaidika na nchi iweze kuongeza pato la taifa.
Akizungumza katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na wakuu wa idara kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kusimamiwa ikiwemo elimu ili wafugaji waweze kunufaika kupitia sekta hiyo.

“Ningependa katika ushirikiano wetu huu tuzidi kushirikiana katika kutoa elimu kwa wafugaji wetu tuwe na ufugaji wenye tija, lakini eneo lingine la pili ni usimamizi dhidi ya magonjwa, la tatu ni kuwawezesha wafugaji wetu kiuchumi lakini la nne ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Mifugo Tanzania.” Alisema Prof. Gabriel

Prof. Gabriel pia ameainisha mambo mengine kuwa ni umuhimu wa kufanyika kwa tafiti, usimamizi na uhakikishaji wa uzalishaji bora wa mifugo ili sekta ya mifugo iweze kuwa na maendeleo endelevu.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Programu Mwandamizi wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki Bibi Mercy Karanja, Mshauri Mwelekezi kutoka taasisi hiyo nchini Tanzania Prof. Marcellina Chijoriga amesema Taasisi ya Bill and Melinda Gates bado itaendelea kufanya kazi nchini kwa kufuata mpango wa serikali.

Aidha Prof. Chijoriga ameshukuru uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao umekuwa ukitoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi hiyo na kutoa ombi kwa uongozi wa wizara kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Bill and Melinda Gates ili iweze kuleta matokeo chanya kwa wafugaji nchini.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka Taasisi ya Bill and Melinda, Mercy Karanja (kulia) na Mshauri Mwelekezi wa taasisi hiyo Prof. Marcellina Chijoriga




NMB YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WIZARA KUKUZA SEKTA YA MAZIWA



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa kutokana na taarifa iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP)
Prof. Gabriel amebainisha hayo Jijini Dodoma, akiwa kwenye kikao na maafisa kutoka idara ya kilimo ya Benki ya NMB, waliofika ofisini kwake kumwelezea mikakati ya Benki ya NMB ambayo imekuwa ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya maziwa lengo likiwa ni kutaka kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani ni kwamba kwa wastani angalau mtu anatakiwa walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za maziwa lakini kwa bahati mbaya kwa watanzania wastani ni lita arobaini na saba tu, bado tuna kazi kubwa sana.” Alisema Prof Gabriel
Prof. Gabriel amesema Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la Sekta Binafsi ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi, ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa yanatumika ipasavyo.
Katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu mkuu huyo pia amesema ni wakati muafaka kwa Benki ya NMB kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji, hususan wafugaji wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.
Aidha Prof. Gabriel amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa tafiti kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo ili tafiti hizo ziweze kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya kwa wafugaji.
“Ningependa sekta hii ya mifugo, iwe pia na tafiti nyingi zinafanyika, sasa tukifanya hizo tafiti tutaweza kuleta mabadiliko chanya na yenye uhakika katika maendeleo ya wafugaji kwa sababu lengo siyo tu kufanya jambo, lakini liwe jambo ambalo linaweza kugusa maisha ya wafugaji.”  Alisema Prof. Gabriel
Katika kikao hicho pia Katibu Mkuu Prof. Gabriel ameshauri uwepo wa mahusiano ya karibu kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Benki ya NMB na taasisi za elimu ya juu, ili kuhakikisha tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na wanafunzi ziweze kutumika katika kuleta mabadiliko na kuleta manufaa kwa wafugaji, badala ya tafiti hizo kuwekwa katika maktaba za vyuo hivyo pekee.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo Bw. Carol Nyagaro amesema kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli pamoja na utendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewalazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja wapya kupitia sekta mbalimbali.
“Kutokana na kasi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo.” Alisema Bw. Ngayaro
Aidha Bw. Nyagaro amesema Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo inafikiria pia kuwekeza katika sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi karibuni.
Bw. Nyagaro amemueleza pia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kuwa Muunganiko wa Vyama vya Ushirika Vikuu vya Maziwa Duniani unatarajia kufanya mkutano wake hapa nchini Tarehe 25 na 26 Mwezi Februari mwaka 2019 kwa kushirikiana na Benki ya NMB lengo kuu likiwa ni kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini.
Amefafanua kuwa muunganiko huo wenye nchi wanachama 95 ambao unafanya biashara ya takriban Dola za Marekani Bilioni 200 kwa mwaka, umeichagua Tanzania kwa ajili ya kufanya majadiliano kwa kuhusisha wadau wa sekta ya mifugo ili kuwekeza katika sekta ya maziwa.
Amesema mkutano huo pia utaainisha mambo ambayo tayari yalishafanyiwa tafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo.



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa kutoka NMB na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Jumatano, 3 Aprili 2019

WAZIRI MPINA ATEKETEZA NYAVU HARAMU TANGA




Waziri wa mifugo na uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ateketeza vipande vya nyavu haramu 773 zenye chini ya mil 10 ambazo zilikutwa katika maeneo ya Kigombe,Moa na Tanga Jiji Mkoani Tanga.

Kufuatia tukio hilo la uteketezaji wa nyavu haramu hizo Mhe Waziri wa Mifugo na Uvuvi amesema, jitihada zinazofanywa na serikali ni kuzuia uvuvi haramu na kulinda rasilimali za Wavuvi.  

“Tutahakikisha wavuvi wetu wanapata elimu juu ya uvuvi na kufata sheria, kanuni na taratibu za uvuvi zilizowekwa, alisema mpina.

Pia Waziri Mpina alisema kuwa tarehe 1/07/2019 kanuni mpya ya uvuvi zitaanza  kutumika ambapo itakuwa imeondoa changamoto ambazo zinazotukabili.

Waziri Mpina alisema pia, jitihada zinazofanywa na serikali ni kuzuia uvuvi haramu na kulinda rasilimali za Wavuvi.


“Tunatumia Bil.56 kila mwaka kuagiza Samaki kutoka nje ya Nchi”, alisema Mpina 

Waziri Mpina alisistiza kuwa nyavu zote zenye chini ya milimita 10 zikabidhiwe Wizarani na nyavu za kuanzia milimita 8 hazitaruhusiwa kuvuliwa na zitatakiwa zichomwe moto.

“Nyavu hizi ambazo hazitakiwi zinaua mazalia ya samaki na kuvua samaki wachanga wasioruhusiwa, anaevua kutumia uvuvi haramu katika mnyoro mzima wa shughuli za uvuvi hatapona”. alisema Mpina

Mpina alisema, tutaendelea kupambana na uvuvi haramu Kila mtu afate sheria na taratibu zilizowekwa na tunashirikiana na viongozi wetu kujua mahitaji na kutembelea wavuvi ili tuwasaidie wavuvi wetu. - Mpina

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Bw. Daudi Mayeji Wawekezaji uvuvi alisema, tukizingatia kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili tuwe na uvuvi wenye tija.

“Natoa elimu kwa wavuvi kuwa,wanavua samaki ambao hawastahili matokeo yake uzalishaji unakuwa mdogo”, alisema Bw. Daudi Mayeji.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luaga Mpina akiteketeza vipande vya nyavu haramu 773 mkoani Tanga