Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka
Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini
kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa kutokana na taarifa
iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP)
Prof. Gabriel
amebainisha hayo Jijini Dodoma, akiwa kwenye kikao na maafisa kutoka idara ya
kilimo ya Benki ya NMB, waliofika ofisini kwake kumwelezea mikakati ya Benki ya
NMB ambayo imekuwa ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya maziwa lengo likiwa ni
kutaka kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kwa takwimu ambazo
zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani ni kwamba kwa wastani angalau mtu
anatakiwa walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za maziwa lakini kwa bahati
mbaya kwa watanzania wastani ni lita arobaini na saba tu, bado tuna kazi kubwa
sana.” Alisema Prof
Gabriel
Prof. Gabriel amesema
Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia
Dawati la Sekta Binafsi ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta ya
mifugo na uvuvi, ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa
yanatumika ipasavyo.
Katika kikao hicho
ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Katibu mkuu huyo pia amesema ni wakati muafaka kwa Benki ya NMB kushirikiana na
Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji,
hususan wafugaji wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa
tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa
kuhamahama.
Aidha Prof. Gabriel
amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa tafiti kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa
kushirikiana na Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo ili tafiti hizo ziweze
kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya kwa wafugaji.
“Ningependa sekta hii
ya mifugo, iwe pia na tafiti nyingi zinafanyika, sasa tukifanya hizo tafiti
tutaweza kuleta mabadiliko chanya na yenye uhakika katika maendeleo ya wafugaji
kwa sababu lengo siyo tu kufanya jambo, lakini liwe jambo ambalo linaweza
kugusa maisha ya wafugaji.” Alisema
Prof. Gabriel
Katika kikao hicho pia
Katibu Mkuu Prof. Gabriel ameshauri uwepo wa mahusiano ya karibu kati ya Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Benki ya NMB na taasisi za elimu ya juu, ili kuhakikisha
tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na wanafunzi ziweze kutumika katika kuleta
mabadiliko na kuleta manufaa kwa wafugaji, badala ya tafiti hizo kuwekwa katika
maktaba za vyuo hivyo pekee.
Kwa upande wake Meneja
Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo Bw. Carol Nyagaro amesema
kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli pamoja na utendaji
wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewalazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna
ya kutafuta wateja wapya kupitia sekta mbalimbali.
“Kutokana na kasi ya
Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia
maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo.” Alisema Bw. Ngayaro
Aidha Bw. Nyagaro
amesema Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo inafikiria pia kuwekeza katika
sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi
karibuni.
Bw. Nyagaro amemueleza
pia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabriel, kuwa Muunganiko wa Vyama vya Ushirika Vikuu vya Maziwa
Duniani unatarajia kufanya mkutano wake hapa nchini Tarehe 25 na 26 Mwezi
Februari mwaka 2019 kwa kushirikiana na Benki ya NMB lengo kuu likiwa ni
kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini.
Amefafanua kuwa
muunganiko huo wenye nchi wanachama 95 ambao unafanya biashara ya takriban Dola
za Marekani Bilioni 200 kwa mwaka, umeichagua Tanzania kwa ajili ya kufanya
majadiliano kwa kuhusisha wadau wa sekta ya mifugo ili kuwekeza katika sekta ya
maziwa.
Amesema mkutano huo
pia utaainisha mambo ambayo tayari yalishafanyiwa tafiti kwa ajili ya
utekelezaji wa mipango hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia
Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na
maafisa kutoka NMB na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni