Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kufanya ufuatiliaji wa
karibu kuhakikisha mikakati ambayo serikali imekubaliana na Taasisi ya Bill and
Melinda Gates katika sekta ya mifugo inatekelezwa kama walivyokubaliana.
Naibu Waziri Ulega
amesema hayo ofisni kwake jijini Dodoma alipotembelewa na ujumbe kutoka Taasisi
ya Bill and Melinda Gates katika ofisi za wizara hiyo na kubainisha kuwa
serikali inahakikikisha Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Mifugo Tanzania
unatekelezwa na kuishukuru taasisi hiyo kwa kutoa mchango mkubwa katika mpango
huo.
“Sisi tuko pamoja na
nyinyi na tunathamini makubaliano yetu na hatuwezi kuvunja makubaliano yetu ninawahakikishia
kuwa nitamuagiza katibu mkuu afanye ufuatiliaji wa karibu sana kuhakikisha
kwamba sisi tuna mikakati yetu tunayoifanya lakini hii mikakati yote
inaenda sambamba na kile tulichokubaliana.” Alisema Mhe. Ulega
Naibu Waziri Ulega pia
amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya ufuatiliaji
wa karibu katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kulinda rasilimali za nchi kwa
kutumia Operesheni Nzagamba na Operesheni Sangara ili kuondoa mambo yaliyokuwa
yakifanywa bila utaratibu na kuisababishia serikali hasara.
“Tunafanya ulinzi wa
rasilimali na kuondoa ule uholela na kuhakikisha kuwa zile sheria, taratibu na
kanuni zinafuatwa sana kwa sababu hata masoko ya kimataifa yalitaka uholela
usiwepo, mambo yawe katika utaratibu wa kisheria na kanuni zinazoongoza sekta.” Alisema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega
amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inahakikisha katika operesheni hizo sheria,
kanuni na taratibu za sekta za mifugo na uvuvi zinafuatwa ili sekta hizo ziweze
kusonga mbele kwa kumuwekea mazingira mazuri mwananchi ili aweze kufaidika na
nchi iweze kuongeza pato la taifa.
Akizungumza katika
kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na wakuu wa idara kutoka Wizara ya Mifugo
na Uvuvi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabriel amebainisha baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kusimamiwa
ikiwemo elimu ili wafugaji waweze kunufaika kupitia sekta hiyo.
“Ningependa katika
ushirikiano wetu huu tuzidi kushirikiana katika kutoa elimu kwa wafugaji wetu
tuwe na ufugaji wenye tija, lakini eneo lingine la pili ni usimamizi dhidi ya
magonjwa, la tatu ni kuwawezesha wafugaji wetu kiuchumi lakini la nne ni
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Mifugo Tanzania.” Alisema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel pia
ameainisha mambo mengine kuwa ni umuhimu wa kufanyika kwa tafiti, usimamizi na
uhakikishaji wa uzalishaji bora wa mifugo ili sekta ya mifugo iweze kuwa na
maendeleo endelevu.
Akizungumza kwa niaba
ya Afisa Programu Mwandamizi wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates katika Ukanda
wa Afrika ya Mashariki Bibi Mercy Karanja, Mshauri Mwelekezi kutoka taasisi
hiyo nchini Tanzania Prof. Marcellina Chijoriga amesema Taasisi ya Bill and
Melinda Gates bado itaendelea kufanya kazi nchini kwa kufuata mpango wa
serikali.
Aidha Prof. Chijoriga
ameshukuru uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao umekuwa ukitoa
ushirikiano mkubwa kwa taasisi hiyo na kutoa ombi kwa uongozi wa wizara
kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Bill and Melinda Gates ili iweze kuleta
matokeo chanya kwa wafugaji nchini.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa
kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka Taasisi ya Bill and Melinda, Mercy
Karanja (kulia) na Mshauri Mwelekezi wa taasisi hiyo Prof. Marcellina Chijoriga
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni