Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka
wananchi hususan wafugaji kutotumia matamko ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli vibaya kwa kutafuta mianya ya kutolipa kodi.
Prof. Gabriel
amebainisha hayo akiwa katika mnada wa upili wa Meserani uliopo wilaya ya
Monduli Mkoani Arusha mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa
watumishi waliopo katika mnada huo na kusikiliza kero za wafugaji.
Akizungumza na
wananchi mara baada ya kufanya ziara hiyo Prof. Gabriel amesema Wizara ya
Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha mwezi mmoja itashirikiana na uongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kutoa tafsiri sahihi ya mfanyabiashara mdogo
anayestahili kukatiwa kitambulisho cha biashara ndogo ndogo (machinga) cha
Shilingi Elfu Ishirini kwa mwaka, kilichotolewa na Rais Magufuli kutokana
baadhi ya wafugaji kutaka kufahamu endapo wanastahili kupatiwa vitambulisho.
“Mheshimiwa rais
alikuwa amelenga hasa wale wafanyabiashara wadogo wadogo na tunachoamini
tutaendelea kulifanyia kazi lakini suala la machinga kwamba naye mfanyabiashara
wa ng’ombe kuhusishwa katika sifa za mfanyabiashara ndogondogo bado ni gumu
kulitolea majibu, lakini ushauri tusitumie matamko ya rais vibaya tusitafute
kichaka cha kujificha kwamba nawe ni machinga, wewe mwenyewe fikiria na jitafakari
tulipe kodi na tujenge nchi yetu.” Alisema Prof. Gabriel
Akizungumza na
wafugaji hao Prof. Gabriel amepokea kilio cha wafugaji kuwa wamekuwa wakiuza
ng’ombe kwa makadirio au matakwa ya mnunuzi kutokana na kutokuwepo kwa mizani
ili waweze kuuza ng’ombe kwa kilo badala ya bei ya kukadiria kati ya mfugaji na
mnunuzi wa ng’ombe, kitendo ambacho wafugaji hao wamesema kimekuwa kikiwafanya
wasiuze mifugo yao kwa bei yenye tija kwao.
“Lengo letu ni
kuhakikisha minada yote hasa ya upili na ile ya mipakani inatumia mizani, mnada
wa Kimesera mzani wake uko tayari unatakiwa kufanyiwa marekebisho ili
kuondokana na bei ya kukisia katika kipindi cha mwezi mmoja.” Alisema Prof.
Gabriel
Aidha katibu mkuu
huyo, amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuhakikisha wanawapatia ng’ombe
malisho bora ili wapate mazao bora ya mifugo yao huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi
ikihakikisha inaendelea kuimarisha matibabu ili mifugo iwe na afya bora.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema pia
licha ya uwepo wa masoko ya mifugo hususan ng’ombe hapa nchini, wizara
inajikita katika kutafuta masoko ya mifugo nje ya nchi.
“Tunachoangalia hivi
sasa ni kuangalia na masoko ya nje ya nchi lakini hauwezi kuuza ng’ombe nje ya
nchi ambaye hana afya bora na tunaamini tukiendelea hivi hata mchango wetu wa
wizara kwenye uchumi wa viwanda utakuwa ni mzuri.” Alisema Prof. Gabriel
Naye Bw. Kandidi
Mlinyi ambaye ni msimamizi wa mnada wa Meserani amesema kuwa wamekuwa
wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika ukanda wa Wilaya ya
Monduli hivyo kuwa na mazingira magumu ya upatikanaji wa huduma hiyo mnadani.
Kauli hiyo imeungwa
mkono na baadhi ya wafugaji ambao wamesema ng’ombe wanaposafirishwa kutoka
maeneo mbalimbali kuja katika mnada huo, kwa wastani wanakunywa maji lita 20
hadi 60 lakini kutokana na ukosefu wa maji ng’ombe wanakuwa katika mazingira
magumu hali inayosababisha ng’ombe hao kuchoka kwa kuwa wanapoteza maji mengi
mwilini.
Katika ziara hiyo ya
Katibu Mkuu Prof. Gabriel wafugaji wamepongeza utendaji kazi wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kwa kuwa viongozi na watendaji wa wizara wamekuwa wakifika mara
kwa mara kwa wananchi wakiwemo wafugaji ili kutatua kero zao.
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka katika uongozi wa mnada wa Meserani kwa siku zaidi ya ng’ombe 500 huuzwa
na kusafirishwa kwenda katika mikoa mbalimbali wakati wa msimu ambao unakuwa na
ng’ombe wengi kuanzia mwezi Machi hadi Julai kila mwaka.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante
Ole Gariel akikagua ubora wa baadhi ya ng'ombe waliofikishwa katika mnada wa
Meserani
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni