MIGOGORO MIKUBWA 14 KATI YA 29 YATATULIWA NA
WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara kupitia timu yake maalum ya
kushughulikia migogoro, hadi sasa imetatua migogoro mikubwa 14 kati ya 29
inayohusisha wakulima na wafugaji pamoja na hifadhi na wawekezaji.
Naibu Waziri Ulega
amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani
Kilimanjaro Bw. Lengai Ole Sabaya pamoja na viongozi wengine wa wilaya hiyo,
mara baada ya kuarifiwa kuwepo kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji katika
Wilaya ya Hai na kubainisha kuwa ni hatari kwa jamii inayoishi pamoja kuwa na
mgogoro wa aina hiyo.
“Nitamsisitiza katibu
mkuu mifugo aliangalie kwa karibu sana hili kwa sababu ni hatari sana kwa jamii
inayoishi pamoja kutokuwa na maelewano ya kuachiana maeneo kwa ajili ya
shughuli zao za kiuchumi.” Alisema Mhe. Ulega
Mhe. Ulega ametoa
kauli hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya kumuarifu kuwa
baadhi ya maeneo yenye migogoro ni Kata ya KIA ambapo wafugaji wamekuwa
wakiingiza mifugo yao katika maeneo ya uwanja wa ndege wa KIA, pamoja na wakulima
wilayani humo kutotaka kuwaachia wafugaji maeneo wasiyoyatumia kwa kilimo
hususan yenye magadi kwa ajili ya malisho kwa wafugaji hivyo kutengeneza chuki
dhidi yao.
Naibu Waziri Ulega
amemshauri pia mkuu huyo wa wilaya kutumia Chuo cha Mifugo Tengeru na Kituo cha
Uhimilishaji cha Taifa (NAIC) vilivyopo Mkoani Arusha ili kuleta mabadiliko kwa
wafugaji katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro kwa kuwa na ng’ombe wachache
na wenye tija ukizingatia ukanda huo kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh
ambacho kinahitaji maziwa kwa wingi katika uzalishaji wao.
“Ukanda huu kuna
kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinahitaji lita laki moja ya maziwa
kwa siku na bado hayatoshelezi hadi inawalazimu kuchukua maziwa kutoka mikoa ya
Iringa na Njombe ni vyema mkashirikiana na wizara kutoa elimu ili wafugaji wa
wilaya hii wabadilike kwa kufuga kisasa hususan ng’ombe wa maziwa badala ya
kuwa na ng’ombe wengi wasio na tija kiuchumi.” Alisema Mhe. Ulega
Naibu Waziri Ulega
amemshauri pia mkuu wa wilaya Bw. Sabaya kuwa na kampeni maalum ya kutoa elimu
kwa wafugaji pamoja na kushirikiana na wataalam ili wilaya hiyo iwe ya mfano
katika kubadilisha fikra za wafugaji.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya amesema changamoto kubwa zilizopo wilayani
hapo ni mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ambao tayari upo katika hatua
mbalimbali za kutatuliwa pamoja na wafugaji kutokuwa tayari kubadilika kutoka
kwenye ufugaji wa zamani wa kuwa na makundi makubwa ya mifugo isiyo na tija.
Kufuatia mazungumzo
baina yake na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ulega, mkuu huyo wa wilaya
amesema atazidi kushirikiana na wizara hiyo ili kuhakikisha changamoto hizo
zinatatulika na kuifanya wilaya hiyo kuzidi kunufaika na mifugo iliyopo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akifafanua
jambo kwa viongozi wa Wilaya ya Hai (hawapo pichani) namna ya kuiboresha sekta
ya mifugo wilayani humo
Baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Hai, wakiongozwa na Mkuu wa
Wilaya ya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya wakiwasilisha hoja mbalimbali kwa Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni