Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) amehudhuria Mkutano
Mkuu wa 23 wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) Kamisheni ya Afrika,
uliofanyika Mjini Hammament nchini Tunisia.
Mkutano
huo uliojumuisha nchi zaidi ya 25 za bara la Afrika zikiwemo Zambia, Zimbabwe,
Misri, Kenya, Uganda, Tunisia na Chad ulikuwa na malengo ya kuangalia afya ya
wanyama, haki za wanyama, uzalishaji wa mifugo na usalama wa chakula
kitokanacho na mifugo na kutoa mapendekezo kulingana na kanuni za shirika hilo
duniani.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) akiambatana na
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa wizara hiyo Dkt. Hezron Nonga amepata fursa
ya kufanya kikao cha ana kwa ana na uongozi mkuu wa Shirika hilo la Afya ya
Wanyama Duniani (OIE) kwa kuzungumza na rais wa shirika hilo Dkt. Mark Schipp,
Mkurugenzi Mkuu Dkt. Monique Eloit na mwakilishi wa shirika hilo kwa Ukanda wa
Nchi za Kusini mwa Afrika Dkt. Samuel Wakusama.
Katika
mazungumzo hayo, Mhe. Ulega ameshukuru uongozi huo kwa ushirikiano wake na
Tanzania kwa kuendelea kuisaidia nchi katika miradi mbalimbali ya kulinda afya
za wanyama hapa nchini.
Aidha
ameelezea nafasi ya Tanzania katika rasilimali za asili ikiwemo mifugo na uvuvi
ambapo kwa upande wa mifugo ametoa takwimu za mifugo iliyopo nchini pamoja na
vikwazo ambavyo sekta ya mifugo inakabiliana navyo yakiwemo magonjwa, kasi
ndogo ya mifugo kuzaliana (Poor Breeding) na uzalishaji duni (Low Productivity)
hali ambayo inasababisha nchi kushindwa kusafirisha mifugo na mazao yatokanayo
na mifugo kama vile nyama kwenda katika masoko ya nje ya nchi.
Mhe.
Naibu Waziri Ulega ameliomba Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kuisaidia
nchi ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto hizo ili kukuza uchumi na
kipato cha wadau wa sekta ya mifugo ambapo kwa pamoja uongozi huo umeahidi
kuzifanyia kazi.
Licha
ya mazungumzo hayo, Mhe. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Hamis Ulega
(MB) kupitia kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Dkt. Hezron Nonga, amewakabidhi
andiko linalofafanua kwa kina sekta ya uvuvi nchini, changamoto zake na maeneo
yenye uhitaji ili kuuwezesha uongozi huo kuendelea katika hatua ya utekelezaji.
Pamoja
na mambo mengine, Mheshimiwa Naibu Waziri Ulega ameueleza uongozi wa OIE kuhusu
nia ya Tanzania kuandaa mkutano ujao kwa kuwa ni nchi yenye mifugo na
wanyamapori wengi, mazingira mazuri ya uwezekaji na taasisi maalum
zinazoshughulikia masuala ya viwango, ubora wa bidhaa na usalama wa chakula.
Katika
kutathmini afya za wanyama, wataalamu wamejadili magonjwa mbalimbali ya wanyama
yaliyopo katika bara la Afrika hususan kwa nchi wanachama, athari na namna
yakuyakabili yakiwemo magonjwa ya miguu na midomo (FMD), Kichaa cha mbwa na
homa ya Bonde la Ufa (RVF).
Aidha
kikao kimetathmini kwa pamoja miradi mbalimbali yenye lengo la kuimarisha afya
za wanyama pamoja na michango ya wahisani ikiwemo Benki ya Dunia, Mchango wa
Wataalam wa Kati wa Mifugo (Veterinary Paraprofessionals) na nafasi yao katika
kuimarisha huduma za afya ya wanyama katika Bara la Afrika.
Kikao cha ana kwa ana kati ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) (wa pili kutoka kulia) na Uongozi wa Shirika la
Afya ya Wanyama Duniani (OIE). Kutoka kushoto: Mwakilishi wa OIE Kanda ya
Kusini mwa Afrika Dkt. Samuel Wakusama, Rais wa OIE na Kamisheni ya Australia
Dkt. Mark Schipp na Mkurugenzi Mkuu wa OIE Dkt. Monique Eloit na Mkurugezi wa
Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (wa kwanza kulia) Dkt. Hezron
Nonga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni