Nav bar

Alhamisi, 27 Januari 2022

WAFUGAJI MKURANGA WAWEZESHWA MADUME YA NG'OMBE AINA YA BORANI*

Wafugaji Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani wawezeshwa na Serikali madume matatu ya ng'ombe aina ya borani ikiwa ni pamoja na  kuwakwamua wafugaji hao kiuchumi.

Wakati akikabidhi madume hayo Januari 27. 2022, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alisema madume hayo matatu ya ng`ombe aina ya borani yatakwenda kuboresha koosafu za ng`ombe wa asili kwa wafugaji watakao yatumia.

"ugawaji wa madume haya bora ya ng'ombe ni  kwa lengo la kuboresha kosaafu za Mifugo Ili  waelekee kwenye ufugaji wa kisasa na hii inaenda sambamba na  utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM (2020 – 2025) inayolenga kuwakwamua kiuchumi wafugaji nchini.

Naye Mkurugenzi wa ranch ya Mbogo, Chalinze Mkoani Pwani, Naweed Mulla ambaye wameshirikiana na Serikali kugawa madume hayo  alisema thamani ya madume ni shilingi milioni 15.

“Uzalishaji wa Ng’ombe hawa aina ya borani utasaidia  kuboresha koosafu bora ambayo watakuwa bora kwenye uzalishaji wa mazao ya mifugo ikiwemo kiwango kikubwa cha maziwa, nyama nyingi, uhimilivu dhidi ya magonjwa na hali ya mazingira ya mikoa yetu” alisema Mulla

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri pia aligawa majokofu 8 kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Uvuvi Ili kusaidia kupunguza upotevu  wa ubora wa   mazao hayo na kuongeza thamani.

Mratibu wa miradi ya Pwani ya bahari ya Hindi nchini kwa miradi inayotekelezwa na Shirika linalojishughulisha na mazingira  (WWF), Dkt. Modesta Medadi alisema wamekabidhi majokofu 8 kwenye Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani,  ikiwa ni mkakati wa kuwezesha shughuli zao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir Ally alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada yake ya kusaidia na kuwaendeleza wafugaji na wajasiriamali wa bidhaa za uvuvi nchini sawa na ahadi yake katika hotuba zake.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, akilishukuru Shirika linalojihusisha na mazingira (WWF) kwa kuwawezesha kupata majokofu nane (8) kwenye Wilaya ya Mkuranga na kuwasihi wanawake wajasiriamali waliokabidhiwa majokofu hayo wayatunze na wayatumie kama ilivyokusudiwa. Januari 27.2022 

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiongea na wafugaji pamoja na vikundi vya wanawake wa Mkuranga wakati wa hafla fupi wa ugawaji wa madume bora aina ya borani na majokofu Januari 27, 2022.

 

 


Jumatano, 26 Januari 2022

UCHUMI WA BULUU KUWANUFAISHA WANANCHI - MHE. ULEGA


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kupitia kampeni ya uchumi wa buluu wanakwenda kuimarisha hali za kiuchumi za mwananchi mmoja mmoja hususan wanaoishi katika mikoa ya Pwani ya bahari ya Hindi na Taifa kwa ujumla.

Hayo aliyasema wakati wa ziara yake ya kutembelea vikundi vinavyojihusisha na shughuli za kilimo cha mwani, na unenepeshaji kaa katika Wilaya za Pangani, Tanga jiji na  Mkinga, Mkoani Tanga Januari 25, 2025.

Alisema kuwa kupitia kampeni hiyo Serikali inakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya namna ya rasilimali za bahari zitakavyotumika kuweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi ambao wanategemea bahari kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.

"Serikali ya Mama Samia inakwenda kuondoa hali duni za wavuvi kwa kuwaunganisha na fursa za kiuchumi zilizopo kwenye ukanda wa bahari ya hindi kwa kushiriki kwenye  fursa zilizopo badala ya kutegemea uvuvi  pekee" alisema Mhe. Ulega.

Aidha alisema wanataka watanzania kuhamasika na kuchangamkia fursa za kilimo cha mwani, kunenepesha kaa, kamba kochi kwani soko la uhakika lipo na Serikali ipo tayari kuwawezesha kwa mitaji sambamba na vifaa.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Pangani Ghaibu Lingo alisema kuwa tayari wameshaanza kunufaika na fursa za uchumi wa buluu kwa wananchi kuweza kushiriki kwenye shughuli ya kunenepesha kaa na kufunga miamba kwa ajili ya Uvuvi wa pweza na kisha kuwauza kwa faida kubwa tofauti na hapo awali.

"Tumeanza hii mbinu ya kufunga miamba kwa ajili ya Uvuvi wa pweza katika eneo la Ushongo na matokeo tumeweza kuyaona hivyo tunaiomba Serikali kuweza kuwasaidia wavuvi wa maeneo mengine kama Kipumbwi na Mkwaja" alisema DC huyo.

Nao wananchi waliipongeza Serikali kwa kuja na fursa ya uchumi wa buluu kwani unakwenda kusaidia kubadilisha uvuvi wao wa mazoea na kuwa wa kisasa na wenye tija.

Hamis Ramadhani Mwenyekiti wa kikundi cha Jifute aliiomba serikali kuwawezesha mitaji pamoja na mashine kubwa ya kuvutia maji ili waweze kukuza mitaji yao na hivyo kupata faida kubwa.

Nae Burhan Ramadhani alisema kuwa uvuvi haramu pamoja na ukosefu wa soko imekuwa ni kikwazo kwa kilimo cha mwani kuweza kufanya vizuri katika maeneo yao hivyo aliiomba wizara kuona namna ya kuwawezesha vifaa na mitaji.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akieleza umuhimu na faida ya mwani kwa wanakijiji wa mwandosi wakati wa ziara yake Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, Januari 25, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akimtambulisha mwakilishi kutoka Benki ya kilimo (TADB), Bw. Furaha Sichula kwa wananchi wa Tanga kueleza namna wanaweza kunufaika na mikopo kutoka Benki hiyo ya kilimo wakati wa ziara yake Mkoani humo Januari 25, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akieleza fursa zinazopatikana kutokana na unenepeshaji kaa wakati wa ziara yake Wilaya ya pangani Mkoani Tanga alipotembelea kikundi cha Jifute kinachojishughulisha na unenepeshaji huo na kukabidhi kikundi hicho kwa  Benki ya kilimo (TADB) Ili iweze kutoa mikopo itakayowasaidia  kujiendeleza na kujipatia kipato. Januari 25, 2022.

Muonekano wa mabwawa ya kienyeji ya unenepeshaji kaa yaliyotengenezwa na akina mama na  vijana kikundi cha jifute, pangani Mkoani Tanga, januari 25, 2022.


Jumanne, 25 Januari 2022

ULEGA AELEZA FURSA ZINAZOPATIKANA KWENYE UCHUMI WA BULUU.


Serikali ya awamu ya Sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi (AFDP) imetenga takribani sh Bil 29 mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kuwezesha kiuchumi shughuli za uvuvi na mikopo kwa wananchi waliopo kwenye sekta hiyo pamoja na kukuza pato la Taifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa mifugo na uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega Januari 24, 2022 wakati wa ufunguzi wa kikao  kazi cha mkakati na kampeni ya  kuhamasisha shughuli za ukuzaji viumbe maji bahari kwa viongozi na  wataalam katika Mamlaka za Serikali za mitaa mkoani Tanga.

Alisema kuwa sehemu ya fedha hizo takribani sh Bil. 2.1 zinakwenda kukopeshwa kwa vikundi vya wafugaji wa samaki, wakulima wa mwani,wafugaji wa majongoo bahari,  wanenepeshaji wa kamba koche na  kaa, katika ukanda wa bahari ya Hindi.

 "Tumekutana sisi wataalamu kwa ajili ya kupeana mbinu na mikakati ya kuweza kuwafikia wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa Mradi huo ili kuona namna ambavyo tutawainua kiuchumi kupitia fursa zilizoko baharini" alisema Naibu Waziri Ulega.

Alisema kuwa kuna utajiri mkubwa kupitia fursa ya rasilimali zinazopatikana katika ukanda huu hivyo Serikali imedhamiria kuinua hali duni za wananchi waishio katika ukanda huo hivyo wataalam hao wanaweza kusaidia kuwaonyesha wananchi fursa zilizopo.

Aliongeza kuwa Benki ya kilimo kwa kushirikiana na mabenki mengine ya biashara yaweke mazingira rafiki ya kutoa mikopo  kwa vyama vya ushirika vya  vijana na wanawake Ili waweze kufanya shughuli za kunenepesha kaa, kamba koche , ufugaji wa samaki,  majongoo bahari,  na kilimo cha  mwani.

Utolewaji wa mikopo hii pia iwaguse wavuvi wadogowadogo, mmojammoja au katika vikundi kwani kwa kufanya hivyo kilio chao cha kutumia fursa hizi za bahari kitakuwa kimesikika.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa alisema kuwa Changamoto kubwa iliyopo kwa wavuvi  wa ukanda huo ni ukosefu wa viwanda pamoja na masoko ya uhakika wa mazao ya bahari.

Alisema kuwa kampeni hiyo itaweza kuleta chachu na maendeleo ya wananchi kwani wataweza kupata fursa nyingine ya kiuchumi katika maeneo yao kupitia kilimo cha mwani pamoja na unenepeshaji wa viumbe bahari.

Aidha mwakilishi kutoka Benki ya kilimo (TADB), Bw. Furaha Sichula amesema kwa mwaka 2021/2022 jumla ya TSH. 4.827bil zimekopeshwa kwenye Sekta ya Uvuvi ikilinganishwa na mwaka  2020/2021 ambapo kiasi cha Tsh. Bil 1.625 kilikopeshwa.

Nae Mkurugenzi wa ukuzaji viumbe maji kutoka wizara ya mifugo na uvuvi, Dkt Nazael Madalla alisema kuwa katika mwaka uliopita uzalishaji wa viumbe vya bahari ulikuwa ni asilimia 11% pekee.

Kampeni hiyo iliyoanzishwa na Serikali inakwenda kuwasaidia wananchi  kujikwamua kiuchumi kupitia fursa za bahari.

Kikao kazi hicho kimeazimia kila baada ya miezi mitatu Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega atapita kukagua utekelezaji wa mikakati iliyoandaliwa.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiongea na viongozi pamoja na  wataalam kutoka mamlaka ya Serikali za mitaa wa  Mkoa wa Tanga (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha mkakati na kampeni na kuhamasisha shughuli za ukuzaji viumbe maji bahari. Januari 24, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Serikali mara baada ya kikao kifupi  juu ya fursa za uchumi wa buluu Mkoani Tanga. Januari 24.2022


 

Ijumaa, 21 Januari 2022

WAZIRI NDAKI ATOA MAELEKEZO KWA WAKUSANYA MADUHULI YA SERIKALI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ametoa maelekezo manne kwa wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwa lengo la kuhakikisha wanafikia lengo lililowekwa.

 

Waziri Ndaki ametoa maelekezo hayo leo (20.01.2022) kwenye kikao na wataalam hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Royal Village ambapo aliwaeleza kuwa mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli ya serikali sio mzuri kwani kati ya bilioni 50 zilizokusudiwa kukusanywa ni bilioni 13.9 ndio zimekusanywa.

 

Katika kikao hicho taarifa za ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ziliwasilishwa kwa kila kituo ambapo pia changamoto ziliwasilishwa na kujadiliwa namna gani ya kuweza kukabiliana nazo ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhili unafikia malengo yaliyowekwa

 

Akizungumza na wataalam hao Waziri Ndaki amesema kuwa wizara iliamua kuunda timu ya ufuatiliaji kwa lengo la kuangalia hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye minada na vituo vilivyo chini ya wizara. Timu hiyo ilibaini changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo ambayo yatasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato.

 

Baada ya majadiliano ya taarifa zilizokuwa zimewasilishwa, Waziri Ndaki aliwaeleza wataalamu hao kuwa ni lazima wajipange vizuri kuhakikisha wanafikia malengo ya ukusanyaji maduhuli ya serikali kama walivyo pangiwa.

 

"Viongozi tutaendelea kuwafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha malengo ya ukusanyaji maduhuli ya serikali yanatimizwa na kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu kwa makusudi hatua zitachukuliwa dhidi yake," alisema Waziri NDAKI

 

Pia amemueleza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda kuwasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuhakikisha Halmashauri zilizotumia fedha za makusanyo ya maduhuli za wizara zikiweno za Halmashauri Mvomero, Tarime na Manyoni zinarejesha fedha hizo.

 

Lakini pia wataalam wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanatimizwa. Waziri Ndaki amewaeleza wataalam hao kuwa katika muda wao wa utumishi ndani ya sekta ya mifugo ni lazima waache alama ikiwemo ya ukusanyaji mzuri wa maduhuli. Wataalam hao wametakiwa kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni, miongozo na taatibu zilizowekwa.

 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda amewataka wataalam hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu lakini pia watalazimika kuwajibika kutokana na matendo yao kwenye suala la ukusanyaji wa mapato. Vilevile amewataka kuhakikisha wanakusanya mapato katika maeneo yao na kucha tabia ya udanganyifu kwani hatua zitachukuliwa dhidi yao. Adiha, amewataka wataalam hao kuwasilisha taarifa za makusanyo kila mwezi.

 

Pia amemshukuru Waziri kwa uamuzi wake wa kuitisha kikao hicho kwani kimesaidia kwa kuwawezesha wataalam wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli Tanzania Bara kukaa kwa pamoja kujadili changamoto walizonazo na kutoka na mkakati wa pamoja ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhuli unakwenda vizuri.

 

Mkuu wa Mnada wa Ipuli mkoani Tabora, Fred Senyagwa amesema kuwa watakwenda kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kuhakikisha wanakusanya maduhuli kulingana na malengo yaliyowekwa.

 

Kaimu Mkuu wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo - Iringa, Bw. Rajon Deule amesema kuwa sababu ya kituo chao kufanya vizuri ni kwamba Kanda yao wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara ambavyo huwa wanajadili changamoto wanazokutana nazo na kujiwekea mikakati ya namna ya kukabiliana nazo. Kwa kutumia njia hiyo imewasaidia kuweza kukusanya maduhuli ya serikali vizuri.

 

Kikao hicho cha wataalam kimefanyika kwa lengo la kuwakutanisha wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili waweze kujadili changamoto na mikakati itakayowezesha sekta ya mifugo kutimiza malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika kikao cha wataalam wa Sekta ya Mifugo kilichojadili hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo amawataka wataalam hao kukusanya fedha ili kufikia malengo yaliyowekwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 ya kukusanya bilioni 50. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma. (20.01.2022)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akizungumza wakati wa kikao cha wataalam wa sekta ya mifugo kilichojadili kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Bw. Nzunda amewataka wataalam hao kuwasilisha taarifa za makusanyo ya maduhuli kila mwezi. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma. (20.01.2022)

Mhasibu Mkuu wa Sekta ya Mifugo, Bi. Veronica Kishala (kulia) akiwasilisha mada kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye sekta ya mifugo kwenye kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wataalam wa sekta hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma. (20.01.2022)


Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akitoa ufafanuzi wakati wa kikao cha Waziri na Wataalam wa Mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kilichofanyika kwenye ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma. (20.01.2022)


Baadhi ya Viongozi na Wataalam wa Sekta ya Mifugo wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu ukusanyaji wa maduhuli kwenye sekta hiyo wakati wa kikao cha Waziri wa Mifugo nna Uvuvi na Wataalam wa Mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kilichofanyika kwenye ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma. (20.01.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) na Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda (kushoto) wakifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa kikao cha wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji maduhuli ya serikali kilichofanyika kwenye ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma. (20.01.2022)



WATAALAM SEKTA YA UVUVI WATAKIWA KUTIMIZA LENGO LA UKUSANYAJI MADUHULI YA SERIKALI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wataalam wa sekta ya Uvuvi kuhakikisha wanakusanya maduhuli ya serikali ili kutimiza lengo la kukusanya bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (15.01.2022) kwenye kikao cha wataalam wa sekta ya uvuvi kilichojadili hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia sekta ya uvuvi ambapo mpaka sasa sekta hiyo imekusanya bilioni 10 kati ya bilioni 40 zilizolengwa.  

 

Katika kikao hicho taarifa za ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ziliwasilishwa kwa kila kituo ambapo pia changamoto ziliwasilishwa na kujadiliwa namna gani ya kuweza kukabiliana nazo ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhili unafikia malengo yaliyowekwa.

 

Akizungumza na wataalam hao Waziri Ndaki amesema kuwa ni lazima wataalam kuhakikisha wanaongeza usimamizi kwenye maeneo yao ili malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yatimie. Ili kuhakikisha malengo ya ukusanyaji maduhuli yanafikiwa Waziri Ndaki amesema vituo vitatakiwa kutoa taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli kila wiki ili kama kunakuwepo na changamoto iweze kutatuliwa kwa wakati.

 

Lakini pia wataalam wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanatimizwa. Waziri Ndaki amewaeleza wataalam hao kuwa katika muda wao wa utumishi ndani ya sekta ya uvuvi ni lazima waache alama ikiwemo ya ukusanyaji mzuri wa maduhuli.

 

Wataalam hao wametakiwa kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni, miongozo na taatibu zilizowekwa. Pia wametakiwa kuhakikisha kuwa wanalinda na kuzisimamia rasilimali za uvuvi. Vilevile amewaonya wataalam hao kutojihusisha na uvuvi haramu kwani wakibainika hatua zitachukuliwa dhidi yao.

 

Waziri Ndaki amesema kuwa wizara ina malengo makubwa ya kuwawezesha wavuvi ili wakue kimapato na hivyo waweze kuchangia kwenye pato la taifa kupitia sekta ya uvuvi. Aidha, amesema kuwa wizara itafanya mapitio ya tozo mbalimbali za uvuvi na kuzifanyia marekebisho endapo yatahitajika.

 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi amesema kuwa lengo la kuitisha kikao hicho ni kufanya tathmini ya hatua iliyofikiwa katika ukusanyaji maduhuli ya serikali pamoja na hali ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi.

 

Pia amemshukuru Waziri kwa uamuzi wake wa kuitisha kikao hicho kwani kimesaidia kwa kuwawezesha wakuu wa vituo vyote Tanzania kukaa kwa pamoja kujadili changamoto walizonazo na kutoka na mkakati wa pamoja ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhuli unakwenda vizuri.

 

Getrude Migodela kutoka Kitengo cha Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Mwanza amesema kuwa watakwenda kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kuhakikisha wanakusanya maduhuli kulingana na malengo yaliyowekwa. Pia ameishikuru Wizara kwa maelekezo yake ya kuwataka wafanyabiashara wa samaki na mazao ya uvuvi waanze kulipia kwenye eneo mzigo unapotoka kwa kuwa hiyo itawasaidia kuongeza mapato kwenye vituo vyao.

 

Kikao hicho cha wataalam kimefanyika kwa lengo la kuwakutanisha wataalam wa uvuvi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili waweze kujadili changamoto na mikakati itakayowezesha sekta ya uvuvi kutimiza malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali lakini pia kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika kikao cha wataalam wa Sekta ya Uvuvi kilichojadili hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo amewaeleza wataalam hao kuwa katika kipindi kilichobaki cha mwaka wa fedha 2021/2022 ni lazima lengo la kukusanya bilioni 40 litimizwe. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma. (15.01.2022)

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi akizungumza wakati wa kikao cha wataalam wa sekta ya uvuvi kilichojadili kuhusu ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Kulia kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma. (15.01.2022)

Mhasibu Mkuu wa Sekta ya Uvuvi, Bw. Lupakisyo Mwakitalima (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye sekta ya uvuvi kwenye kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wataalam wa sekta hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma. (15.01.2022)

Baadhi ya Viongozi na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu ukusanyaji wa maduhuli kwenye sekta hiyo. (15.01.2022)

Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na baadhi ya Viongozi na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi walioshiriki kikao cha kujadili kuhusu hali ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma. (15.01.2022)

Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi waliofanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo wote wamekusanya zaidi ya asilimia 50 ya lengo walilopangiwa. Kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala. (15.01.2022)





Jumamosi, 15 Januari 2022

ULEGA: SERIKALI YAJA NA SULUHISHO KUKABILIANA NA UKAME, VIFO VYA MIFUGO NCHINI

Serikali imekuja na suluhisho katika kukabiliana na changamoto za ukame uliosababisha vifo vingi vya mifugo kwa kutumia Sh bilioni 130 ili kuchimba visima, kukarabati na kujenga mabwawa ikianza na maeneo yaliyoathirika zaidi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega alieleza mkakati huo wa Serikali Januari 14,2022 wakati alipofanya ziara Wilaya ya Kiteto,Mkoani Manyara ili kuwapa pole kwa kufiwa na ng'ombe 1,874 kati ya Septemba 2020 hadi Januari mwaka huu.

"Serikali ya Mama Samia ni sikivu na inawajali wananchi wake, imenituma kuja kuwapa pole kwa kufiwa na ng'ombe wengi waliokufa kutokana na ukame kutokana na kukosa maji na malisho" alisema.

Aidha Mhe. Ulega baada ya kushuhudia mizoga ya ng'ombe katika kijiji cha Makame kata ya Makame akiwa katika mikutano ya hadhara kwenye kijiji cha Makame na Ndede alisema, Serikali inawapa Pole lakini imekuja na suluhisho la kukabiliana na ukame huo kwa kuchimba visima na mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo.

Katika kuhakikisha wafugaji wanaondokana na vifo vingi vya mifugo na wanakabiliana na uhaba wa mifugo, Serikali itasambaza nyasi za malisho kwa  mifugo kwa ajili ya wafugaji kuzipanda, kuvuna na kuhifadhi ili kuzitumia wakati wa ukame na msimu kama huu.

Katika kukabiliana na ukame huo, pia aliwataka wafugaji Kiteto na Tanzania kwa ujumla, kuacha kufuga mifugo kwa mazoea, wanatakiwa kuanza kupunguza mifugo yao kwa kuuza ili kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kuboresha mifugo inayobaki na kuuza sokoni ikiwa bora.

Mhe.Ulega alisema, wafugaji wanatakiwa kuitikia wito wa Serikali wa kuweka hereni kwenye masikio ya ng'ombe kwa lengo la kuweka alama ili badae kuzikatia bima ili zikifa waweze kulipwa na pia wakopesheke na taasisi za kifedha kuliko ilivyo sasa.

Naye Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaite (CCM) alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Shilingi bilioni 130 kwa Wizara ya Maji kwa ajili ya kununua mtambo mmoja wa kuchimba visima, mabwawa na malambo katika mikoa yote nchini na akaomba mitambo ikifika mkoani kwake kutokana na sababu ya ukame apewe kipaumbele.

Mhe. Lekaite alisema kutokana na changamoto ya ukame Wilaya yake ambayo imeua mifugo mingi inaomba mtambo wa kuchimba mabawa ukifika mkoani basi Wilaya yake iwe ya kwanza kupewa.

Akizungumzia vifo vya mifugo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Afya kutoka Wizara ya Mifugona Uvuvi, Dk Vayan Laizer alisema vifo hivyo vinatokea sababu ya uhaba wa maji hivyo ng'ombe wanapokula majani mwituni na kukosa maji miili yao inakuwa na kinga kidogo na hivyo wanashindwa kujikinga na maradhi kutokana na sumu kubaki mwilini.

Naye Kaimu Mkurugenzi Sekta ya Afya Wilaya ya Kiteto, Dk Lunonu Sigalla wakati akitoa taarifa ya athari za ukame wilayani humo alisema kati ya Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu ngombe 1874 kutokana na ukame na waliobaki wamedhoofu sana kutokana na changamoto hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,Bw. Mbaraka Batenga alisema uboreshaji wa miundombinu ya mifugo unatakiwa kwa lengo la kufungamanisha na miradi ya ujenzi wa shule sikizi zaidi ya 47 zilizojengwa katika wilaya hiyo na hivyo kuzuia kuhama hama wafugaji hao.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiangalia mfugo aliyekufa kwa athari ya ukame kwenye kata ya Makame Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, akiambatana na Mbunge wa Kiteto Mhe. Edward Lekaita(wa kwanza kutoka kushoto),  Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bw. Mbarak Batenga, (wa pili kutoka kushoto), viongozi wa chama, wafugaji na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Januari 14,2022 

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiongea na watendaji wa Wilaya ya Kiteto mara baada ya kuwasili Wilayani humo kuona athari ya ukame kwa wafugaji, kukusanya mawazo ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo Januari 14, 2022. Kulia ni Mbuge wa Kiteto Bw. Edward Ole Lekaita na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bw. Mbarak Batenga. 


Alhamisi, 13 Januari 2022

WIZARA YAHIMIZA USHIRIKI WA WAZEE WA KIMILA KATIKA ZOEZI LA UTAMBUZI WA MIFUGO KIELEKTRONIKI

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Dkt. Annette Kitambi amewaomba Viongozi wa Vyama vya Wafugaji nchini kufikisha elimu ya utambizi wa mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki kwa wazee wa kimila ili kusaidia kufanikisha zoezi hilo bila vikwazo.

Dkt. Kitambi alitoa rai hiyo  wakati wa kufungua mafunzo ya siku moja ya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki jijini Dodoma Disemba 24,2021.

Alisema katika jamii za wafugaji hasa wamasai wazee wa kimila ndio wenye nguvu na kusikilizwa na vijana na watu wao wanaowaongoza hivyo endapo elimu hiyo itawafikia itasaidia wafugaji hao kutambua mifugo yao kirahisi.

"Chama cha Wafugaji tunawategemea sana kufikisha elimu kwa wafugaji lakini msiwasahau wale wazee maarufu na wazee wa mila kwa sababu akishaelewa akiwaambia watu wa jamii yake wanatekeleza kwa kuwa wanaheshimika", alisema

Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine Wizara ya Mifugo imeweka milango wazi kwa wafugaji kutoa maoni yao juu ya zoezi hilo la utambuzi kwa njia ya kielektroniki hasa wanapo baini kuwepo kwa mapungufu wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga  aliwatoa hofu wafugaji juu ya utekelezaji wa zoezi hilo kwa kuwa limelenga kuweka miundo mbinu bora ya ufugaji hasa swala la malisho.

Alisema changamoto ya malisho imekuwa ikiwasumbua wafugaji wengi na kujikuta wakihama sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu Serikali ilikuwa ikikwamishwa na takwimu zisizo sahihi ambazo zilikuwa zikitolewa awali kulinganisha na uhalisia wa mifugo iliyopo.

"Nataka niwahakikishie wafugaji mara baada ya zoezi hili changamoto ya malisho itaenda kutatuliwa kwa sababu Serikali itakuwa na takwimu sahihi ya mifugo kila sehemu ya nchi kwa hiyo hata migogoro isiyo ya lazima haitakuwepo" alisema

Naye Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Uchumi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Aziza Mumba  alisema kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kutakuwa kumesaidia nchi kuendana na matakwa  ya kidunia ya kutaka mazao yote ya mifugo yatokane na mifugo ambayo imesajiliwa kwa njia ya kielektroniki.


Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uhamasishaji wa zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki Mkoani Dodoma. Disemba 24,2021. 

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama Dkt. Annette Kitambi akieleza lengo na faida ya zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki kwa maafisa Mifugo na maafisa TEHAMA (hawapo pichani) wa Wilaya na Mkoa wa Dodoma, Disemba 24,2021 

 


Afisa kutoka Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  Neema Kelya  akionyesha namna ya kutumia Mfumo wa usajili kwa maafisa Mifugo na maafisa TEHAMA wa Wilaya na Mkoa wa Dodoma  wakati wa kikao cha uhamasishaji wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya kielektroniki , Disemba 24,2021 

WALIOVAMIA KARANTINI YA MIFUGO WATAKIWA KUONDOKA KWA HIYARI*

Na Mbaraka Kambona, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Wananchi wakiwemo Wafugaji waliovamia eneo la kuhifadhia na kuiangalia kwa muda Mifugo  inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kuondoka katika eneo hilo kwa hiyari huku akionya kuwa atakayekaidi Serikali itatumia nguvu kuwaondoa.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipotembelea eneo la Karantini ya Kwala iliyopo katika Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 23, 2021. 

Alisema kuwa eneo hilo lina maslahi mapana kitaifa na hivyo wananchi kuvamia na kufanya shughuli zao katika eneo hilo linafanya karantini hiyo kupoteza sifa ya kibiashara kimataifa.

"Hili eneo lina  maslahi ya kitaifa hivyo wananchi walioingia na kukaa huku bila utaratibu wowote tuwaambie waondoke kwa hiyari, wale tutakaowakuta wakati tutakapoanza kazi ya ujenzi wa Karantini ya kisasa basi tutatumia nguvu kuwaondoa", alisema Mhe. Ndaki

Aidha, alisema kuwa mwaka wa fedha ujao watatenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga Karantini hiyo ili iwe ya kisasa itakayokidhi matakwa ya biashara ya kimataifa ya kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi.

"Hatuwezi kwenda kimataifa bila ya  kuwa na kituo hiki, wenzetu wakija hapa ghafla na hali hii watatuambia msiuze Ng'ombe wala Nyama zenu kwa sababu hakuna mahali watakuwa wamehakikishiwa usalama wao", alifafanua

Awali, Mkuu wa Kituo hicho cha Kwala, Dkt. Othman Makusa alimueleza Waziri Ndaki kuwa kituo hicho kina miundombinu duni na kimevamiwa na Wananchi kutoka Vijiji vya jirani na wanafanya shughuli zao mbalimbali ikiwemo Kilimo, Makazi na Ufugaji jambo ambalo linasababisha kituo hicho kupoteza sifa za kimataifa za kuwa Karantini.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi watakwenda kuliainisha eneo hilo vizuri na kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi wataambiwa wahame na maeneo mengine yatabakishwa kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akipatiwa maelezo mafupi kuhusu Karantini ya Kwala na Mkuu wa Kituo cha Karantini hiyo, Dkt. Othman Makusa (kushoto) alipotembelea kuona na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya kujenga Karantini mpya lililopo Mkoani Pwani Disemba 23, 2021. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akikagua eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya kujenga Karantini mpya ya Kwala alipotembelea eneo hilo lililopo katika Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 23, 2021. Akiwa katika eneo hilo alisema kuwa wananchi wote waliovamia eneo hilo waondoke kwa hiyari vinginevyo shughuli za ujenzi zitakapoanza wataondolewa kwa nguvu. 

 


UZINDUZI WA MWONGOZO WA UPATIKANAJI, USIMAMIZI NA UENDELEZAJI WA MAENEO YA MALISHO.

Waziri ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho katika hafla fupi ya kuzindua mwongozo huo iliyofanyika Mkoani Pwani Disemba 22, 2021. Wakati akizindua Mwongozo huo, Mhe. Ndaki alisema mwongozo huo ukitekelezwa vizuri utatatua changamoto ya malisho na maji kwa mifugo na itasaidia kupunguza migogoro ya Wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akimkabidhi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) nakala ya mwongozo ili awagawie baadhi ya Wakuu wa Mikoa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho iliyofanyika Mkoani Pwani Disemba 22, 2021. 

 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Bw. Jeremiah Wambura nakala ya Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho katika hafla fupi ya kuzindua Mwongozo huo iliyofanyika Mkoani Pwani Disemba 22, 2021


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge nakala ya Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho katika hafla fupi ya kuzindua mwongozo huo iliyofanyika Mkoani Pwani Disemba 22, 2021. 

 

 

WATAKAOSHINDWA KUSAJILI MIFUGO KWA HIYARI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA.

Serikali imesema itawachukulia hatua wafugaji watakaoshindwa kusajili mifugo yao kwa njia ya utambuzi wa hereni za kielekroniki pindi zoezi hilo litakapofungwa agosti 2022.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama, Dkt. Annette Kitambi wakati wa utoaji mafunzo ya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki Disemba 21,2021 Mkoani Morogoro.

Alisema kwa sasa zoezi hilo linaendelea kwa utoaji elimu kwa wataalam na viongozi kutoka Serikali za mitaa ngazi ya mkoa na wilaya pamoja na wafugaji ambao kwa pamoja watahusika katika kutekeleza zoezi hilo linalotarajiwa kuanza mapema Januari mwakani.

"Sheria zipo lakini kwa sasa hivi tunafanya kwa kuwahamasisha na kuwaelimisha, zoezi hili litaenda mpaka agosti mwakani tutakuwa tumemaliza kwa hiyari ndipo sheria zitaanza kutumika na sheria imeweka wazi kwamba ikibainika haijatambulika utapigwa faini ya shilingi milioni 2 au kwenda jela miezi sita au vyote kwa pamoja" alisema

Akisoma hotuba kwa niaba ya mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Ezron Kilamhama akawataka wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki.

Alisema zoezi hilo linaloenda na utoaji elimu kwa watendaji wa serikali ngazi ya halmashauri ni vyema kwa wataalam kila mmoja akaelewa vizuri muongozo, sheria na kanuni ili aweze kwenda kutoa elimu kwa wafugaji na wataalam waliopo ngazi za chini.

"Niwaagize wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhakikisha elimu hii inayotolewa inawafikia wafugaji na kuhakikisha mifugo yote iliyoainishwa kwenye muongozo ambayo ni Ng'ombe, Punda, Mbuzi na kondoo inavalishwa hereni katika maeneo yenu" alisema.


Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Ezron Kilamhama akiongea na Wakuu wa Wilaya (DC), Wakurugenzi (DED), Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS), Wenyeviti wa Halmashauri, maafisa Mifugo na maafisa TEHAMA wa Mkoa wa Morogoro wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kuhamasisha zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya kielektroniki Mkoani humo na kuwaagiza kuakikisha elimu waliyopata inawafikia wafugaji na Mifugo yote iliyoainishwa inavalishwa hereni Disemba 21, 2021. 


Sehemu ya washiriki wa mkutano wa kuhamasisha zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki wakiwa kwenye mkutano huo Disemba 21, 2021 Mkoani Morogoro.