Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kupitia kampeni ya uchumi wa buluu
wanakwenda kuimarisha hali za kiuchumi za mwananchi mmoja mmoja hususan
wanaoishi katika mikoa ya Pwani ya bahari ya Hindi na Taifa kwa ujumla.
Hayo aliyasema wakati wa
ziara yake ya kutembelea vikundi vinavyojihusisha na shughuli za kilimo cha
mwani, na unenepeshaji kaa katika Wilaya za Pangani, Tanga jiji na Mkinga, Mkoani Tanga Januari 25, 2025.
Alisema kuwa kupitia
kampeni hiyo Serikali inakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya namna ya
rasilimali za bahari zitakavyotumika kuweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa
wananchi ambao wanategemea bahari kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
"Serikali ya Mama
Samia inakwenda kuondoa hali duni za wavuvi kwa kuwaunganisha na fursa za
kiuchumi zilizopo kwenye ukanda wa bahari ya hindi kwa kushiriki kwenye fursa zilizopo badala ya kutegemea uvuvi pekee" alisema Mhe. Ulega.
Aidha alisema wanataka
watanzania kuhamasika na kuchangamkia fursa za kilimo cha mwani, kunenepesha
kaa, kamba kochi kwani soko la uhakika lipo na Serikali ipo tayari kuwawezesha
kwa mitaji sambamba na vifaa.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya
Pangani Ghaibu Lingo alisema kuwa tayari wameshaanza kunufaika na fursa za
uchumi wa buluu kwa wananchi kuweza kushiriki kwenye shughuli ya kunenepesha
kaa na kufunga miamba kwa ajili ya Uvuvi wa pweza na kisha kuwauza kwa faida
kubwa tofauti na hapo awali.
"Tumeanza hii mbinu ya
kufunga miamba kwa ajili ya Uvuvi wa pweza katika eneo la Ushongo na matokeo
tumeweza kuyaona hivyo tunaiomba Serikali kuweza kuwasaidia wavuvi wa maeneo
mengine kama Kipumbwi na Mkwaja" alisema DC huyo.
Nao wananchi waliipongeza
Serikali kwa kuja na fursa ya uchumi wa buluu kwani unakwenda kusaidia
kubadilisha uvuvi wao wa mazoea na kuwa wa kisasa na wenye tija.
Hamis Ramadhani Mwenyekiti
wa kikundi cha Jifute aliiomba serikali kuwawezesha mitaji pamoja na mashine
kubwa ya kuvutia maji ili waweze kukuza mitaji yao na hivyo kupata faida kubwa.
Nae Burhan Ramadhani
alisema kuwa uvuvi haramu pamoja na ukosefu wa soko imekuwa ni kikwazo kwa
kilimo cha mwani kuweza kufanya vizuri katika maeneo yao hivyo aliiomba wizara
kuona namna ya kuwawezesha vifaa na mitaji.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akieleza umuhimu na faida ya mwani kwa wanakijiji wa
mwandosi wakati wa ziara yake Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, Januari 25, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akimtambulisha mwakilishi kutoka Benki ya kilimo
(TADB), Bw. Furaha Sichula kwa wananchi wa Tanga kueleza namna wanaweza
kunufaika na mikopo kutoka Benki hiyo ya kilimo wakati wa ziara yake Mkoani
humo Januari 25, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akieleza fursa zinazopatikana kutokana na
unenepeshaji kaa wakati wa ziara yake Wilaya ya pangani Mkoani Tanga
alipotembelea kikundi cha Jifute kinachojishughulisha na unenepeshaji huo na
kukabidhi kikundi hicho kwa Benki ya
kilimo (TADB) Ili iweze kutoa mikopo itakayowasaidia kujiendeleza na kujipatia kipato. Januari 25,
2022.
Muonekano wa mabwawa ya
kienyeji ya unenepeshaji kaa yaliyotengenezwa na akina mama na vijana kikundi cha jifute, pangani Mkoani Tanga, januari 25, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni