Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wataalam wa sekta ya Uvuvi kuhakikisha wanakusanya maduhuli ya serikali ili kutimiza lengo la kukusanya bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Waziri Ndaki ameyasema hayo
leo (15.01.2022) kwenye kikao cha wataalam wa sekta ya uvuvi kilichojadili hali
ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia sekta ya uvuvi ambapo mpaka sasa
sekta hiyo imekusanya bilioni 10 kati ya bilioni 40 zilizolengwa.
Katika kikao hicho taarifa za
ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ziliwasilishwa kwa kila kituo ambapo pia
changamoto ziliwasilishwa na kujadiliwa namna gani ya kuweza kukabiliana nazo
ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhili unafikia malengo yaliyowekwa.
Akizungumza na wataalam hao
Waziri Ndaki amesema kuwa ni lazima wataalam kuhakikisha wanaongeza usimamizi
kwenye maeneo yao ili malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yatimie. Ili
kuhakikisha malengo ya ukusanyaji maduhuli yanafikiwa Waziri Ndaki amesema
vituo vitatakiwa kutoa taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli kila wiki ili kama
kunakuwepo na changamoto iweze kutatuliwa kwa wakati.
Lakini pia wataalam wametakiwa
kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea ili kuhakikisha malengo
yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanatimizwa. Waziri Ndaki
amewaeleza wataalam hao kuwa katika muda wao wa utumishi ndani ya sekta ya
uvuvi ni lazima waache alama ikiwemo ya ukusanyaji mzuri wa maduhuli.
Wataalam hao wametakiwa kuwa
wabunifu katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuhakikisha wanasimamia
sheria, kanuni, miongozo na taatibu zilizowekwa. Pia wametakiwa kuhakikisha
kuwa wanalinda na kuzisimamia rasilimali za uvuvi. Vilevile amewaonya wataalam
hao kutojihusisha na uvuvi haramu kwani wakibainika hatua zitachukuliwa dhidi
yao.
Waziri Ndaki amesema kuwa
wizara ina malengo makubwa ya kuwawezesha wavuvi ili wakue kimapato na hivyo
waweze kuchangia kwenye pato la taifa kupitia sekta ya uvuvi. Aidha, amesema
kuwa wizara itafanya mapitio ya tozo mbalimbali za uvuvi na kuzifanyia
marekebisho endapo yatahitajika.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi amesema kuwa lengo la kuitisha kikao
hicho ni kufanya tathmini ya hatua iliyofikiwa katika ukusanyaji maduhuli ya
serikali pamoja na hali ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi.
Pia amemshukuru Waziri kwa
uamuzi wake wa kuitisha kikao hicho kwani kimesaidia kwa kuwawezesha wakuu wa
vituo vyote Tanzania kukaa kwa pamoja kujadili changamoto walizonazo na kutoka
na mkakati wa pamoja ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhuli unakwenda vizuri.
Getrude Migodela kutoka
Kitengo cha Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Mwanza amesema kuwa watakwenda
kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kuhakikisha wanakusanya
maduhuli kulingana na malengo yaliyowekwa. Pia ameishikuru Wizara kwa maelekezo
yake ya kuwataka wafanyabiashara wa samaki na mazao ya uvuvi waanze kulipia kwenye
eneo mzigo unapotoka kwa kuwa hiyo itawasaidia kuongeza mapato kwenye vituo
vyao.
Kikao hicho cha wataalam
kimefanyika kwa lengo la kuwakutanisha wataalam wa uvuvi wanaohusika na
ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili waweze kujadili changamoto na mikakati
itakayowezesha sekta ya uvuvi kutimiza malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya
serikali lakini pia kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi akizungumza wakati wa kikao cha wataalam wa sekta ya uvuvi kilichojadili kuhusu ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Kulia kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma. (15.01.2022)
Mhasibu Mkuu wa Sekta ya Uvuvi, Bw. Lupakisyo Mwakitalima (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye sekta ya uvuvi kwenye kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wataalam wa sekta hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma. (15.01.2022)
Baadhi ya Viongozi na
Wataalam wa Sekta ya Uvuvi wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu
ukusanyaji wa maduhuli kwenye sekta hiyo. (15.01.2022)
Picha ya pamoja ya Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na baadhi ya Viongozi na Wataalam wa
Sekta ya Uvuvi walioshiriki kikao cha kujadili kuhusu hali ukusanyaji wa
maduhuli ya serikali. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini
Dodoma. (15.01.2022)
Picha ya pamoja ya Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi
waliofanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo wote
wamekusanya zaidi ya asilimia 50 ya lengo walilopangiwa. Kulia waliokaa ni
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi na kushoto ni
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala. (15.01.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni