Nav bar

Alhamisi, 13 Januari 2022

WIZARA YAHIMIZA USHIRIKI WA WAZEE WA KIMILA KATIKA ZOEZI LA UTAMBUZI WA MIFUGO KIELEKTRONIKI

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Dkt. Annette Kitambi amewaomba Viongozi wa Vyama vya Wafugaji nchini kufikisha elimu ya utambizi wa mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki kwa wazee wa kimila ili kusaidia kufanikisha zoezi hilo bila vikwazo.

Dkt. Kitambi alitoa rai hiyo  wakati wa kufungua mafunzo ya siku moja ya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki jijini Dodoma Disemba 24,2021.

Alisema katika jamii za wafugaji hasa wamasai wazee wa kimila ndio wenye nguvu na kusikilizwa na vijana na watu wao wanaowaongoza hivyo endapo elimu hiyo itawafikia itasaidia wafugaji hao kutambua mifugo yao kirahisi.

"Chama cha Wafugaji tunawategemea sana kufikisha elimu kwa wafugaji lakini msiwasahau wale wazee maarufu na wazee wa mila kwa sababu akishaelewa akiwaambia watu wa jamii yake wanatekeleza kwa kuwa wanaheshimika", alisema

Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine Wizara ya Mifugo imeweka milango wazi kwa wafugaji kutoa maoni yao juu ya zoezi hilo la utambuzi kwa njia ya kielektroniki hasa wanapo baini kuwepo kwa mapungufu wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga  aliwatoa hofu wafugaji juu ya utekelezaji wa zoezi hilo kwa kuwa limelenga kuweka miundo mbinu bora ya ufugaji hasa swala la malisho.

Alisema changamoto ya malisho imekuwa ikiwasumbua wafugaji wengi na kujikuta wakihama sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu Serikali ilikuwa ikikwamishwa na takwimu zisizo sahihi ambazo zilikuwa zikitolewa awali kulinganisha na uhalisia wa mifugo iliyopo.

"Nataka niwahakikishie wafugaji mara baada ya zoezi hili changamoto ya malisho itaenda kutatuliwa kwa sababu Serikali itakuwa na takwimu sahihi ya mifugo kila sehemu ya nchi kwa hiyo hata migogoro isiyo ya lazima haitakuwepo" alisema

Naye Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Uchumi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Aziza Mumba  alisema kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kutakuwa kumesaidia nchi kuendana na matakwa  ya kidunia ya kutaka mazao yote ya mifugo yatokane na mifugo ambayo imesajiliwa kwa njia ya kielektroniki.


Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uhamasishaji wa zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki Mkoani Dodoma. Disemba 24,2021. 

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama Dkt. Annette Kitambi akieleza lengo na faida ya zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki kwa maafisa Mifugo na maafisa TEHAMA (hawapo pichani) wa Wilaya na Mkoa wa Dodoma, Disemba 24,2021 

 


Afisa kutoka Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  Neema Kelya  akionyesha namna ya kutumia Mfumo wa usajili kwa maafisa Mifugo na maafisa TEHAMA wa Wilaya na Mkoa wa Dodoma  wakati wa kikao cha uhamasishaji wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya kielektroniki , Disemba 24,2021 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni