Serikali ya awamu ya Sita
ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi
(AFDP) imetenga takribani sh Bil 29 mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kuwezesha
kiuchumi shughuli za uvuvi na mikopo kwa wananchi waliopo kwenye sekta hiyo pamoja
na kukuza pato la Taifa.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri wa mifugo na uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega Januari 24, 2022 wakati wa
ufunguzi wa kikao kazi cha mkakati na
kampeni ya kuhamasisha shughuli za ukuzaji
viumbe maji bahari kwa viongozi na
wataalam katika Mamlaka za Serikali za mitaa mkoani Tanga.
Alisema kuwa sehemu ya
fedha hizo takribani sh Bil. 2.1 zinakwenda kukopeshwa kwa vikundi vya wafugaji
wa samaki, wakulima wa mwani,wafugaji wa majongoo bahari, wanenepeshaji wa kamba koche na kaa, katika ukanda wa bahari ya Hindi.
"Tumekutana sisi wataalamu kwa ajili ya
kupeana mbinu na mikakati ya kuweza kuwafikia wananchi ambao ndio walengwa
wakuu wa Mradi huo ili kuona namna ambavyo tutawainua kiuchumi kupitia fursa
zilizoko baharini" alisema Naibu Waziri Ulega.
Alisema kuwa kuna utajiri
mkubwa kupitia fursa ya rasilimali zinazopatikana katika ukanda huu hivyo
Serikali imedhamiria kuinua hali duni za wananchi waishio katika ukanda huo
hivyo wataalam hao wanaweza kusaidia kuwaonyesha wananchi fursa zilizopo.
Aliongeza kuwa Benki ya
kilimo kwa kushirikiana na mabenki mengine ya biashara yaweke mazingira rafiki
ya kutoa mikopo kwa vyama vya ushirika
vya vijana na wanawake Ili waweze kufanya
shughuli za kunenepesha kaa, kamba koche , ufugaji wa samaki, majongoo bahari, na kilimo cha
mwani.
Utolewaji wa mikopo hii pia
iwaguse wavuvi wadogowadogo, mmojammoja au katika vikundi kwani kwa kufanya
hivyo kilio chao cha kutumia fursa hizi za bahari kitakuwa kimesikika.
Awali Mkuu wa Wilaya ya
Tanga Hashim Mgandilwa alisema kuwa Changamoto kubwa iliyopo kwa wavuvi wa ukanda huo ni ukosefu wa viwanda pamoja na
masoko ya uhakika wa mazao ya bahari.
Alisema kuwa kampeni hiyo
itaweza kuleta chachu na maendeleo ya wananchi kwani wataweza kupata fursa
nyingine ya kiuchumi katika maeneo yao kupitia kilimo cha mwani pamoja na
unenepeshaji wa viumbe bahari.
Aidha mwakilishi kutoka
Benki ya kilimo (TADB), Bw. Furaha Sichula amesema kwa mwaka 2021/2022 jumla ya
TSH. 4.827bil zimekopeshwa kwenye Sekta ya Uvuvi ikilinganishwa na mwaka 2020/2021 ambapo kiasi cha Tsh. Bil 1.625
kilikopeshwa.
Nae Mkurugenzi wa ukuzaji
viumbe maji kutoka wizara ya mifugo na uvuvi, Dkt Nazael Madalla alisema kuwa
katika mwaka uliopita uzalishaji wa viumbe vya bahari ulikuwa ni asilimia 11%
pekee.
Kampeni hiyo iliyoanzishwa
na Serikali inakwenda kuwasaidia wananchi
kujikwamua kiuchumi kupitia fursa za bahari.
Kikao kazi hicho kimeazimia
kila baada ya miezi mitatu Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega
atapita kukagua utekelezaji wa mikakati iliyoandaliwa.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiongea na viongozi pamoja na wataalam kutoka mamlaka ya Serikali za mitaa
wa Mkoa wa Tanga (hawapo pichani) wakati
wa ufunguzi wa kikao kazi cha mkakati na kampeni na kuhamasisha shughuli za
ukuzaji viumbe maji bahari. Januari 24, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji
wa Serikali mara baada ya kikao kifupi
juu ya fursa za uchumi wa buluu Mkoani Tanga. Januari 24.2022
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni