Nav bar

Alhamisi, 13 Januari 2022

WALIOVAMIA KARANTINI YA MIFUGO WATAKIWA KUONDOKA KWA HIYARI*

Na Mbaraka Kambona, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Wananchi wakiwemo Wafugaji waliovamia eneo la kuhifadhia na kuiangalia kwa muda Mifugo  inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kuondoka katika eneo hilo kwa hiyari huku akionya kuwa atakayekaidi Serikali itatumia nguvu kuwaondoa.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipotembelea eneo la Karantini ya Kwala iliyopo katika Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 23, 2021. 

Alisema kuwa eneo hilo lina maslahi mapana kitaifa na hivyo wananchi kuvamia na kufanya shughuli zao katika eneo hilo linafanya karantini hiyo kupoteza sifa ya kibiashara kimataifa.

"Hili eneo lina  maslahi ya kitaifa hivyo wananchi walioingia na kukaa huku bila utaratibu wowote tuwaambie waondoke kwa hiyari, wale tutakaowakuta wakati tutakapoanza kazi ya ujenzi wa Karantini ya kisasa basi tutatumia nguvu kuwaondoa", alisema Mhe. Ndaki

Aidha, alisema kuwa mwaka wa fedha ujao watatenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga Karantini hiyo ili iwe ya kisasa itakayokidhi matakwa ya biashara ya kimataifa ya kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi.

"Hatuwezi kwenda kimataifa bila ya  kuwa na kituo hiki, wenzetu wakija hapa ghafla na hali hii watatuambia msiuze Ng'ombe wala Nyama zenu kwa sababu hakuna mahali watakuwa wamehakikishiwa usalama wao", alifafanua

Awali, Mkuu wa Kituo hicho cha Kwala, Dkt. Othman Makusa alimueleza Waziri Ndaki kuwa kituo hicho kina miundombinu duni na kimevamiwa na Wananchi kutoka Vijiji vya jirani na wanafanya shughuli zao mbalimbali ikiwemo Kilimo, Makazi na Ufugaji jambo ambalo linasababisha kituo hicho kupoteza sifa za kimataifa za kuwa Karantini.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi watakwenda kuliainisha eneo hilo vizuri na kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi wataambiwa wahame na maeneo mengine yatabakishwa kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akipatiwa maelezo mafupi kuhusu Karantini ya Kwala na Mkuu wa Kituo cha Karantini hiyo, Dkt. Othman Makusa (kushoto) alipotembelea kuona na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya kujenga Karantini mpya lililopo Mkoani Pwani Disemba 23, 2021. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akikagua eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya kujenga Karantini mpya ya Kwala alipotembelea eneo hilo lililopo katika Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani Disemba 23, 2021. Akiwa katika eneo hilo alisema kuwa wananchi wote waliovamia eneo hilo waondoke kwa hiyari vinginevyo shughuli za ujenzi zitakapoanza wataondolewa kwa nguvu. 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni