WATAALAMU WAJADILI VIGEZO VYA KUTATHMINI UWEZO WA MAABARA ZA MIFUGO TANZANIA BARA NA ZANZIBAR
Na Daudi Nyingo - Kibaha
WATAALAMU wa sekta ya mifugo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamekutana kupitia zana zitakazotumika kutathmini miundombinu na uwezo wa maabara zilizochaguliwa za Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) na Zanzibar kwa lengo la kukubaliana kuhusu vigezo vitakavyotumika na vitakavyoachwa katika tathmini kwa kuzingatia malengo ya Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP).
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika Novemba 9 hadi 11, 2026, katika ukumbi wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Kibaha mkoani Pwani, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutege, amesema tathmini hiyo itasaidia kubaini mapungufu na kupanga vipaumbele vya kuimarisha maabara ili zitambue magonjwa kwa haraka na kuwezesha hatua za udhibiti kuchukuliwa kwa wakati.
“Katika kufanya jambo hili tunategemea angalau mambo matatu: kutokomeza magonjwa yenye athari kwa biashara na afya ya binadamu, kuondoa vikwazo vya kufikia masoko ya kikanda na kimataifa, na kuimarisha uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na matukio yenye athari kwa afya na uzalishaji wa mifugo, ambayo baadaye yanaweza kuathiri afya ya binadamu,” amesema Dkt. Lutege.
“Huwezi kuyafikia haya kama huna maabara yenye uwezo wa kutambua magonjwa kwa haraka. Ukitambua kwa haraka, inakusaidia kuchukua hatua kwa haraka na kuwa na uwezo wa kudhibiti. Tunahitaji kufanya uchambuzi wa kina ili fedha zilizopo ziweze kuziba mapungufu yatakayobainika,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, amesema TVLA na Maabara Kuu ya Veterinari Zanzibar zimehusishwa katika mradi huo ili kuimarisha huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa. Ameeleza kuwa tathmini inayotarajiwa kufanyika itaangalia hali ya maabara hizo, viwango vilivyopo na maeneo yanayohitaji maboresho.
Dkt. Bitanyi amesema wataalamu walioshirikishwa wanatarajia kupitia zana za kutathmini na kuandaa orodha ya vipengele vya ukaguzi itakayoongoza ukusanyaji wa taarifa. Ameongeza kuwa matokeo ya tathmini hiyo yatawawezesha kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuboresha miundombinu na uwezo wa maabara kwa kuzingatia malengo ya mradi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wawakilishi wa TVLA, Ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania Bara, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (ZALIRI), Ofisi ya Lishe ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mifugo Zanzibar kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo. Makubaliano kuhusu zana na vigezo vya tathmini yataweka msingi wa kubaini mahitaji halisi na kupanga maboresho ya huduma za maabara za mifugo Tanzania Bara na Zanzibar.









Maoni
Chapisha Maoni