TDB NA C-SDTP WAENDELEA KUJENGEA UWEZO WADAU WA TASNIA YA MAZIWA SIHA
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Siha, imeendelea kutoa elimu na kujenga uwezo wa wadau wa tasnia ya maziwa ili kuboresha uzalishaji, ukusanyaji, usafirishaji, uhifadhi na usindikaji wa maziwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Oktoba 31, 2026, katika Ukumbi wa Jimboni, Sanya Juu, yalilenga kuwawezesha wadau kuelewa taratibu, kanuni na matakwa ya kisheria yanayosimamia shughuli za tasnia ya maziwa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa TDB, Bi. Neema Moshi, aliwahimiza wadau kujisajili Bodi ya Maziwa kwa mujibu wa Sheria ya Tasnia ya Maziwa, Sehemu ya 17(1), inayomtaka kila anayejihusisha na biashara ya maziwa na bidhaa zake kusajiliwa.
Alieleza kuwa usajili unawezesha Bodi kuwatambua na kuwasimamia wadau kupitia ukaguzi, elimu na ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha maziwa yanazalishwa na kushughulikiwa katika mazingira safi na salama.
Aidha, alieleza kuwa kupitia C-SDTP, TDB inaendelea kushirikiana na Halmashauri katika kuimarisha usimamizi na maendeleo ya tasnia ya maziwa.
Juhudi hizo zinahusisha ukaguzi wa vituo vya kukusanya maziwa, mafunzo kwa wafugaji na wahudumu wa vituo, kuhamasisha kanuni bora za uzalishaji na utunzaji wa maziwa, pamoja na matumizi ya teknolojia zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa mradi pia unachangia kuboresha miundombinu ya vituo vya kukusanya maziwa, upatikanaji wa matanki ya kupoozea maziwa na kuongeza ujuzi wa wadau kuhusu ufugaji bora, lishe ya mifugo, ukamuaji na usindikaji. Hatua hizo zinalenga kuongeza tija na kuimarisha fursa za biashara katika ya Tasnia ya Maziwa.
“Bodi inapowatambua wadau wa maziwa, imekuwa ikiwapatia mafunzo na miongozo kuhusu ufugaji bora, lishe ya mifugo, ukamuaji na usindikaji, pamoja na kuwaunganisha na taarifa za mwenendo wa soko na fursa mbalimbali za biashara,” alisema Bi. Moshi.
Kwa upande wake, Bw. Lucas Kaaya, mzalishaji, mkusanyaji wa maziwa na msindikaji kutoka Kiwanda cha West Kilimanjaro Dairy, aliishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo na kuiomba TDB kuendelea kuyatoa mara kwa mara ili kuwafikia wadau wengi zaidi. Alisema mafunzo hayo yanaongeza ujuzi na maarifa yanayowasaidia kuboresha shughuli zao na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa.
TDB ina mamlaka ya kisheria ya kusimamia na kudhibiti shughuli za ya nchini kwa kuhakikisha wadau wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Hivyo, wadau wote wanahimizwa kujisajili na kuzingatia matakwa ya kisheria ili kuhakikisha maziwa na bidhaa zake zinakidhi viwango vya ubora na usalama, kulinda afya za walaji na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.






Maoni
Chapisha Maoni