SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA WAFUGAJI WANAPATA MITAMBA BORA, YALENGA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZIWA

Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wafugaji wanapata mitamba bora kwa wakati kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato cha wafugaji na kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa nchini, hatua ambayo inatokana na uchambuzi wa mradi huo, ambapo upatikanaji wa mitamba bora uliainishwa kuwa eneo linalohitaji hatua za haraka, na serikali imebainisha kuwa bado kuna haja ya kuhakikisha mitamba inawafikia wafugaji kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi leo Novemba 10, 2026 jijini Dodoma katika kikao kilichowakutanisha wadau wa sekta ya mifugo, taasisi za fedha, wamiliki wa mashamba binafsi, wasindikaji wa maziwa pamoja na taasisi za utafiti, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele amesisitiza umuhimu wa wadau hao kushirikiana kuondoa vikwazo vinavyochelewesha upatikanaji wa mitamba.

“Katika utekelezaji wa mwaka huu serikali imepanga kuanza na mitamba 405, huku mitamba 56 yenye mimba kutoka mashamba ya serikali ikitarajiwa kukabidhiwa kwa wanufaika kabla ya Desemba 15, 2026 na kupitia mradi huo, takribani Shilingi bilioni 26 zimeelekezwa TADB kwa ajili ya mtaji wa dirisha la mikopo ya mitamba, na serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 6.25 katika kuimarisha huduma za uhimilishaji, ikiwemo ununuzi wa madume bora 10 ya mbegu, mitambo tisa ya maabara, mitambo miwili ya kuzalisha hewa ya naitrojeni ya kimiminika na vifaa vya kuanzia kazi kwa wataalamu 60 wa uhimilishaji” amesema Dkt. Madele

Aidha, Dkt. Madelea amesema katika kuharakisha utekelezaji huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameelekeza wizara kuunda timu ya pamoja ya kiufundi ambayo ndani ya siku 14 itakamilisha mfumo wa viwango vya ubora wa mitamba, bei elekezi, ratiba ya upatikanaji na masharti ya mikopo, TADB kukamilisha makubaliano na benki washirika ili dirisha la mikopo lifunguliwe kabla ya mwisho wa Desemba 2026, huku TALIRI na NAIC zikitakiwa kuwasilisha ndani ya siku 30 mpango wa kuongeza uzalishaji wa mitamba bora nchini kwa kutumia teknolojia ya upandikizaji wa viinitete na mbegu zilizochaguliwa jinsia, ambapo lengo kuu ni kuhakikisha mitamba bora inawafikia wafugaji, uzalishaji wa maziwa unaongezeka na kipato cha kaya kinaboreshwa, kwa kuzingatia kugeuza wingi wa mifugo nchini kuwa tija ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo wa C-SDTP, Dkt. Lazaro Kapella amesema serikali kupitia Mradi huo inaendelea kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya mifugo, ambapo Mradi umeazimia kuja na kikao cha leo ikiwa na lengo la kuwaunganisha wafugaji na wazalishaji wa ng’ombe bora, wakiwemo wanaoagiza mifugo hiyo kutoka nje ya nchi, ili kurahisisha upatikanaji wa ng’ombe wenye sifa na tija katika uzalishaji, na kupitia mpango huo, wafugaji watawezeshwa kupata taarifa, ramani na anuani za wazalishaji kulingana na aina ya ng’ombe wanaohitaji, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa mifugo bora na kuongeza ufanisi katika shughuli za ufugaji.

Naye, Mbunge wa jimbo la Nzega Mjini, Mhe. Hussein Mohamed Bashe amesema ni vyema Mradi huo kuangalia ni namna gani wanaweza kuwekeza katika teknolojia na kuhakikisha Tanzania inakuwa na vituo bora vya uhimilishaji ili kuzalisha mbegu bora zaidi katika Mifugo, kutatua changamoto mbalimbali za wafugaji ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti ambazo zitaleta tija katika Sekta.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ranchi ya Mbogo, Bw. Naweed Mulla amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali wafugaji na kuwaletea Mradi huo wa C-SDTP ambao utaenda kuongeza tija katika sekta ya mifugo hususan katika kuwawezesha wafugaji kupata mbegu bora ya ng’ombe.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, akihutubia wadau wa Sekta za Mifugo, katika kikao cha Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP) kilichoshirikisha taasisi za fedha, wazalishaji na wauzaji wa mitamba ya ng’ombe wa maziwa, kilichoofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 10, 2026, Dodoma.

Mkurugenzi msaidizi hakimiliki za waboreshaji mbari na maendeleo ya kosaafu za wanyama Bw. Jeremiah Temu, akizungumza na wadau wa Sekta za Mifugo, katika kikao cha Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP) kilichoshirikisha taasisi za fedha, wazalishaji na wauzaji wa mitamba ya ng’ombe wa maziwa, kilichoofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 10, 2026, Dodoma.

Mratibu wa Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP), Dkt. Lazaro Kapella, akielezea lengo la kikao hicho kilichowakutanisha taasisi za fedha, wazalishaji na wauzaji wa mitamba ya ng’ombe wa maziwa, kilichoofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 10, 2026, Dodoma.

Mratibu wa Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP), Dkt. Lazaro Kapella, akitoa wasilisho kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mradi, katika kikao cha Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP) kilichoshirikisha taasisi za fedha, wazalishaji na wauzaji wa mitamba ya ng’ombe wa maziwa, kilichoofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 10, 2026, Dodoma.

Mbunge wa jimbo la Nzega Mjini, Mhe. Hussein Mohamed Bashe, akisikiliza mawasilisho mbalimbali kutoka kwa wadau wa Sekta ya Mifugo, katika kikao cha Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP) kilichoshirikisha taasisi za fedha, wazalishaji na wauzaji wa mitamba ya ng’ombe wa maziwa, kilichoofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 10, 2026, Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (aliyekaa katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Sekta ya Mifugo, katika kikao cha Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi (C-SDTP) kilichoshirikisha taasisi za fedha, wazalishaji na wauzaji wa mitamba ya ng’ombe wa maziwa, kilichoofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 10, 2026, Dodoma.










Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI