SERIKALI KUENDELEA KUUNGANISHA NGUVU KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI KWA MIFUGO
Serikali imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji ili kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji kwa mifugo inatatuliwa nchini, kauli ambayo imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kiteto, Mhe.Edward Kisau Olelekaita, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuunganisha nguvu za wizara hizo katika kuboresha miundombinu ya maji katika Jimbo la Kiteto.
Akijibu swali katika Kikao cha Bunge la kumi na tatu, mkutano wa tano, kikao cha sita, leo Novemba 3, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, swali la Mhe. Olelekaita aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha mradi wa bwawa la maji ya mifugo la Kiwani, lililopo Kata ya Ndeda, Wilaya ya Kiteto, Mhe. Kamani alisema Serikali inatambua umuhimu wa mradi huo katika kuboresha upatikanaji wa maji kwa mifugo na wananchi, na kwamba mradi huo utaendelea kuzingatiwa katika mipango ya bajeti ya Wizara ili ujenzi wake uweze kukamilika.
Aidha, Mhe. Kamani alisema Serikali tayari ina utaratibu wa kuunganisha nguvu za wizara mbalimbali katika kupanga bajeti na kuendeleza miundombinu ya maji, huku akieleza kuwa ushirikiano huo unatokana na Azimio la Mawaziri lililofikiwa jijini Mbeya mwaka 2022, lililowahusisha mawaziri wa wizara tisa, zikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Maji, Nishati, Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TAMISEMI.
Mhe. Kamani alisema kupitia azimio hilo, wizara hizo zimekubaliana kushirikiana katika kupanga bajeti na kuendeleza miundombinu ya maji kwa manufaa ya watumiaji wote, wakiwemo wafugaji na wakulima, na alitolea mfano wa visima viwili vilivyojengwa na Wizara ya Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa ajili ya wakulima, pamoja na visima 18 vilivyojengwa na Wizara ya Maji katika eneo la Mtorofu, Morogoro, kwa ajili ya matumizi ya wafugaji.
Mhe. Kamani aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya Sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuhimiza matumizi ya mitambo ya uchimbaji visima na vifaa vya ujenzi wa mabwawa vilivyosambazwa nchini ili viweze kunufaisha pia sekta ya mifugo, na alisisitiza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kushirikiana na wizara nyingine kuhakikisha changamoto ya maji kwa wafugaji inashughulikiwa, ikiwemo katika Wilaya ya Kiteto.



Maoni
Chapisha Maoni