MKAKATI WA AFYA, USTAWI WA VIUMBE MAJI WAANDALIWA
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya ufadhili wa Shirika lisilo la Serikali la OHDI imeandaa mkakati wa kuratibu afya na ustawi viumbe maji ikiwa unaolenga kulinda afya ya walaji pia.
Akizungumza katika uzinduzi wa rasimu ya mkakati huo uliofanyika Oktoba 29,2026 jijini Dar-es-Salaam Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ulimwenguni ambazo zina ithibati ya kusafirisha samaki kwenye masoko makubwa na mpaka sasa hakuna tatizo lolote lililoripotiwa kutokana na changamoto ya afya ya samaki kwa binadamu.
“Ni matumaini yetu kuwa mkakati huu unaongeza thamani kwenye mnyororo wa biashara ya samaki na mazao yake kwani Serikali ina mategemeo makubwa katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji na tunaamini itatusaidia kupunguza upungufu wa mahitaji ya samaki uliofikia karibu asilimia 50 mpaka sasa ” Amesema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji nchini Dkt. Nazael Madala amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa wa uwekezaji kwenye upande wa tasnia ya viumbe maji nchini ambapo amesisitiza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ili uzalishaji unapoongezeka uguse mpaka katika masoko ya nje.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wakuzaji Viumbe maji Tanzania, Katibu wa chama hicho Bw. Jofrey Rucho ametoa rai kwa wadau wote wanaohusika kuandaa mkakati huo kutumia nguvu kubwa ya kuhakikisha unakuwa ni msaada kwa wakuzaji viumbe maji wote nchini bila kujali mahali walipo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la OHDI Bi. Julie Bwoga amesema kuwa shirika lake litaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za Serikali katika kukuza afya za viumbe maji nchini na ustawi wao kwa ujumla.






Maoni
Chapisha Maoni