MAFUNZO YA TDB YAIBUA UWEZO MPYA KWA WADAU WA MAZIWA MUFINDI

Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), imeendelea kuwajengea uwezo wadau wa mnyororo wa thamani wa maziwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, kwa kuwapatia elimu na ujuzi wa vitendo kuhusu ubora na usalama wa maziwa.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Novemba 4, 2026, yalilenga kuwawezesha wadau kutumia kanuni bora za usafi katika uzalishaji na ushughulikiaji wa maziwa, pamoja na kujifunza mbinu rahisi za kupima na kuhakiki ubora wake.

Afisa  Mtekinolojia wa Chakula kutoka TDB Bw. Israel Mwingira aliwaongoza washiriki katika mafunzo ya vitendo kuhusu namna ya kutambua ubora wa maziwa na kuzingatia taratibu za usalama katika shughuli zao za kila siku.

Katika sehemu nyingine ya mafunzo, Mwanasheria wa TDB Wakili Msomi Haruna Maarufu alitoa ufafanuzi kuhusu sheria inayoipa Bodi mamlaka ya kusimamia na kudhibiti Tasnia ya Maziwa nchini.

Aliwakumbusha washiriki kuhusu wajibu wa kisheria wa kujisajili TDB kwa kila mtu anayejihusisha na shughuli yoyote katika mnyororo wa thamani wa maziwa, akisisitiza kuwa usajili ni takwa la kisheria linalopaswa kuzingatiwa na wadau wote.

Kwa upande wao, washiriki walieleza kuridhishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewaongezea uelewa na ujuzi wa vitendo kuhusu namna ya kuzalisha, kuhakiki na kushughulikia maziwa kwa kuzingatia ubora na usalama. 

Pia waliipongeza TDB kupitia C-SDTP kwa kuwafikia na kuwajengea uwezo, wakieleza kuwa maarifa waliyopata yatawasaidia kuboresha shughuli zao na kuongeza thamani ya maziwa.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TDB kupitia C-SDTP za kuimarisha uwezo wa wadau, kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazozingatia mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku yakilenga kuhakikisha upatikanaji wa maziwa salama na yenye ubora kwa ajili ya kulinda afya za walaji na kukuza Tasnia ya Maziwa nchini.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI