KATIBU MKUU BI. AGNES MEENA, AKUTANA NA NAIBU WIZARA YA BAHARI NA UVUVI WA KOREA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amekutana na Bw. Seo Jeong-ho, Naibu Waziri anayeshughulikia Sera katika Wizara ya Bahari na Uvuvi ya Jamhuri ya Korea, pembezoni mwa Jukwaa la Bahari la Dunia.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Novemba 07, 2026 Nchini Korea, Bi. Meena aliishukuru Serikali ya Korea kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ya Uchumi wa Buluu kupitia Hati ya Makubaliano iliyosainiwa kati ya Wizara hizo mbili.
Pia, aliishukuru Serikali ya Korea kwa kuwezesha mradi wa Kituo cha Matumizi ya Satelaiti katika Usimamizi wa Bahari na Uvuvi kinachowekwa katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), pamoja na mafunzo ya kuwajengea uwezo Watanzania katika matumizi ya taarifa za satelaiti kwa usimamizi wa bahari na rasilimali za uvuvi, pia aliwasilisha hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya ujenzi wa Bandari Janja ya Uvuvi Bagamoyo na kuiomba Serikali ya Korea kuendelea kushirikiana na Wizara katika kukamilisha upembuzi yakinifu na ujenzi wa bandari hiyo.
Katika hatua nyingine Bi. Meena aliwasilisha Andiko Dhana la mradi wa Maabara ya Taifa ya Ubora wa Samaki, itakayosaidia kuhakikisha mazao ya uvuvi yanayopitia bandarini hapo yanakidhi viwango vya usalama na ubora kwa walaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Bahari na Uvuvi wa Korea aliahidi kulipa kipaumbele andiko la mradi wa Maabara ya Ubora wa Samaki na kuendelea kuwezesha hatua za utekelezaji wa Bandari Janja ya Uvuvi Bagamoyo, ikiwemo upembuzi yakinifu.
Katibu Mkuu yupo nchini Korea kwa mwaliko wa Wizara ya Bahari na Uvuvi kuhudhuria Jukwaa la Bahari la Dunia, akiwa ameambatana na viongozi na wataalamu kutoka TAFIRI na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Maoni
Chapisha Maoni