DKT. BASHIRU AITAKA LITA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA KUFANYA MAGEUZI SEKTA YA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kisekta ili kufanya mageuzi katika sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma ya mafunzo ya Mifugo nchini.

Akizungumza leo Novemba 7, 2026, jijini Dodoma, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya LITA na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, Dk. Bashiru amesema ni muhimu sana kuongeza ushirikiano na sekta binafsi katika kuhamasisha vijana na wanawake kuwekeza kwenye sekta ya mifugo, huku akibainisha kuwa ushirikiano wa taasisi hiyo na taasisi zingine kama kampuni ya AKM Glitters ni miongoni mwa hatua za kufikia azma hiyo. 

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza na maagizo hayo yanasimamiwa na Mhe. Waziri Mkuu kwamba wizara za kisekta zisifanye kazi kwa kutengana bali zifanye kazi kama timu moja" amesema Dkt. Bashiru 

Aidha, Dkt. Bashiru ameielekeza LITA kuwa inapaswa kushirikiana na sekta binafsi na kutumia maeneo ya uwekezaji kama vituo vya mafunzo kwa vitendo, huku wanafunzi na wakufunzi wakiongeza huduma za ushauri kupitia programu za mafunzo na ziara za uwandani. 

Vilevile, Dkt. Bashiru ameisisitiza LITA na taasisi zingine zilizopo chini ya wizara juu ya umuhimu wa kulinda maeneo yao dhidi ya uvamizi, na kuboresha miundombinu mbalimbali, kutoa mafunzo kwa wafugaji na kuongeza kasi ya kuwafikia wafugaji, hususan waishio vijijini, ambao kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa wanaunda asilimia 62 ya kaya zinazofuga mifugo nchini.

Dkt. Bashiru amewataka wajumbe wa bodi hiyo walioteuliwa kwa kipindi kingine cha miaka mitatu kutumia uzoefu, weledi na uadilifu wao kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu ya LITA, kusimamia utoaji wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, huduma za ushauri kwa wafugaji, tafiti tumizi pamoja na uzalishaji wa mbegu bora za mifugo na malisho, na umuhimu wa kuweka mipango madhubuti ya uwekezaji inayoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele amesema ni wajibu wa Bodi kuhakikisha inaweka mikakati katika kufikia azma iliyowekwa na kuhakikisha LITA inatoa mchango mkubwa katika sekta ya Mifugo pamoja na kutoa ushauri namna ya kuendesha Mafunzo ya Mifugo nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya LITA ambaye pia ni Mkurugenzi Mkaazi wa Heifer International Tanzania, Bw. Mark Tsoxo, ameishukuru Wizara kwa kuaminiwa na kuweka bayana kuwa wao kama wajumbe wa Bodi wameipokea dhamana hiyo waliyopewa na wizara na kuahidi ushirikiano na kuwajibika kikamilifu hasa katika kuishauri wizara pamoja na LITA katika kufanya mageuzi katika Sekta ya Mifugo ili kukuza uchumi wa wafugaji na wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya LITA, Dkt. Pius Lazaro Mwambene, amesema LITA ina mpango wa kuongeza vyuo kumi ili kuendelea kutoa mafunzo ya ufugaji kwa wananchi na vilevile inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na za serikali katika kuhakikisha sekta ya Mifugo inakuwa zaidi na kuongeza tija katika uzalishaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akihutubia wadau wa Sekta za Mifugo, katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, uliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, akizungumza na wadau wa Sekta za Mifugo, katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, uliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto), akimkabidhi nyaraka za utendaji kazi Mwenyekiti wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkaazi wa Heifer International Tanzania, Bw. Mark Tsoxo (kulia), katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi hiyo na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, uliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Lazaro Mwambene (aliyekaa kulia akisaini), akisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi wa Kampuni AKM Glitters Co. Ltd, Bi. Elizabeth Swai (aliyekaa kushoto akisaini), katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya LITA na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, uliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Lazaro Mwambene (kulia), na Mkurugenzi wa Kampuni AKM Glitters Co. Ltd, Bi. Elizabeth Swai (kushoto), wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano mara baada ya kuisaini, katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya LITA na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, uliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.

Picha ni wadau mbalimbali wa Sekta ya Mifugo wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (aliyesimama kushoto), katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya tano ya ushauri ya Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi hiyo na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya LITA na AKM Glitters, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema - Kisasa, Novemba 7, 2026, Dodoma.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI