BENKI YA DUNIA YAENDELEA KUUNGA MKONO MRADI WA TASFAM

Na. Edward Kondela

Ujumbe kutoka Benki ya Dunia umeendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Bahari Tanzania (TASFAM) ili kuhakikisha mradi huo unawafikia walengwa.

Ujumbe huo ukiongozwa na Bw. Mirko Ivo Serkovic umekutana na uongozi wa TASFAM jijini Dar es Salaam Oktoba 27, 2026 katika makao makuu ya ofisi ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na kupeana mrejesho wa hatua ambazo zimefikiwa na ambazo zinatarajiwa kufikiwa ili kuhakikisha mradi huo wa miaka mitano (2025-2030) unafikia malengo.

Aidha, katika kikao hicho Mratibu wa Mradi wa TASFAM Tanzania Bara Dkt. Nichrous Mlalila ameuhakikishia ujumbe wa Benki ya Dunia kuwa jitihada zinafanywa kuhakikisha mipango yote inatekelezwa na hatimaye mradi ufikie malengo yaliyokusudiwa na kuacha alama kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji katika mikoa ya Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Awali ujumbe wa Benki ya Dunia ulipata fursa kutembelea Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Pangani, kwenye Kijiji cha Ushongo na kukutana na kamati ya kushughulikia malalamiko ngazi ya kijiji kuona muundo wake pamoja na kufahamu majukumu yao pamoja na kujionea eneo la mradi kutakapojengwa kituo cha taarifa.

Kuhusu zao la mwani katika Wilaya ya Mkinga, ujumbe wa Benki ya Dunia umekutana na wananchi wa Kijiji cha Ndumbani, viongozi wa serikali ya kijiji, maafisa uvuvi, waratibu wa Mradi wa TASFAM kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na kutembelea ofisi za Hifadhi ya Silikanti iliyopo Kigombe Halmashauri ya Muheza na Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kwenye Mialo (BMU).

Katika Mkoa wa Pwani, ujumbe wa Benki ya Dunia umekutana na uongozi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Mradi wa TASFAM. 

Katika mradi huo FETA imewezesha mafunzo ya muda mfupi kwa mabaharia na waendeshaji wa vyombo baharini juu ya usalama majini, mafunzo ya uchakataji mazao ya uvuvi na mwani yamefanyika pamoja na kuwezesha zoezi la uhuishaji wa mitaala mitano na uanzishwaji wa mitaala mipya 12.

Aidha, imewezesha mafunzo ya matengenezo na utunzaji wa boti na injini za uvuvi kwa washiriki 40 kutoka Mikoa ya Tanga na Lindi.

Miongozo minane ya mafunzo ya muda mfupi imeandaliwa, mitaala kwa ajili ya mabaharia STCW imeandaliwa, watumishi wamejengewa uwezo kupata mafunzo mbalimbali hususan matumizi ya vifaa vya maabara.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza Mradi wa TASFAM katika mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara iliyopo katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia.







Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI